Nukta Africa kuwakutanisha wadau wa habari, teknolojia ‘Wiki ya Ubunifu’ Dar
- Mkutano huo utafanyika Machi 27, 2019 katika ukumbi wa Rotunda uliopo katika jengo la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
- Utakuwa ni miongoni mwa mikutano katika ya Wiki ya Ubunifu itakayofanyika Machi 25 hadi 30, 2019 takuwa na mjadala wa wazi kuhusu mchango wa vyombo vya habari kukuza katika ubunifuTanzania na ni sehemu
Dar es Salaam. Kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa imeandaa mkutano utakaowakutanisha wadau wa habari, mawasiliano na teknolojia kujadili mchango wa vyombo vya habari kukuza ubunifu Tanzania.
Mkutano huo, utakaofanyika Machi 27, 2019 Saa 2.30 hadi 4:30 asubuhi katika ukumbi wa Rotunda uliopo Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Kijitonyama jijini Dar es Salaam, ni miongoni mwa matukio ya Wiki ya Ubunifu (Innovation Week 2019) itakayofanyika kuanzia Machi 25 hadi 30, 2019.
Wiki ya Ubunifu huandaliwa na Mfuko wa Ubunifu na Maendeleo ya Watu (HDIF) kwa kushirikiana na wadau wengine kama Costech ambapo inalenga kuwaleta pamoja wote wenye miradi ya ubunifu na wale ambao wanaweza kuwawezesha.
Katika wiki hiyo mambo kama vile mafanikio na changamoto mbalimbali katika eneo la ubunifu huzungumzwa kwa uwazi na wabunifu huonyesha kazi zao walizozifanya katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa Nukta Africa, Nuzulack Dausen amesema mkutano huo utahusisha mjadala wa wazi wa nini kifanyike kuhakikisha vyombo vya habari vina kuwa sehemu ya kukuza na kuendeleza ubunifu wa teknolojia nchini.
“Mjadala huo utaianisha fursa zilizopo kwa pande zote mbili za wabunifu na vyombo vya habari katika kuhakikisha kila upande unakua na unachochea maendeleo,” amesema Dausen.
Dausen amesema mkutano huo pia ni fursa kwa wanahabari, wahariri, wabunifu na watunga sera kukaa meza moja kujadili mbinu rafiki zitakazosaidia kukua kwa kasi kwa ubunifu nchini.
“Tunaamini baada ya mjadala huo wa Machi 27, 2019 utakuwa ni chachu ya kutangaza mambo makubwa ya kiubunifu yanayofanywa nchini lakini kukosoa pale wabunifu wa teknolojia wanapoteleza katika kazi zao ili kuleta kilicho bora zaidi, ” amesema Dausen ambaye amekuwa akiripoti habari za teknolojia nchini kwa miaka saba sasa.
Soma zaidi:
- NALA yaja na teknolojia ya kijanja kutuma, kupokea pesa
- Wanafunzi kubadilishana uzoefu maonyesho ya teknolojia Dar
Amewasihi wadau wote wanaopenda ubunifu nchini kujisajili bure na kuhudhuria mkutano huo ambao ni chachu ya mahusiano mazuri katika vyombo vya habari, wabunifu, washirika wanaounga mkono kazi za ubunifu na Serikali.
Kujisajili fuata kiunganishii=> http://www.timetickets.co.tz/innovationweek2019/session/media-for-innovation-growth
Kampuni ya Nukta Africa imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo kuhakikisha sekta ya teknolojia nchini inakua kwa kiwango kizuri ambapo kupitia tovuti yao ya habari ya www.nukta.co.tz wamekuwa wakiripoti kazi zinazofanywa na wabunifu zikiwemo kampuni zinazochipukia (Startups) ambazo zimejikita kutumia teknolojia kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii.
Latest