Kijana aliyeahirisha masomo elimu ya juu kuwafungulia fursa wanafunzi wa sekondari Tanzania

August 13, 2019 11:58 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Anaendesha programu ya mafunzo shuleni ya kuwaunganisha wanafunzi na watu waliofanikiwa kitaaluma.
  • Wanafunzi hao wanapata wasimamizi wanaowasaidia kutimiza ndoto zao za kielimu.
  • Programu hiyo inapunguza pengo la wazazi kutokua karibu na watoto wao.

Dar es Salaam. Kutokana na mabadiliko ya kiuchumi, wazazi wengi kwa sasa hawapati muda wa kukaa na watoto wao ili kujua maendeleo ya kiafya, kiakili na wawapo shuleni. 

Hali hiyo imesababisha baadhi ya wanafunzi kukosa muongozo na hata motisha ya kusoma kwa juhudi kwani hakuna mtu anayewaulizia maendeleo yao darasani, jambo linalowaweka katika sintofahamu ya kuwa na mstakabali mzuri wa maisha yao. 

Siyo tu wanakosa ukaribu wa wazazi na walezi kuwaongoza katika njia nzuri ya maisha bali wanakosa fursa muhimu ya kujifunza ujuzi na kupata stadi za maisha ambazo hazipatikani darasani. 

Lakini wabunifu wakati wote wanaona changamoto kama fursa ya kuboresha maisha ya watu na jamii inayowazunguka. 

Joseph Sosoma (21) ambaye ni muhitimu wa kidato cha sita mwaka 2018 ameamua kuanzisha programu maalum ya kuwaunganisha wanafunzi wa shule za sekondari Tanzania na wataalam waliopo katika sekta mbalimbali nchini, ikiwa ni hatua kuwasaidia kufahamu kile wanachokipenda katika taaluma zao. 

Kupitia taasisi yake ya “Walk of Life” anayoiongoza wanatoa mafunzo mbalimbali ya ujuzi kwa wanafunzi yanayowasaidia kuwaanda kufikia ndoto za kielimu na kuhakikisha wanapata wasimamizi sahihi ambao wanawashauri katika masuala mbalimbali ya maisha. 

“Ni rahisi kwa mwalimu kumwambia mwanafunzi asome awe daktari lakini ni rahisi zaidi kwa daktari kumwambia uzuri wa kuwa daktari ni upi akiambatanisha na shuhuda na hata changamoto,” amesema Sosoma ambaye aliahirisha masomo ya elimu ya juu kwa mwaka mmoja ili kuimarisha taasisi yake.


Zinazohusiana


Mpaka sasa wameweza kuzifikia shule mbili za Sekondari za Gerezani na Jamhuri za jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kuwajengea uwezo baadhi ya wanafunzi wa shule hizo ikiwemo kuwakutanisha na watu waliofanikiwa katika maisha. 

Mathalani, taasisi hiyo ya “Walk of Life” kuwaunganisha wanafunzi wa kike Halima Mabrouck kutoka shule ya Gerezani na Msimamizi Mkuu wa biashara kutoka kampuni ya gesi ya Zil, Mary Sonda iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam.

Sosoma ameaiambia wwww.nukta.co.tz kuwa ni vyema elimu itolewe shuleni juu ya umuhimu wa programu za kuwaandaa wanafunzi kitaaluma zaidi na kupata watu wanaoweza kuwashauri njia sahihi kuelekea mafanikio yao.  

Sonda anasema kumsimamia Halima imekua rahisi kwani ana ndoto ya kufanya kazi ambazo anazifanya sasa za usimamizi wa biashara na  zaidi kwake ni jambo muhimu kwani anamsaidia msichana anayetazamia kuleta mabadiliko kwenye jamii kwa kutumia ubunifu wa mavazi. 

Safari bado ndefu

Licha ya hatua ambazo “Walk of Life” imepiga, bado itakuwa na kibarua kigumu cha kuongeza elimu hiyo mashuleni, kwa sababu bado walimu na wanafunzi hawajawa na muamko mkubwa wa kuipokea kutokana na changamoto ukosefu wa vifaa vya mawasiliano kwa wanafunzi.

Ili kuongeza ufanisi italazimika kutumia mifumo na majukwaa ya mtandaoni ili kuongeza wigo wa kuwafikia wanafunzi wengi kwa wakati mmoja ili kuhakikisha malengo yake yanatimia kwa wakati na wanafunzi wengi wananufaika. 

Mary Sonda (kulia) akiwa na Halima Mabrouk baada ya semina iliyofanyika Shule ya Sekondari Gerezani | Picha na Walk of life.

Wadau wa maendeleo ya elimu wanena

Frank Mbaga ambaye ni mhitimu wa kozi ya Ualimu kutoka Chuo kikuu cha Tumaini kampasi ya Dar es Salaam (TURDACO) amesema mawazo ya Sosoma yana umuhimu mkubwa kwa wanafunzi wa Tanzania lakini bado anahitaji kupambana na vikwazo vilivyopo mbele yake ikiwemo umri alionao.  

“Siku hizi hizi program zimekua nyingi sana. Watu wanaenda mashuleni kupeleka maono yao lakini wanashindwa kuyatekeleza hiyo inapelekea hata wale wenye malengo ya dhati kushindwa kupewa hiyo nafasi,” amesema Mbaga.

Programu hizo za kuwasaidia wanafunzi kutanua wigo wa mstakabli wa maisha yao, zinahitaji kuwa na moyo wa kujitolea ili kuwasaidia wanafunzi wenye kiu ya kutimiza ndoto zao. 

Mtaalamu wa Programu za kompyuta kutoka kampuni ya Code for Africa, Khadija Mahanga anasema japo ni kazi ya kujitolea, kazi hiyo ina manufaa makubwa  kwa wanafunzi kwani imawapatia rafiki wa kuzungumza naye kadiri wanavyopiga hatua katika maisha. 

Mahanga ambaye mpaka sasa ameshiriki programu nne za kuwasimamia wanafunzi ikiwemo ya “Fanaka” na “Code Lady” ameiambia www.nukta.co.tz kuwa msimamizi ni rafiki wa mwanafunzi hasa pale mwanafunzi anapokua hana mahusiano ya karibu baina yake na mzazi na hata mwalimu.

“Kuna vitu mwanafunzi anashinda kuongea na mzazi wala mwalimu anakuambia msimamizi wake. Msimamizi kwa mwanafunzi ni kama rafiki mkubwa,” anasema Mahanga na kuongeza kuwa, 

Sosoma na timu yake wanakusudia kujitanua zaidi na kuwafikia wanafunzi wa vyuo vikuu kuanzia mwaka wa masomo wa 2019/2020 ambazo watakuwa wanachangia kiasi kidogo cha pesa ambacho kitakuwa kinatumika kuendesha semina na mikutano mbalimbali mashuleni.

Enable Notifications OK No thanks