Unakutana na mpenzi wako kwa mara ya kwanza? Zingatia haya

January 17, 2020 8:04 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Vaa nguo zinazoendana na mazingira unayokwenda kukutana na mpenzi wako.
  • Tafuta eneo ambalo utamudu gharama zake.
  • Jitahidi kuwa halisi na epuka kuigiza maisha.

Dar es Salaam. Huwa inakuwa ni pata shika katika chumba cha mtu anayejiandaa kwenda kuonana na mpenzi wake kwa mara ya kwanza. Siku hiyo, hata mwenye kabati lililopangika hujikuta akijaribu kila nguo kuona ni ipi itampatia muonekano mzuri.

Kama wewe ni miongoni mwa watu ambao wanapata shida katika kuchagua nguo ya kuvaa wakati mtoko wa aina yoyote ile basi dondoo hizi zinawaweza kukusaidia kurahisisha maisha na ukapanga nguo nzuri: 


Fahamu rangi unazozipenda

Unakumbuka yale maongezi ya mwanzo ulipoulizwa “unapenda rangi gani?” Haswaa, huu ni muda wa kuanza kuzingatia rangi, licha ya kuwa wanaume, kwao ni changamoto katika kuchagua rangi. 

Endapo mpenzi wako anapendelea rangi ambayo haipo miongoni mwa nguo zako kabati lako, ni vema ukaanza kulifikiria.

Kwa binti, ni muhimu kuvaa rangi ambayo inaendana na ngozi yako hasa endapo baadhi ya sehemu ya mwili wako kama miguu na mikono zikiwa zinaonekana. 

Kama unakaa kwenye jiji lenye joto kama Dar es Salaam, epuka kuvaa nguo nyeusi majira ya mchana kwani itakulazimu jujifuta futa jasho kutokana na nguo hizo kusababisha joto mwilini.


Fahamu sehemu unayoenda kukutana na mpenzi wako

Huenda mna miadi ya kukutana ufukweni na wewe ukajikoki kwa kuvaa viatu virefu yaani “high heels” utaishia kulazimika kuvivua na kutembea peku.

Kabla hujaonana na umpendaye, dasisi sehemu unapoenda na muda wa kuonana naye ili kuepuka kukosa amani kiasi cha kutokufurahia na mpenzi wako.

Haijalishi kama utaenda kula mihogo kwenye ufukwe wa Coco beach Masaki au kufurahia sharubati ya Mac Juice Sinza na uji wa Habpap wa Idriss Magesa, kinachojalisha zaidi ni muda ambao utatumia na mpenzi wako. Picha|  Blue ocean strategy.

Kuwa halisi

Ni kweli kila mtu anapotarajia kumuona mpenzi wake anatarajia kuhisi dunia yote inasimama na kumuona yeye pekee ndiyo anatembea.

Anatarajia kuona nyota nyota na kushindwa kuamini kama yeye ndiye anamiliki penzi lako. Ni kwanini umuondolee mpenzi wako wasaa huo kwa kujibadilisha kiasi cha kukusahau?

Wasichana wengi hujikuta wakijipodoa kupitiliza na hivyo kuwafanya wapenzi wao kuwasahau kabisa mpaka watambilishwe tena. Jitahidi kuwa halisi kwa kuepuka kujipodoa sana ili mpenzi wako azidi kukupenda kwa jinsi ulivyo.

Hii itakusaidia hata ikitokea siku umekosa hela ya kununua vipodozi, utabaki yule yule ambaye mpenzi wako amezoea kukuona. 


Waulize rafiki zako juu ya muonekano wako

Kuna wakati mwingine unaweza kuona umeyaweza mambo na unafanana na mwanadada Nancy Sumari kumbe wala haupo kwenye hali ya kutazamwa mara mbili.

Jaribu kuuliza rafiki zako kama umependeza ili kama nywele zako haujachana au kinywa chako kinatoa harufu kidogo au nguo uliyovaa haiendani na wewe uweze kulitatua suala hilo mapema.


Zinazohusiana


Nenda sehemu unayoimudu

Hauna haja ya kuonyesha umwamba wako kwa kumpeleka mpenzi wako sehemu ya gharama ilhari ukijua pochi yako inapumulia mashine.

Haijalishi kama utaenda kula mihogo kwenye ufukwe wa Coco beach Masaki au kufurahia sharubati ya Mac Juice Sinza na uji wa Habpap wa Idriss Magesa, kinachojalisha zaidi ni muda ambao utatumia na mpenzi wako.

Ijumaa ijayo tutaongelea namna unavyoweza kufurahia muda wako ukiwa “Single” baki na Nukta.

Enable Notifications OK No thanks