Wabuni jukwaa la mtandaoni linalotatua changamoto za kilimo kwa SMS
- Linawawezesha wakulima kuwasiliana na kusaidiana kutatua changamoto za kilimo kwa kutumia ujumbe mfupi wa maneno.
- Mkulima haihitaji kwa wa ofisa ugani lakini anapata suluhisho kwenye simu yake.
Dar es Salaam. Wakulima wa Tanzania wasio na fursa ya kukutana na maofisa ugani mara kwa mara huenda wakanufaika na teknolojia ya simu za mkononi, baada wabunifu kubuni jukwaa la kuwaunganisha kutatua changamoto za kilimo ili kuongeza uzalishaji na kutanua wigo wa masoko ya mazao yao.
Jukwaa hilo la mtandaoni, linalojulikana kama Wefarm, linawawezesha wakulima kuwasiliana kwa kutumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS) ili kusaidiana kutatua changamoto za kilimo ikiwemo magonjwa ya mimea na mifugo kulingana na uzoefu walionao katika sekta hiyo.
Pia linatoa fursa ya kuwakutanisha na wataalam wa kilimo kwa kutumia SMS ili kupata ushauri wa njia bora za uzalishaji na kuongeza tija katika maeneo yao.
Mkuu wa Uendeshaji kutoka kampuni ya Wefarmtz Limited inayosimamia jukwaa hilo, Cyrila Anton ameiambia www.nukta.co.tz kuwa jukwaa hilo lilianza kutumika kwa majaribio tangu mwanzoni mwa mwaka huu katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini hasa Mbeya, Iringa na Njombe.
Amesema mpaka sasa limewafikia wakulima 50,000 na litazinduliwa rasmi hivi karibu ikiwa ni hatua ya kuwafikia wakulima wengi wa Tanzania baada ya kuonyesha mafanikio katika nchi za Uganda na Kenya.
Ili kuhakikisha jukwaa hilo linakuwa na ufanisi, wanafanya kazi na vijana wanaojitolea kuwawezesha wakulima kutumia mfumo huo wa SMS kuwasiliana kwa urahisi na kubadilishana uzoefu na mawazo katika shughuli zao za kila siku.
“Wakulima hatozwi gharama zozote wakati wakituma ujumbe wa maneno kwa sababu tunasimamia sisi, wanawasiliana wao kwa wao na watalaam wa kilimo ili kupata ushauri,” amesema Anton.
Zinazohusiana:
- Tanzania ni miongoni mwa nchi 11 zinazowekeza kwenye utafiti wa GMO Afrika
- Wakulima washauriwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kilimo cha umwagiliaji
- Apps za kilimo zinazoweza kuwanufaisha wakulima Tanzania
Mfumo huo pia umekuwa ukitoa fursa kwa Wefarm kufahamu kwa kina changamoto kuu zinawazowakabili wakulima na kuzipa kipaumbele wakati wa kuzitafutia suluhisho la kudumu.
Katika kipindi kifupi tangu jukwaa hilo lianze kufanya kazi, Anton amesema changamoto inayowakumba zaidi wakulima ni magonjwa ya mimea na mifugo, upatikanaji wa pembejeo za kilimo ikiwemo mbegu bora na masoko ya uhakika ya bidhaa.
Mfumo huo wa SMS unawawezesha wakulima kuwasiliana wakiwa shambani na kutatua changamoto zao bila kuhitaji mtu wa tatu. Picha|Wefarm.
Wakati jukwaa la Wefarm linalokusudia kuwafikia wakulima takriban 400,000 mwishoni mwa mwaka huu, litakuwa na kibarua kigumu cha kuwawezesha wakulima kutumia kwa ufanisi teknolojia hiyo ambayo inasaidia kuondoa changamoto ya upatikanaji kwa wakati kwa maofisa ugani.
Mbali na changamoto hiyo, litatakiwa kukabiliana na tabu za kuwafikia wakulima wengi kwa wakati mmoja hasa katika maeneo ya vijijini yanayokabiliwa na changamoto za ubovu wa miundombinu na mabadiliko ya hali ya hewa.
Ubunifu wa teknolojia katika sekta ya kilimo umekuwa ukihamasishwa zaidi ulimwenguni kwa sasa ili kuhakikisha wakulima wanaongeza ufanisi katika uzalishaji wao.