Kutana na mwanadada anayejisomesha elimu ya juu kwa kuuza pipi
- Alianza kuuza pipi akiwa shule ya Sekondari Debrabant iliyopo wilaya ya Temeke kwa mtaji wa Sh2,000.
- Hana wazazi wote wawili wala ndugu anaowategemea kumsomesha.
- Kipato anachokipata anatumia kulipia ada chuoni na kujihudumia.
Dar es Salaam. Anthonita ni mwanafunzi wa mwaka wa pili ngazi ya diploma katika Chuo Cha Usimamizi wa Fedha (IFM) jijini Dar es Salaam. Ni miongoni mwa watoto wa kike unaoweza kuwaita mashujaa wa kuruka vikwazo vya maisha ili kutimiza ndoto zao.
Akiwa ni mtoto wa mwisho kati ya watoto wawili katika familia ya marehemu Mzee Joseph Chaba ya Jijini Dar es Salaam, ameweza kufika elimu ya juu kwa biashara ya kuuza pipi tangu akiwa sekondari.
Alianza kuuza pipi kwa mtaji wa Sh2,000 wakati anasoma shule ya Sekondari ya Debrabant iliyopo wilaya ya Temeke ambapo wateja wake walikuwa wanafunzi wenzake.
Alifikiria kuanza biashara ya kuuza pipi baada ya kuona wanafunzi wenzake wakipendelea kwenda nje ya mazingira ya shule kununua vitu vitamu kama pipi na biskuti.
Hivyo alitumia nafasi hiyo, kupeleka kile kinachopendwa zaidi na wanafunzi ili kupata mkate wake wa kila siku.
“Safari yangu haikua rahisi kama inavyoweza kufikirika ila niliweka aibu nyuma na kuzingatia kile ninachokitafuta kama mtu nisiye na mahali pa kutegemea,” anasema mwanadada huyo.
Zinazohusiana:
- Hawa ndiyo wanamuziki wa kike wanaotikisa dunia kwa wafuasi wengi Youtube.
- Jessica Mshama: Mwanamuziki, Mjasiriamali anayebadilisha maisha ya Watanzania kwa biashara
- Wanapokwama wanamuziki wa kike Tanzania kutamba kimataifa.
Hata alipompoteza mama yake pamoja na kaka yake ndani ya miezi miwili mfululizo, jambo lililomletea huzuni kubwa katika maisha yake, hakukata tamaa aliinuka tena na kuendelea kuisaka ndoto ya kufika chuo kikuu na kusomea kile anachokipenda.
Anthonita mwenye umri wa miaka 26 hakuwa na msaada wowote toka kwa ndugu baada ya kupoteza watu aliokua akiwategemea katika kuishi kwake, ila kwa mtaji wa Sh2,000 dada huyu aliweza kubadilisha historia ya maisha yake.
“Sikukata tamaa kwa namna yoyote baada ya kupata pigo lile, ila lilinipa kujisimamia kwani nilijiuliza nisiposimama nani atanisimamia?”, anahoji Anthonita.
Kiasi cha pesa alichokua anakipata kwenye biashara yake ya pipi alikuwa anatumia kulipa ada na kukidhi mahitaji ya shule.
Ili kuendelea na kufanikiwa uthubutu na nia ni kila kitu. Picha| Anthonita.
Hata wale walionekana kuwa marafiki wa karibu na Anthonita walikuwa wakimcheka na kumkatisha tamaa katika biashara yake huku wakimwambia ni biashara ya aibu na ya kumpotezea muda.
Kutokana na kuipenda biashara yake hakukuta tamaa, imeendelea kukua siku hadi siku na kufikia hatua ya kuwa msambazaji wa pipi za jumla katika maduka mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Ili kuhakikisha biashara na masono yanaenda vizuri, Anthonita anatumia muda wake ambao hana vipindi darasani kuwasambazia wateja wake pipi.
Mwanadada huyo ana kila sababu ya kujivunia, mapambano kwa sababu biashara yake ina manufaa kwake ikiwemo kumuingizia kipato kinachomuwezesha kuendelea na masomo ya chuo.
Anaamini kwa biashara hiyo atakamilisha masomo yake ya diploma na kisha shahada ya kwanza ili elimu atakayoipata aitumie kuboresha biashara yake na kuajili watu wengi zaidi.
Katika kusaidia jamii, anatumia siku yake ya kuzaliwa kila mwaka kusheherekea na watoto yatima katika vituo mbalimbali vyenye uhitaji.
Moyo wa kutokata tamaa alionao Anthonita ni funzo tosha kwa wasichana na wanawake wengine wanaopigania ndoto zao.