Njia rahisi za kukabiliana na ongezeko la joto mwilini

January 10, 2020 7:57 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Hakikisha kabati lako lina nguo za kuvaa misimu yote ikiwemo kipindi cha joto kali.
  • Unashauri kuepuka kuvaa nguo nzito na zinazovuta joto. 
  • Kunywa maji mengi na wakati wa kulala vaa nguo nyepesi. 

Dar es Salaam. Katika kituo cha daladala cha Victoria, jijini Dar es Salaam barobaro amesimama akingojea gari la kuelekea katika shughuli zake za maisha. 

Tofauti na wenzake walio naye kituoni hapo, kijana huyo amevalia koti la suti la rangi ya udongo akifananisha rangi hiyo na suruali iliyonyooshwa kiasi cha kukata upepo huku viatu viking’aa mithiri ya kioo ambacho mlimbwende Flaviana Matata hukitumia kila asubuhi.

Kinachoendelea kumpatia umaridadi zaidi barobaro huyo, ni sweta aina ya kaba shingo lisilo na kifungo hata kimoja lenye rangi nyeusi lililovaliwa ndani ya koti kama mbadala wa shati na kukamilisha vazi lake la siku ambayo ina joto la kiwango cha sentigredi 33.

Hata baada ya Mamlaka ya Hali ya hewa Tanzania (TMA) kuonya juu ya ongezeko la kiwango cha joto katika baadhi ya mikoa nchini, huenda baadhi ya wakazi wa jijini Dar es Salaam walifikiri hautatimia.

“Vipindi hivi vya joto kali vinatarajiwa kuendelea kuongezeka katika mwezi Februari 2020 ambapo jua litakua la utosi hapa nchini,” imesomeka taarifa ya TMA iliyotolewa Januari 6, 2019. 

Ukivaa nguo za kukuachia kidogo, itakupunguzia adha ya kuonekana umeloa pale jasho linapotoka katika mwili wako. Picha| Texas A&M.

Kama wewe ni maridadi wa mitindo, tumia dondoo hizi kuhimili na kukabiliana na  joto hasa katika jiji la Dar es Salaam na Tanga ili kukuhakikishia afya njema:


Hakikisha kabati lako lina nguo za kuvaa misimu yote

Mbunifu wa mavazi wa kampuni ya kushona nguo za kiume ya Mtani Bespoke, Mtani Nyamakababi amesema ni muhimu kufahamu kuwa kila nguo ina msimu wake. Licha ya baadhi ya wafanya kazi kufungamana na mavazi fulani, bado wanaweza kuepuka mateso ya joto kwa kuwa na nguo zinazoendana na msimu.

“Cha kuzingatia ni malighafi ambazo zimetumika kutengeneza nguo. Malighafi aina ya Linen (kitani) zinafaa kuvaliwa kwani ni nyepesi na zinapitisha hewa. Usivalie nguo za Silk (silika), lazima upate tabu,” amesema Mtani.

Licha ya kwamba nguo zinazoendana na msimu wa joto zinauzwa kwa bei ya juu, ni heri uingie gharama ili uwe na amani kwenye msimu wa joto ambao kwa mujibu wa TMA, kila mwaka unaanza Oktoba hadi Machi hasa katika mikoa inayopata vipindi viwili vya mvua kwa mwaka. 

“Shati lenye malighafi ya pamba linauzwa kwa Sh70,000, lenye linen huuzwa kwa Sh90,000 huku lenye material (malighafi) ya manyoya ya kondoo likiuzwa kwa bei ya juu zaidi kufikia Sh200,000 kwa shati moja,” amesema Mtani.


Fahamu

Najua umeshangaa gharama ya nguo hizo kwani huenda unazinunua kila mara kwa bei ya chini zaidi.

Mbunifu huyo wa mavazi amesema wakati mwingine, malighafi hizi huchakachuliwa kwa kuchanganywa na malighafi nyingine na zinakuwa siyo halisi. 

Mtani amesema “kuipata pamba inamtaka mtu ailime, aiandae na kutengeneza nyuzi na kisha vitambaa vya nguo na wool (pamba) itokanayo na manyoya ya kondoo ni ghali zaidi haiwezi kuuzwa kwa bei rahisi.”


Kuwa makini na rangi unayoichagua

Mbunifu wa mavazi, Frank Maston ambaye pia ni mwanamitindo amesema  nguo zenye rangi nyeusi hufyonza joto hivyo lazima zimpatie tafrani mtu aliyezivaa hasa katika maeneo yenye joto la juu. 

“Nguo kama “dark blue” (nyeusi) na yoyote yenye weusi lazima itakupa tabu. Valia nguo zinazoakisi mwanga ambao ni chanzo cha joto,” amesema Maston ambaye pia ni mwanamuziki.

Wakati wengi wakiogopa mashati meupe kwa kuwa hushika uchafu haraka, Maston amesema zipo rangi kama bluu bahari, njano nyepesi, pinki nyepesi na kijani cha tufaa (green aple) ambazo ni mbadala wa rangi nyeupe.

Nguo hizo zinaweza kukusaidia kupunguza hali ya joto katika mwili wako. ​

Wataalamu wa afya wanashauri kunywa maji mengi kwa kuwa msimu huu humfanya mtu kupoteza maji mengi. Picha| Folio.

Usivae nguo za kubana mwili

Hakika unahitaji kuusikia upepo unapovuma na huwezi kuipata hisia hiyo kama umevaa nguo za kubana.

Ukivaa nguo za kukuachia kidogo, itakupunguzia adha ya kuonekana umeloa pale jasho linapotoka katika mwili wako.

“Tuweka “jeans” za kubana pembeni kwa msimu huu. Vaa gauni au suruali isiyokubana pia vaa shati linaloachia ngozi yako kidogo. Lisikushike sana,” ameshauri Maston.


Zinazohusiana


Epuka kujifunika sana

Usinukuu vibaya! Haijaandikwa usivae kimaadili bali uvalie nguo zenye uwazi kiasi. Pale unapokuwa hauna shughuli za kiofisi, ni bora ukavalia kaptula na flana kubwa kiasi ili uipatie ngozi yako ahueni.

Kama hautojali, unaweza kuvaa “Ripped wear” (Nguo zilizo chanika kimtindo) au zile zenye matobo. Ndiyo, Alikiba huvaa nguo hizi kwenye shoo zake.


Kunywa maji mengi

Hakika huihitaji kuishiwa nguvu katikati ya safari yako au kuanza kuumwa kichwa. Kwa msimu huu wa joto, wataalamu wa afya akiwemo Jonas Kagua ambaye ni daktari kwenye Kituo cha Afya cha Ngarenanyuki jijini Arusha amesema “kunywa maji mengi kwani mwili wako unapoteza maji mengi pia.”

Ana ahueni ya joto yule anayefanya kazi kwenye ofisi yenye kiyoyozi lakini kama upo juani, unahitaji kunywa maji mengi ili kufidia maji ambayo mwili wako unayapoteza kwa jasho na hata haja ndogo.

Yapo mengi ambayo yanaweza kukusaidia yakiwemo ya kulala “nusu uchi” kipindi cha usiku ili kuepuka kuamka shuka na godoro lako likiwa limeloa jasho.

Enable Notifications OK No thanks