Makonda aomba radhi kwa adha ya usafiri wakati mwili wa Ruge ukiwasili Dar

March 2, 2019 6:28 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Adha ya foleni kubwa ya magari ilijitokeza jana wakati msafara wa marehemu alipokuwa unapita katika barabara za Jiji.
  • Amesema haikuwa nia yake hadha hiyo itokee kwasababu msiba hauvumiliki na hauna uzoefu.
  • Amesema atatafuta namna ya muenzi Ruge katika mkoa wake kwa sababu alikuwa ni zaidi ya rafiki.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewaomba radhi wananchi wa mkoa huo kwa mateso na adha waliyoipata wakati wanaupokea mwili wa marehemu Ruge Mutahaba kutoka uwanja wa kimataifa wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) hadi walipouhifadhi katika hospitali ya jeshi ya Lugalo. 

Ruge alifariki Februari 26 mwaka huu wakati akipatiwa matibabu huko nchini Afrika Kusini na mwili wake uliwasili jana jijini Dar Salaam ambapo msafara wa viongozi na wanafamilia waliokwenda kumpokea uwanja wa ndege ulisababisha baadhi ya barabara kufungwa kwa muda na foleni za magari.

Makonda aliyekuwa akizungumza leo (Machi 2, 2019) wakati wa kutoa salamu za mwisho kwa marehemu katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam, amesema haikuwa nia yake kuwatesa wakazi wa mkoa huo kutokana na usumbufu wa foleni za magari na mapokezi hayo.

“Niwaombe radhi wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kwa mateso na adha waliyoipata jana wakati tunampokea ndugu yetu, kaka yangu kutoka Airport mpaka tunamfikisha Clouds hatimaye tunamfikisha tulipomuhifadhi pale Lugalo,” amesema Makonda na kuongeza;

“Haikuwa nia yangu kuwateseni kwenye foleni, natamani sana nami niwe na namna fulani ya kumuenzi kaka yangu ndani ya mkoa ameacha alama kubwa na kuleta matokeo kwa watanzania na vijana.”

Amesema kutokana na mchango aliouacha Ruge katika jamii atatafuta namna yake ya kumuenzi katika mkoa huo kwasababu alikuwa ni zaidi ya rafiki yake ambaye walikuwa wanashirikiana katika mambo mengi ambayo yalikuwa hayajulikani katika vyombo vya habari.

“Jana wakati tunajadiliana habari ya kutoa salamu za rambirambi, kwangu nilikuwa na wakati mgumu sana. Wakati mgumu kwasababu Ruge ni zaidi ya rafiki kwangu na familia inajua namna gani tulikuwa karibu pamoja na hata kuendelea kushirikishana mambo ambayo hayana sababu ya kwenda kwenye vyomba vya habari,” amesema Makonda.


Soma zaidi: 


Hata alipopewa nafasi ya kuongea leo wakati wanamuaga marehemu Ruge, Makonda amesema hana neno la kuongea kwa sababu amemsihii sana Mungu usiku wa jana ampe neno lakini mpaka inafika leo asubuhi hajapata neno la kuongea na akipata kibali kwa Mungu ataongea wakati ujao.

“Mpaka leo nimefika hapa asubuhi sina cha kusema, zaidi nimemsihi sana Mungu nipatie angalau neno moja la kusema mbele za watu juu ya wema na uaminifu na mapenzi mema aliyokuwanayo Ruge kwangu lakini bado Mungu hajanipa cha kusema.

“Naendelea kumuamba akinipa cha kusema kwa sababu bado tuko wote hata kule Bukoba na hata kama sio huko pale Mungu akinipa kibali cha kusema atanipa neno la kusema,” amehitimisha Makonda na kurudi kukaa.

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais John Magufuli, waombolezaji wamemuelezea kwa undani marehemu huku wengi wakiguswa na ujasiri na uthubutu alikuwa nao katika kuchangamkia na kuwafungulia fursa vijana katika jamii.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira, January Makamba amesema Ruge ameyaishi maisha ambayo aliandika bango lake vizuri kwa sababu alikuwa na masikio ya kumsikiliza kila mtu ambapo ni tofauti na viongozi wengi ambao wanajificha kwa kisingizio cha muda kuwakwepa wanadamu wenzao.  

“Ruge alikuwa mwalimu wangu. Alinifundisha kwamba sisi tulio na dhamana tukitoa kauli ina maana kubwa sana…alinifundisha uzito wa kauli,” amesema Makamba na kuongeza;

“Nimemfahamu Ruge Mutahaba kwa muda wa miaka 20, hahitaji kupewa sifa za marehemu ila maisha yake yanajieleza, msiba wake umenichoma sana.”

Naye Mbunge wa Mikumi na Msanii wa muziki Joseph Haule maarufu kama Profesa Jay amesema alikutana na marehemu Ruge mwaka 1999 siku ambayo walikuwa wanarekodi wimbo wa ‘Chemsha Bongo ambapo tangu hapo walikuwa wakishirikiana katika shughuli mbalimbali za muziki. 

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amesema alimfahamu Ruge kwa ubunifu  na uwezo wake kuendesha mambo hasa katika tasnia ya habari na muziki.

Amesema haoni sababu ya kumjengea mnara wa chokaa kwasababu tayari amejenga mnara katika mioyo ya watu ambao hauwezi kuvunjika kwa miaka ijayo kuhusu mchango wake.

Shughuli ya kumuaga marehemu Ruge imehitimishwa hapa jijini na jumatatu ya Machi 4, 2019 atapumzishwa katika nyumba yake milele huko Bukoba mkoani Kagera.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV