Hifadhi ya Taifa ya milima Mahale nyumba ya maelfu ya wanyamapori

January 16, 2020 9:14 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni hifadhi inayotunza wanyama na mimea mingi kwenye ardhi yenye ukubwa wa Kilometa za mraba 1,613.
  • Kati ya wanyama waishio kwenye hifadhi hiyo, baadhi hawapatikani kwingine duniani.
  • Muda mzuri wa kutembelea hifadhi hiyo, ni msimu wa ukame yaani Mei hadi Oktoba.

Dar es Salaam. Msitu wa mianzi, miti ya kutosha kuficha milima na ardhi iliyopambwa kwa kapeti la majani asilia kiasi cha kushindwa kuona mchanga pale unapoutafuta ni kati ya sifa zinazoifanya  hifadhi ya Taifa ya Milima Mahale kuwa ya kipekee.

Upekee wa hifadhi yenye ukubwa wa kilometa za mraba 1,613 ndiyo unaifanya kuwa kivutio kikubwa cha watalii wa ndani na nje ambao wanakwenda kwa shughuli za mapumziko kupata hali ya hewa nzuri  na utulivu. 

Hifadhi hiyo ambayo inahifadhi aina takriban 337 za ndege, ni kati ya hifadhi adimu nchini Tanzania huku kati ya ndege hao wanafungamana na mazingira ya Milima ya Mahale pekee kwa maana ya kuwa hawapatikani sehemu nyingine yeyote duniani.

Miongoni mwa ndege hao ni bundi mvuvi anayefahamika kwa jina la “Pel’s fishing owl” ambaye samaki na vyura wanaoishi kwenye bonde la Albertine ambalo lipo Afrika Mashariki hufikiria kifo kila wakimuona.

Zaidi, Mahale inahifadhi takribani aina za sokwe 700 hadi 1,000 na hivyo kuifanya kuwa kati ya hifadhi chache duniani iliyofanikiwa kuwalinda viumbe hao.


Zinazohusiana:


Maajabu ya Mahale  yatakuacha mdomo wazi kwani ina nyani wa njano, bluu, nyani aina ya “Red colubus” na “Pied Colubus” huku nyani aina ya “Vervet” wakipatikana katika hifadhii hiyo pekee duniani.

Zaidi, takribani aina tatu ya wanyama waitwao Golago au “Bushbabies” wanaishi kwenye hifadhi hiyo ambayo Ziwa Tanganyika ni sehemu ya vivutio vyake. 

Ziwa hilo ni la pili kwa urefu na kina kirefu kwenda chini duniani kati ya maziwa yenye maji baridi (Fresh water).

Ziwa Tanganyika ni nyumba ya takribani aina 400 za samaki ikiwemo samaki aina ya “Cichlids” ambao asilimia 98 ya samaki hao hawapatikani sehemu nyingine yoyote duniani.

Hifadhi hiyo inafikika kirahisi ukiwa mkoani Kigoma kwa kutumia boti, gari au ndege. Kufika Hifadhi ya Milima Mahale kwa kutumia boti ya mwendokasi ambazo huratibiwa na wafanyakazi wa hifadhi ni kati ya saa nne hadi tano.

Lakini kama utatumia mitumbwi utafika katika hifadhi hiyo baada ya saa 15 kutoka Kigoma mjini. 

Muda mzuri wa kutembelea hifadhi hiyo, ni msimu wa ukame yaani Mei hadi Oktoba.

Enable Notifications OK No thanks