Wachambuzi watabiri neema soko la Hisa Dar, thamani ya mauzo ikipaa
- Imeongezeka hadi Sh337.7 milioni kutoka Sh156.4 milioni iliyorekodiwa juma lililopita.
- Mauzo hayo yamechangiwa zaidi na benki ya CRDB baada ya kurekodi asilimia 79.33 ya thamani ya mauzo yote ikifuatiwa kwa mbali na kampuni ya Twiga yenye asilimia 14.55.
- Wachambuzi wamebainisha kuwa kunaweza kutokea mwenendo mzuri siku zijazo.
Dar es Salaam. Thamani ya mauzo ya wiki nzima katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) imeongezeka hadi Sh337.7 milioni kutoka Sh156.4 milioni iliyorekodiwa juma lililopita huku wachambuzi wakibainisha kuwa kunaweza kutokea mwenendo mzuri siku zijazo.
Uchambuzi wa soko kwa wiki iliyoanzia Oktoba 11 hadi Oktoba 18 uliofanywa na kampuni ya udalali ya masoko ya mitaji na dhamana, Zan Securities, unaeleza kuwa thamani ya mauzo katika soko hilo iliongezeka kwa asilimia115.9 kutoka yale ya wiki iliyopita.
Wiki za DSE hujumuisha siku za kazi pekee yaani Jumatatu hadi Ijumaa.
Mtendaji Mkuu wa Zan Securities, Raphael Masumbuko, ameeleza kuwa mauzo hayo yamechangiwa zaidi na benki ya CRDB baada ya kurekodi asilimia 79.33 ya thamani ya mauzo yote ikifuatiwa kwa mbali na kampuni ya Twiga yenye asilimia 14.55.
“Mauzo ya soko yameonyesha matumaini kiasi wiki hii. Tunafikiri mwenendo huu utaendelea wiki zijazo,” amesema Masumbuko katika taarifa yake iliyotolewa jana (Oktaba 18,2019).
Zinazohusiana:
- M-pesa, intaneti vyachangia Vodacom Tanzania kupata faida ya Sh90 bilioni
- Wawekezaji wa Acacia soko la hisa Dar tabasamu tupu
- Maumivu kwa wawekezaji wa kampuni ya bia soko la hisa Dar
Mauzo ya soko la hisa yamekuwa na mwenendo wa kupanda na kushuka ambapo wiki iliyoishia Septemba 30 thamani ya mauzo ilikuwa Sh357.43 milioni na ikapanda zaidi ya mara tatu hadi Sh1.17 bilioni wiki iliyoishia Oktoba 4.
Lakini wiki iliyofuata ya Oktoba 11 ikaporomoka kwa kasi hadi kufikia Sh156.4 milioni kabla ya kupanda hadi Sh337.7 milioni.
Latest