Unayotakiwa kuzingatia wakati wa kutembelea mbuga za wanyama usiku

November 11, 2019 1:13 pm · TULINAGWE ALSON
Share
Tweet
Copy Link
  • Unatakiwa kufuata utaratibu uliowekwa na Tanapa ikiwemo kuomba kwa njia ya mtandao.
  • Pia utalii huo unatakiwa kusimamiwa na waongozaji watalii na askari wanyamapori ili kuhakikisha usalama wa wageni. 
  • Utalii nyakati za usiku huusisha kutembelea mbuga na kujionea wanyama ambao ni vigumu kuwaona mchana. 

Dar es Salaam. Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) limetoa mwongozo wa kuzingatiwa na  watalii wanaopenda kutembelea mbuga za wanyama nyakati za usiku ili kujionea mandhari nzuri ya maeneo hayo na wanyama ambao siyo rahisi kuwaona mchana. 

Utalii huo ambao unajulikana kama “Night game drive” huusisha waongoza watalii kuwatembeza wageni katika maeneo mbalimbali ya mbuga na mapori wakati wa usiku kwa lengo kujionea wanyama na viumbe mbalimbali wakiwemo popo, fisi na baadhi ya jamii ya nyoka.

Pia hutumiwa na watafiti wa wanyamapori kuendesha shughuli zao kwa saa 24 ili kupata matokeo yaliyokusudiwa. 

Kwa Tanzania, Hifadhi za Taifa za Manyara na Tarangire ni miongoni mwa maeneo ambayo unaweza kufanya utalii nyakati za usiku. 

Kwa mujibu wa mwongozo  uliotolewa na Tanapa Agosti 2019, utalii huo wa usiku unatakiwa kusimamiwa vizuri na waongazaji watalii wenye uzoefu na maeneo ambayo wanawapeleka wageni ili kuwahakikishia usalama wao.

Ili muongoza watalii afanye kazi hiyo anatakiwa kuwa na leseni kutoka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), awe na rekodi safi, utalaam wenye weledi kwenye kazi yake. 

Kwa watalii wanapaswa kujaza fomu maalum inayoanisha taarifa zao kabla ya kuanza kutembelea mbuga usiku ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufanikisha matembezi yao. 


Zinazohusiana:


Mambo ya kuzingatia mkiwa mbugani

Tanapa inaeleza katika mwongozo huo kuwa, baada ya kupata kibali cha kuingia katika hifadhi wakati usiku, gari inayoruhusiwa ni ile yenye magurudumu manne na yenye uwezo wa kubeba watu 16 na siyo zaidi. 

Lakini kwa kila msafara hautakiwi kuzidi magari matatu na taa za kumurika maeneo mbalimbali hazitakiwa kuzidi mbili ili kupunguza mwanga mkubwa. 

Waongozaji watalii wanakumbushwa kuhakikisha shughuli hiyo inafanyika kwa ustarabu mkubwa ili kupunguza athari kwa wanyamapori pamoja na mazingira ya hifadhi. 

Kutokana na ukweli kuwa hifadhi zinakuwa na shughuli mbalimbali, watalii wanaofanya utalii nyakati za usiku wanatakiwa kuheshimu watumiaji wengine wa hifadhi ili kuepusha usumbufu usio wa lazima. 

Utalii huo ambao unajulikana kama “Night game drive” huusisha waongoza watalii kuwatembeza wageni katika maeneo mbalimbali ya mbuga na mapori wakati wa usiku kwa lengo kujionea wanyama na viumbe mbalimbali wakiwemo popo, fisi na baadhi ya jamii ya nyoka. Picha|Mtandao.

Usalama na muda wa kufanya utalii huo

Tanapa inaeleza kuwa usalama wa watalii ni suala la kwanza. Waongozaji watalii wanatakiwa kubeba vifaa vya huduma ya kwanza ili kujihadhari na dharura inayoweza kutokea wakati wakitembea mbugani. 

“Askari wanyamapori wanatakiwa kuwasindikiza watalii wakati wa zoezi hilo la usiku,” inaeleza sehemu ya mwongo huo ambao unapatikana katika tovuti ya Tanapa. 

Hata hivyo, utalii huo hautakiwi kufanyika kwa muda mrefu kama ilivyo kwa wanaotembea mchana. Muda uliowekwa ni kuanzia saa 1:00 usiku hadi saa 5:00 usiku. 

Tanapa inaeleza kuwa mwongozo huo ni sehemu ya mikakati yake ya kulinda na kuendeleza hifadhi za Taifa na maliasili zilizopo ndani yake ili kuongeza mapato yatokanayo na utalii. 

Enable Notifications OK No thanks