CAG: Taasisi zenye kasoro ya manunuzi zaongezeka, zaigharimu Serikali Kuu Sh5.35 bilioni
Bila kuwapo kwa thamani ya fedha kwenye manunuzi yaliyofanyika ni sawa na fedha kutumika bila kuwa na manufaa kwa umma au kama vile zimepotea. Picha!Mtandao.
- Idadi ya taasisi za Serikali Kuu zilizokuwa na kasoro kwenye manunuzi zimeongezeka toka taasisi nane hadi 13 kwa mwaka 2017/2018 ikiwa ni ongezeko la asilimia 62.5 ukilinganisha na mwaka 2016/2017.
- Hali hiyo imesababisha malipo ya Sh5.35 kufanyika bila bidhaa, kazi na huduma kutolewa.
- CAG azitaka taasisi za Serikali Kuu kuzingatia sheria na kanunuzi za manunuzi.
Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Professa Mussa Juma Assad amesema idadi ya taasisi za Serikali Kuu zilizokuwa na kasoro kwenye manunuzi zimeongezeka toka taasisi nane hadi 13 kwa mwaka 2017/2018, jambo lililosababisha malipo ya Sh5.35 kufanyika bila bidhaa, kazi na huduma kutolewa.
Ongezeko hilo ni sawa asilimia 62.5 ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2016/2017.
Katika ripoti ya ukaguzi wa hesabu za Serikali Kuu ya mwaka wa fedha wa 2017/18 iliyotolewa Aprili 10, 2019 inaeleza kuwa kutokana na manunuzi kulipiwa bila bidhaa na huduma kupokelewa au kazi kutokufanyika, thamani ya fedha na tija havikuweza kupatikana kwa manunuzi hayo.
CAG anabainisha kuwa bila kuwapo kwa thamani ya fedha kwenye manunuzi yaliyofanyika ni sawa na fedha kutumika bila kuwa na manufaa kwa umma au kama vile zimepotea.
“Katika ukaguzi wangu nilibaini kuwa taasisi za serikali kuu kumi na tatu (13) zimelipia bidhaa, huduma na kazi mbalimbali; zenye thamani ya Sh 5,356,549,884.76 ambazo bidhaa hazijapokelewa, wala huduma haijatolewa na kazi hazijafanyika,”
“Ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2016/17, idadi ya taasisi za Serikali Kuu zilizokuwa na kasoro kwenye manunuzi zimeongezeka toka taasisi nane (8) hadi kumi na tatu (13) kwa mwaka huu wa fedha; hilo ni ongezeko la asilimia 62.5,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Anabainisha kuwa manunuzi ya jinsi hiyo ni kinyume na makubaliano yaliyofanyika kati ya wazabuni/wakandarasi na taasisi za Serikali Kuu ambayo imeweka bayana kwamba malipo yasifanyike kabla ya kazi kufanyika, bidhaa kuletwa na huduma kutolewa.
Soma zaidi:
- CAG: HESLB imeshindwa kuwapata wadaiwa wa Sh1.46 trilioni
- Bunge lamtenga rasmi CAG Assad
- CAG hajaiacha salama sekta ya utalii, aibua utofauti wa takwimu za watalii
Sheria ya Manunuzi ya Umma namba 7 ya Mwaka 2011 iliyorekebishwa mwaka 2016 pamoja na kanuni zake za mwaka 2013 hutoa mfumo wa kisheria unaosimamia taasisi na mchakato wa manunuzi katika sekta ya umma ili kuhakikisha uwazi na uwajibikaji unakuwepo.
“Hii ni hatari katika kufanya manunuzi ya umma kwa kuwa bidhaa yawezekana zisipokelewe kabisa au kazi na huduma kutofanyika au vikafanyika kwa muda usiokuwa muafaka,” inaeleza ripoti hiyo.
CAG amezishauri menejimenti za taasisi za Serikali Kuu kufanya jitihada za kufuatilia bidhaa ambazo hazijapokelewa ili kuokoa fedha za umma, pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria wazabuni na wakandarasi ambao watashindwa kufanya kazi au kutoa huduma kwa wakati.
Latest