Kicheko, kilio bei mpya za mafuta ya petroli, dizeli

January 2, 2020 8:18 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Bei za rejareja za petroli kwa mwezi Januari iliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam imeongezeka kwa asilimia 2.07.
  • Watumiaji wa vyombo vya moto watalipia Sh45 kwa lita zaidi ya bei ambayo walikuwa wananunulia Desemba 2019. 
  • Bei za rejareja za dizeli zimepungua kwa Sh5 kwa lita sawa na asilimia 0.21. 

Dar es Salaam. Wakati mwezi Januari ukitajwa kuwa mgumu kwa wazazi wenye watoto wanaosoma katika shule mbalimbali Tanzania, baadhi ya watumiaji wa mafuta ya petroli kuendesha vyombo vya moto watakuwa na maumivu baada ya nishati hiyo kupanda. 

Hatua hiyo inakuja baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei mpya kikomo za mafuta za mwezi Januari 2020 na kuonyesha kuwa bei za rejareja za petroli iliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam imeongezeka kwa asilimia 2.07.

Kutokana na ongezeko la bei hiyo, watumiaji wa vyombo vya moto watalazimika kutoboa mifuko yao, ambapo watalipia Sh45 kwa lita zaidi ya bei ambayo walikuwa wananunulia Desemba 2019. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Nzinyangwa Mchany, mabadiliko haya yanatokana na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia na ongezeko la gharama za usafirishaji.

Vilevile, ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita la Desemba 2019, bei za jumla za petroli zimeongezeka kwa Sh44.53 kwa lita (sawa na asilimia 2.19).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Nzinyangwa Mchany, mabadiliko haya yanatokana na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia na ongezeko la gharama za usafirishaji. Picha| Alwin Kroon/Unsplash.

Hata hivyo, mwenendo wa bei za rejareja za petroli inayoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam zimekuwa za kupanda na kushuka, jambo ambalo limekuwa likiwapa ahueni na maumivu watumiaji wa vyombo vya moto.

Mathalani, bei za rejareja za petroli kwa mwezi Novemba 2019 inayoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam ziliongezeka kwa asilimia 4.67 ikilinganishwa na mwezi uliotangulia wa Oktoba. 

Lakini mwezi uliofuata wa Desemba 2019, bei hizo zikapungua kwa asilimia 1.39 kabla ya kupanda tena mwezi huu wa Januari. 

Hata wakati bei za petroli zikipanda, bei ya dizeli kwa mwezi Januari iliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam, imepungua kwa Sh5 kwa lita sawa na asilimia 0.21.


Soma zaidi: 


Wengine kwao ni ahueni

Wakazi wa mikoa ya Kaskazini na Kusini mwa Tanzania wataendelea kutumia bei zilizokuwepo Desemba 2019 kwa sababu ya kutokuwepo kwa mabadiliko ya bei.

Kwa mwezi Januari 2020, bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara hazina mabadiliko na zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo lililopita la Desemba 4, 2019

“Vilevile, kwa mwezi Januari 2020, bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya Petroli na Dizeli kwa Mikoa ya Kusini (Lindi, Mtwara na Ruvuma) hazina mabadiliko na zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo lililopita la tarehe 4 Desemba 2019,” inaeleza sehemu ya taarifa ya Ewura. 

Hiyo ni kwa sababu, kwa mwezi Desemba 2019, hakuna shehena ya mafuta iliyopokelewa kupitia bandari ya Mtwara na Tanga. Aidha, kwa kuwa hakuna mafuta ya taa yaliyopokelewa katika bandari ya Mtwara, wamiliki wa vituo vya mafuta katika mikoa tajwa, Ewura inawashauri kununua mafuta hayo kutoka Dar es Salaam na hivyo bei za rejareja za mafuta ya taa kwa mikoa hiyo zinatokana na gharama za mafuta hayo kutokea Dar es Salaam na kusafirishwa hadi mkoa husika.

EWURA inaukumbusha umma kuwa bei kikomo za mafuta kwa eneo husika, zinapatikana pia kupitia simu za mkononi kwa kupiga namba *152*00#

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW