Serikali yajiwekea mikakati kuongeza mapato ya utalii kutoka China
- Serikali imesema licha ya msoko ya asili, nguvu kubwa inaelekezwa kutumia watalii kutoka nchi za China, Israel, Oman, Russia na Australia.
- Wasafiri kutoka China wanaongoza kwa matumizi ya pesa na muda wakati wakiwa katika shughuli za utalii duniani.
- Bara la Afrika litaendelea kushuhudia ongezeko la watalii kutoka China ambao wanavutiwa na mandhari nzuri na shughuli za kitamaduni.
Dar es Salaam.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla amesema China imewekwa katika kundi la masoko ya kimkakati ili kuongeza mapato na idadi ya watalii kutoka nchi hiyo wanaotembelea vivutio mbalimbali vilivyopo Tanzania.
Katika soko hilo la kimkakati China imewekwa katika kundi moja na nchi za Israel, Oman, Russia na Australia ambazo zimekuwa na mafungamano ya muda mrefu na Tanzania katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Ukiachilia mbali masoko ya asili ya utalii ambayo Tanzania imekuwa ukiyategemea, Dk Kigwangalla alieleza kwenye ukurasa wake wa Twitter Februari 13, 2019 kuwa wameamua kuelekeza nguvu katika masoko mengine ambayo yanaweza kuleta matokeo makubwa zaidi.
“Katika masoko yetu makubwa ya kimkakati, Israel ni mojawapo. Ukiacha masoko traditional (asili) kama Marekani, Ujerumani, Uingereza, Italia na ufaransa, tumeamua kuwekeza kwa nguvu zaidi na kimkakati zaidi kwenye soko la Israel, China, Oman (Gulf countries), Russia na Australia,” inasomeka sehemu ya ujumbe huo.
Januari 19 mwaka huu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema wamejipanga kupokea kundi la watalii wasiopungua 300 kutoka China ambao wanatarajiwa kuwasili nchini Machi, mwaka huu.
Watalii hao ni kundi la kwanza miongoni mwa watalii 10,000 wanaotarajiwa kuwasili nchini katika mwaka 2019 chini ya mpango unaosimamiwa baina ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na kampuni ya TouchRoad International Holding Group ya China.
“Tanzania imeamua kuweka mkakati wa kuongeza idadi ya watalii nchini kwa kuboresha miundombinu ya usafiri na kukuza utalii kupitia vivutio vya vyakula vya asili, mavazi ya asili, wanyama, fukwe za bahari na milima. Kwa hiyo, ujio wa kundi hili kubwa, unatoa fursa mpya ya kutangaza vivutio vya nchi yetu,” alisema Majaliwa alipokutana na Mwenyekiti wa Touchroad Group, Liehui He jijini Dodoma.
Katika kuhakikisha fursa ya watalii kutoka China inatumiwa vizuri, He alisema wameweka lengo la kuongeza idadi ya watalii kwa asilimia 20 kila mwaka kwa muda wa miaka mitano ambapo ndege za Air Tanzania zitasaidia kuchochea idadi ya wageni hao kuja nchini.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mwenyekiti wa Kampuni ya Touchroad Group ya China, He Liehui, ofisini kwa Waziri Mkuu, jijini Dodoma, Januari 19, 2019. Lengo lilikuwa kuangalia namna kampuni hiyo inaweza kusaidia kuongeza idadi ya watalii. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kwanini soko la kimkakati la China?
Kwa mujibu wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO), wasafiri kutoka China wanaongoza kwa matumizi ya pesa na muda wakati wakiwa katika shughuli za utalii duniani ambapo mwaka 2017 pekee walitumia Dola za Marekani 258 bilioni.
Hali inasadifu kidogo hata nyumbani Tanzania baada ya Ripoti ya utafiti wa wageni wa nje ya nchi mwaka 2017 (International Visitors’ Exit Survey Report 2017) kubainisha kuwa watalii kutoka China ni wa pili kwa kutumia fedha nyingi kwa siku wakiwa nchini baada ya Wamarekani.
Wachina wanatumia Dola za Marekani 277(Sh635,000) kwa siku ikilinganishwa na wastani wa matumizi ya Dola za Marekani 161(Sh369,000).
Matumizi hayo yanafanyika zaidi Afrika kutokana na urahisi wa upatikanaji wa visa, vivutio vingi vya kitamaduni na kihistoria. Hali hiyo imeifanya Afrika kuwa kivutio kikubwa kwa watalii kutoka China.
Zinazohusiana:
- Serikali kuwabana wanaopangisha nyumba kwa watalii bila leseni.
- Tamasha la Urithi Festival kufanyika mikoani kila mwaka.
- Tanzania yaangazi masoko 18 kukuza utalii duniani
Jambo la kuvutia katika nchi za Afrika ni kuanzishwa kwa visa zenye masharti rahisi kwa raia wa China. Kwa mujibu wa Kampuni ya usafiri ya ForwardKeys, baada ya Morocco na Tunisia kurahisisha upatikanaji wa visa, kumekuwa na ongezeko la asilimia 240 na 378 ya wasafiri wa China walioingia katika nchi hizo.
Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Jukwaa la usafiri duniani la Travelzoo umebaini kuwa bara la Afrika limekuwa chagua la kwanza la mapumziko ya watalii wa China kwa mwaka 2018 na kuzipiku nchi za Japan na Australia.
Watalii hao hutembelea zaidi nchi za Morocco,Tunisia, Afrika Kusini, Namibia, Madagascar na Tanzania. Mwaka huu, nchi jirani ya Kenya imezindua kampeni ya masoko kuifikia China ikitarajia kuwapata wageni 53,000 kutoka China ambao tayari walitembelea nchi hiyo mwaka uliopita.
Travelzoo wanaeleza kuwa bara la Afrika litaendelea kushuhudia ongezeko la watalii hasa kutoka China ambao wanavutiwa na mandhari nzuri na utamaduni.
Watalii kutoka China ni mfano mzuri wa jitihada za China kuchangia ukuaji wa uchumi wa Afrika hasa Tanzania ambayo imekuwa mshirika muhimu wa maendeleo wa China katika sekta za ujenzi, elimu, afya, miundombinu ambazo zimetengeneza ajira na kukuza ujuzi na teknolojia kwa wananchi.