Wanasayansi waeleza madereva wa kiume wanavyokengeuka kirahisi barabarani

October 17, 2019 8:10 am · Zahara
Share
Tweet
Copy Link
  • Wanaeleza kuwa madereva wa kiume ndiyo vinara wa kukengeuka na husababisha ajali za barabarani zaidi kuliko wanawake.
  • Ukengeukaji ni pamoja na matumizi ya simu ya mkononi, kuangalia luninga na kusikiliza redio na kukosa umakini wakati wa kuendesha chombo cha moto.
  • Serikali na wadau waendelea kutoa elimu ili kupunguza ajali za barabarani.

Madai kwamba madereva wa jinsia ya kike ni wazembe sasa yanaweza kuwa yamefutwa na utafiti wa hivi karibuni uliogundua kuwa madereva wa kiume ndiyo wanaongoza kwa kukengeuka wanapoendesha vyombo vya moto barabarani.

Utafiti huo uliofanyika nchini Norway na kuoongozwa na mtafiti Ole Johansson na ulichapishwa na jarida la mtandaoni la MailOnline toleo  la Novemba 17, 2017 umegundua kuwa ukengeukaji  wa madereva barabarani unachangia  asilimia 12 ya ajali za barabarani katika nchini mbalimbali duniani katika mazingira tofauti. 

Hata hivyo, ripoti ya utafiti huo inaeleza kuwa madereva wa kiume ndiyo vinara wa kukengeuka na husababisha ajali za barabarani zaidi kuliko wanawake.  

Dereva mkengeukaji ni yule anayedhihirisha tabia yoyote ile ambayo  itamlazimisha ahamishe mikono na fahamu za akili yake toka kwenye usukani na mazingira ya usalama barabarani. 

Tabia hizo ni pamoja na matumizi ya simu ya mkononi, kuangalia luninga na kusikiliza redio na kukosa umakini wakati wa kuendesha chombo cha moto.

Tabia hii inachangiwa na kasi ya ukuaji wa teknologia iliyorahisisha shughuli za mawasiliano katika maeneo mbalimbali duniani.

Utafiti huo uliopewa jina la uchunguzi wa usumbufu wa madereva (An Examination of Drivers’ Distractions, Causes, and Potential Interventions) ulihusisha uchunguzi wa  tabia na hisia za madereva, umri na jinsia zao  ili kugundua ni kundi gani linaongoza kwa tabia ya kukengeuka na kusababisha mazingira hatarishi kwa ajali za barabarani kutokea.

Kwa mujibu wa utafiti huo, madereva wa jinsia ya kike  huonyesha unyenyekevu na uangalifu wakiwa wanaendesha vyombo vya moto katika  mazingira hatarishi  barabarani ikiwemo kuzingatia taa za kuongozea magari au alama za vivukio vya waenda kwa miguu.

Madereva wazee wa kike wametajwa kuwa makini wakati wanaendesha magari, jambo linalowaweka salama zaidi wakiwa barabarani.

Udereva kengeushi ni moja ya vyanzo vikubwa vya watu kupoteza maisha vinavyotokana na ajali za barabarani katika maeneo mbalimbali duniani. Picha|Mtandao.

Lakini vijana madereva wa jinsia ya kiume wasio makini (extroverted) na wale wenye ulemavu ‘vuguvugu’ wa akili (neurotic) na madereva wenye uzoefu wa miaka mingi, huonyesha zaidi tabi kengeushi kuliko makundi mengine.

Vile vile, utafiti huo uligundua kuwa tabia ya udereva kengeushi iliyokithiri ni matumizi ya redio na hasa tabia ya madereva kupendelea kubadilisha vituo vya redio wanapoendesha magari.

Utafiti huo ulihusisha sampuli ya watu 1,514 na kueleza kuwa “japo kumekuwepo na kampeni nyingi sana zikilenga kuboresha usalama barabarani, utafiti kuhusu athari za udereva kengeushi ulikuwa bado haujafanyika”.   

Tabia kengeushi zinavyochangia ajali barabarani 

Udereva kengeushi ni moja ya vyanzo vikubwa vya watu kupoteza maisha vinavyotokana na ajali za barabarani katika maeneo mbalimbali duniani.

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2018 juu ya hali ya usalama barabarani (Global status report on road safety (2018) inabainisha kuwa udereva kengeushi unazidi kuchangia viwango vya ajali za barabarani na kwamba  vijana kati ya umri wa miaka 15 hadi 29 wanaongoza kwa kupata ajali na kupoteza maisha.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa watu milioni 1.25 hufariki kwa ajali kila mwaka ambapo watu milioni 20 hadi milioni 50 hubaki na majeraha na ulemavu wa aina mbalimbali.


Zinazohusiana:


Nini kifanyike kupunguza ajali?

Mapendekezo ya utafiti wa WHO ni mamlaka, taasisi na hata makampuni binafsi kubuni hatua za kuchukua ikiwemo kutoa miongozo na ikibidi sera mahsusi za kudhibiti udereva kengeushi ili kupunguza ajali zinazosababisha vifo na majeruhi duniani.

Umoja wa Mataifa (UN) limeonyesha mfano wa kuigwa ambapo tangu mwaka 2016, ulitoa mwongozo kwa wafanyakazi wake wote waliodhaminiwa magari kutojihusisha na udereva kengeushi kwa sababu yoyote ile.

Nchini Tanzania, Serikali, wadau mbalimbali wanaendelea na juhudi za kutoa elimu kwa madereva na watumiaji wa barabara kuhakikisha wanaendesha bila kukengeuka wakiwa barabarani ili kuokoa uhai wao.

Mwenyekiti wa shirika la Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA), John Seka amesema kuwa asasi yake  inajitahidi kwa kiasi kikubwa kutoa elimu juu ya athari za matumizi ya vihatarishi vya ajali ikiwemo ukengeukaji.

“Tunafanya kampeni ya “Abiria Paza Sauti” kuwahamasisha  madereva kuheshimu sheria za barabarani na kuacha matumizi ya simu wakiwa wanaendesha,” amesema Seka.

Pia wanawajengea uwezo wananchi kuwa na ujasiri wa kukemea  pale wanapoona dereva wa basi au daladala anakiuka miongozo ya kutokutumia simu wakati anaendesha gari.


Kutokana na juhudi za kutoa elimu ya usalama barabarani kutoka wadau mbalimbali, idadi ya ajali za barabarani inapungua kila mwaka, lakini juhudi zaidi zinahitajika kutokomeza ajali zote.

Ripoti ya takwimu muhimu ya ‘Tanzania in Figures 2018’ iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha kuwa ajali kubwa zinapungua kila mwaka.

Mathalani, mwaka 2016 ajali kubwa zilikuwa 10,297 na zikapungua hadi 6, 022 mwaka uliofuata kabla hazijapungua zaidi hadi kufikia 3,988 mwaka jana. 

Hata hivyo, nguvu ya pamoja inahitajika kwani ajali ndogo ndogo bado zinaongezeka, kwa mujibu wa ripoti hiyo ajali hizo zimeongezeka kutoka milioni 2.5 mwaka 2017 hadi milioni 2.7 mwaka jana.

Naye Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda ya Dar es Salaam, Marison Mwakyoma amesema wanaendelea kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari na kampeni maalum juu ya umuhimu wa kuzingatia sheria za usalama barabarani kwa madereva na watembea kwa miguu.

“Tunatoa elimu ya usalama barabarani radioni na hata kwenye TV (televisheni), vilevile huwa tunatoa elimu kipindi cha wiki ya nenda kwa usalama, na kushirikiana na wadau wengine katika kutoa elimu,” anasema.

Enable Notifications OK No thanks