Hawa ndiyo wanamuziki wa kike wanaotikisa dunia kwa wafuasi wengi Youtube

Rodgers George 0002Hrs   Agosti 21, 2019 Maoni & Uchambuzi
  • Yupo Ariana Grande, Taylor Swift na Rihanna ambao wote wanatoka Marekani. 
  • Wasanii wa kike Bongo wafyata mkia baada ya wakwanza kuwa na wafuasi 275,567.
  • Kundi la wasanii wa kike la Blackpink la nchini Korea Kusini nalo limefanikiwa kupenya kwenye orodha hiyo. 

Dar es Salaam. Katika ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia, mambo mengi yanafanyika kidijitali. Hata sekta ya muziki, sanaa na burudani nayo imepiga hatua kubwa katika kutumia teknolojia kuwainua na kuwaingizia kipato wasanii.

Mtandao wa Youtube umekuwa ukitumiwa zaidi na wasanii kuonyesha na kuuza kazi ikizingatiwa kuwa unaweza kuwafikia watu wengi kwa urahisi na kwa haraka. 

Wasanii wa kike wa Tanzania nao hawajabaki nyuma kuchangamkia fursa ya kufaidika na uwepo wa Youtube wakati wakitumia majukwaa mengine ya muziki ili kufikisha ujumbe kwenye jamii. 

Uchunguzi mdogo uliofanywa na timu ya www.nukta.co.tz katika mtandao huo ukihusisha wasanii wa kike wa Tanzania wenye wafuasi wengi (subscribers) umebaini kuwa Faustina Mfinaga maarufu kama Nandy ndiye anayeongoza kuwa na wafuasi wengi. 

Takwimu za Youtube za hadi Agosti 20, 2019, zinaonyesha kuwa Nandy alikuwa na wafuasi 275,567 akifuatiwa na Vanessa Mdee (165,131). 

Wengine wenye wafuasi wengi ni pamoja na Maua Sama (149,480), Ruby (69, 078) na Rosa Ree (55,351).


Zinazohusiana:


Wakati wasanii wa kike wa Tanzania wakijikongoja kupata wafuasi Youtube, wenzao wa nchi zingine hasa zile zilizoendelea kama Marekani na Uingereza wamepiga hatua kubwa, jambo linalotoa changamoto kwa wasanii wa Tanzania kuongeza juhudi ya kujitanua kimataifa. 

Nukta kwa yanayokuhusu (www.nukta.co.tz) inakuletea orodha wasanii wa muziki watano wenye wafuasi wengi Youtube ambao wamefanikiwa kutokana na shughuli wanazofanya katika sekta ya muziki duniani.

1. Ariana Grande

Ariana mwenye umri wa miaka 26 alianza sanaa kama muigizaji kupitia filamu ya muendelezo (TV series) ya Victorious iliyoonyeshwa kupitia chaneli ya Nickelodeon mwaka 2010 hadi 2013. Mwaka 2013, Grande alitoa albamu yake ya kwanza iliyoitwa “Yours Trully”. 

Mpaka jana, Agosti 20, akaunti yake ya Youtube ilikuwa na wafuasi zaidi ya milioni 37.5 ambao ni mara kumi zaidi ya wafuasi alionao Nandy.

Kupitia albamu hiyo, Grande aliwika na ngoma kama The Way aliyomshirikisha marehemu Mac Miller. The Way iliingia kwenye 10 bora ya chati ya nyimbo 100 bora za Marekani ya Billboard Hot 100 Machi 25, 2013. 

Amepata tuzo za muziki zaidi ya 81 ambapo kwa sasa anatamba ngoma yake ya  Side to side aliyoshirikiana na msanii Nicki Minaj yenye watazamaji takriban 1.6 hadi kufikia jana Agosti 20. 

Pia Grande anatikisa spika mbalimbali duniani na kibao chake kipya alichokiita Boyfriend  aliyoiachia Agosti 2 ambayo hadi mchana wa leo ilikuwa imetazamwa na watu zaidi ya milioni 55.9 katika mtandao wa Youtube.


Amepata tuzo za muziki zaidi ya 81 ambapo kwa sasa anatamba ngoma yake ya  Side to side aliyoshirikiana na msanii Nicki Minaj yenye watazamaji takriban 1.6 hadi kufikia jana Agosti 20. Picha|Mtandao. 


2. Taylor Swift 

Swift (29) ambaye ni mzaliwa wa Marekani anafahamika zaidi kwa vibao vyake vya Shake it off, Blank space na Bad blood ambavyo vyote vinatikisa Youtube kwa kuangaliwa na watu wengi wanaozidi bilioni moja. 

Hadi majira ya 2:30 mchana wa leo alikuwa na wafuasi takribani milioni 35.3 huku akiwa ameshinda tuzo 446 na kutajwa kwenye tuzo zipatazo  700 duniani.

Baada ya kuanza safari yake ya mziki mwaka 2004 na safari hiyo kushika kasi mwaka 2008, Swift amebaki akifahamika kama msanii mwenye nyimbo za masimulizi huku nyingi zikigusia maisha yake binafsi. 


Msanii wa muziki, Taylor Swift ni kati ya wasanii wenye idadi kubwa ya mashabiki mtandaoni. Picha|Taylor Swift.

3. Katty Perry

Roar, Dark horse, firework na Last friday night ni baadhi ya nyimbo za mwanadada huyo ambazo mpaka sasa kila nyimbo ina watazamaji zaidi ya bilioni 1 Youtube.

Licha ya kuanza muziki kama mwimbaji wa nyimbo za injili, Perry ambaye hadi mchana wa leo alikuwa na wafuasi 34.7 ni kati ya wasanii waliodumu kwenye muziki tangu mwaka 2002 bila kupoteza uhalisia wa muziki wake. 

Perry mwenye umri wa miaka 34 ana tuzo 91 huku akiwa ametajwa kushindana kwenye tuzo takribani 300 tangu kuanza kwa muziki wake. Pamoja na muziki, Perry ni jaji kwenye mashindano ya “American Idol” na muigizaji wa filamu.

Hadi sasa, Perry ameuza albamu milioni 18 na “single” milioni 125 huku albamu ya “Prism” ikiwa ni kati ya albamu zake zilizofanya vizuri kwenye chati mbalimbali duniani.Katty Perry alianza kama mwanamuziki wa  nyimbo za injili lakini sasa anatikisa dunia kwa nyimbo kali. Picha|Katty Perry.


4. Rihanna 

Akiwa na wafuasi 32.6 kwenye chaneli yake ya YouTube, Rihanna ni kati ya wasanii wa muda mrefu walioweza kukaa kwenye chati ya muziki kwa muda mrefu.

Kama mwanadada aliyeweza kuchuana na msanii mkongwe Beyonce, Rihanna kwa sasa anatamba ngoma Diamonds ambayo mpaka mchana wa leo imetazamwa na watu zaidi ya bilioni 1.3.

Rihanna (31) ambaye pia ni muigizaji, amefanikiwa kupata tuzo 214 zikiwemo Grammy (9) na Billboard (12) huku akiwa ametajwa kushindania za takriban 584.

Rihanna (31) ambaye pia ni muigizaji, amefanikiwa kupata tuzo 214 zikiwemo Grammy (9) na Billboard (12) huku akiwa ametajwa kushindania za takriban 584. Picha|Rihanna.

5. Blackpink 

Hili ndilo kundi pekee nje ya Marekani ambalo limefanikiwa kuingia kwenye chati hii. Kutoka Korea Kusini, akaunti ya kundi hili la wasichana wanne (Jisoo, Jennie, Rosé na Lisa) ina wafuasi milioni 29.4 hadi kufikia Agosti 20, 2019.

Licha ya kuanzishwa mwaka 2016, kundi hili limefanikiwa kuingiza nyimbo kwenye chati ya Billboard. Nyimbo hiyo inafahamika kama Boombayah huku Ddu-Du Ddu-Du ikitajwa kuwa nyimbo iliyovunja rekodi kwa kutizamwa na watu wengi zaidi ndani ya saa 24 nchini korea.

Hadi sasa, kundi hilo linashikilia tuzo takribani 25 huku likiwa limetajwa kushindania tuzo mara 108. BlackPink ni kati ya makundi ambayo Wakorea wanajuvunia lililofanikiwa kutoboa anga za kimataifa kwa kasi ndani ya muda mfupi. 


Kundi la BlackPink ni kundi pekee la wanamuziki  wa kike nje ya Marekani lililotikisa kwa wafuasi wengi Youtube. Picha|BlackPink.

Related Post