Vifaa vya kielektroniki vinavyosaidia kutibu maumivu ya shingo

November 8, 2019 11:53 am · TULINAGWE ALSON
Share
Tweet
Copy Link
  • Wabunifu wametengeneza kifaa maalum kinachosaidia utendaji mzuri misuli ya shingo na kukuepusha na maumivu yote. 
  • Kinasaidia mishipa na misuli ya shingo kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
  • Wataalam wa afya washauri watu kufanya mazoezi kabla ya kutumia vifaa hivyo. 

Dar es Salaam. Wakati wote teknolojia inayovumbuliwa duniani huwa na lengo la kutatua changamoto fulani kwenye jamii ili kuboresha maisha ya watu. 

Baadhi ya watu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya maumivu ya shingo katika mazingira tofauti ikiwemo wakati wa kulala, safari na hata ofisini. 

Daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba katika Chuo cha Tiba na Sayansi Shirikishi Moshi (KCMC), Joshua Sultan anasema zipo sababu mbalimbali zinazosababisha maumivu ya shingo ikiwemo kukaa sehemu moja  kwa muda mrefu na kukaa katika mikao isiyoendana na mwili, jambo linalosababisha mishipa na misuli ya shingo kuchoka na kushindwa kufanya kazi ipasavyo. 

“Sababu zinazopelekea maumivu ya shingo ni nyingi, lakini kwa kawaida binadamu kukaa sehemu moja kwa muda mrefu ndiyo sababu kubwa ya kupata maumivu ya shingo. Kitaalam binadamu anatakiwa kukaa sehemu moja kwa muda wa dakika 15 tu,” amesema Dk Sultan.

Ufanye nini kutuliza maumivu ya shingo?

Kama ni miongoni mwa watu ambao wanapata maumivu ya mara kwa mara ya shingo, basi wabunifu wametengeneza kifaa maalum kinachosaidia utendaji mzuri wa misuli ya shingo na kukuepusha na maumivu yote. 

Kifaa hicho, kinaitwa NeckMassager ambacho mtu anaweza kuvaa sehemu yoyote alipo ambapo humsaidia kunyoosha misuli ya shingo na kuhakikisha kunakuwa na mzunguko mzuri wa damu katika mishipa ya shingo yake. 

Mhusika anatakiwa kuvaa kifaa hicho cha kielektroniki shingoni wakati akiendelea na shughuli zake au akiwa amelala ili kuiimarisha shingo yake.


Zinazohusiana:


Pia siyo tu inasaidia kuondoa maumivu ya shingo, hata ya kichwa, kwa sababu maumivu hayo wakati mwingine husababishwa na kukaza kwa mishipa na misuli ya shingo. 

NeckMassager, ni kifaa kimoja tu. Vipo vifaa vingi vya muundo tofauti ambavyo vinaweza kukusaidia kulingana na mahitaji na changomoto unayopata kutegemeana na mazingira uliyopo. 

Hata hivyo, Dk Sultan anasema kabla ya kutumia teknolojia ni vema watu wajenge utamaduni wa kufanya mazoezi ya viungo mara kwa mara hata wakiwa kazini.

Pia wanashauriwa kutokukaa sehemu moja kwa muda mrefu ili kujiweka katika nafasi ya kutokuuchosha mwili. 

Enable Notifications OK No thanks