Apps hizi kukuepusha na uteja mitandao ya kijamii
- Mitandao inachukua sehemu kubwa ya maisha ya watu, jambo lilaloweza kuathiri afya na maendeleo ya mtu.
- Wataalamu wa usalama mtandaoni wanashauri elimu itolewe zaidi juu matumizi sahihi ya mtandao.
Dar es Salaam. Huenda wewe ni miongoni mwa watu ambao wanatumia muda mwingi kuperuzi kwenye mitandao ya kijamii. Ukitoka Facebook basi utaingia Instagram kuangalia picha mbalimbali za watu lakini unajikuta unavutwa kwenda Youtube kuangalia video.
Umekuwa ukitumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii kuliko shughuli za maendeleo au kupata muda ya kukaa na familia yako, na wakati mwingine umejikuta ukihatarisha afya yako kwa kukosa usingizi wa uhakika na kupata msongo wa mawazo. Na hata unapojaribu kujitoa kwenye hali hiyo unashindwa kutoka.
Usiogope kwa sababu hauko peke yako. Tatizo hilo linawapata watu wengi duniani. Wataalam wa teknolojia ya mawasiliano wanaeleza kuwa kwa wastani mtu anaangalia simu yake mara 150 kwa siku lakini wengine ni zaidi ya hapo.
Hali hiyo huchochewa zaidi na miito iliyopo kwenye simu janja ambayo humjulisha mtumiaji kila ujumbe au bandiko linapoingia kwenye mtandao anaotumia na kulazimika kufungua simu mara kwa mara ili asipitwe na yanayoendelea katika ulimwengu wa digitali.
Unatokaje katika mkwamo huo? Kila teknolojia ina changamoto zake lakini zipo programu (Apps) ambazo zimetengenezwa maalum kukusaidia kudhibiti muda anaotumia kwenye mitandao na kujikita katika shughuli zingine za uzalishaji au mapumziko.
Mtandao wa Facebook ambao una watumiaji zaidi ya 2.23 bilioni duniani, umeanzisha App inayojulikana kama Muda Wako Kwenye Facebook (Your Time on Facebook feature) ambayo inamsaidia mtumiaji wa mtandao huo kufahamu muda aliotumia kuperuzi kurasa na ametumia muda mwingi zaidi aliopaswa kutumia inamletea ishara ya onyo (warning alert).
Pia inamuwezesha kutenga muda ambao anapenda kutumia kwa siku kuingia Facebook. App hiyo hufuatilia kwa karibu muda uliowekwa na ukiisha husitisha apps zinazokujulisha taarifa ya mabandiko mapya yanayoingia kwenye ukurasa wako.
Kwa watumiaji wa mitandao mingine kama Twitter, Instagram, Whatspp au barua pepe na michezo ya mtandaoni wanaweza kutumia Apps mbalimbali kujinasua na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
App ya AntiSocial ni mojawapo ya sehmu inakuwezesha kutumia muda wako vizuri ambapo unaipakua kwenye simu yako. Inachokifanya ni kukutumia ripoti za muda aliotumia na kujilinganisha na watu wengine wakiwemo marafiki, wafanyakazi wenzako au hata watu wenye umri sawa na wake. Ikiwa mtu atatumia muda zaidi ya aliojipangia, programu hiyo inamletea ujumbe wenye ishara ya hatari na kumtaka asitishe kutumia simu.
Pia unaweza kutumia App ya Offtime iliyotengenezwa mahususi kusimamia programu za simu ili zifanye kazi kwa kwa kiwango kinachopendekezwa na mmiliki. Ikiwa mtumiaji atazidisha muda aliojiwekea, App hiyo huzima programu zote za simu kwa muda uliopanga ili kukupa nafasi ya kutimiza majukumu mengine ya kikazi. Pia inakupa uchambuzi wa tabia na matumizi ya simu ya watu wengine ili kujiweka katika nafasi ya kufahamu mwenendo wa matumizi ya simu duniani.
Lakini ukiona Apps hizo hazijakusaidia kutoka kwenye uteja wa mitandao ya kijamii au simu basi App ya Space inaweza kuwa msaada kwako.
Awali ilikuwa inajulikana kama BreakFree, inampa mtu uhuru wa kujiwekea kanuni za kutumia simu yake. Ikiwa mtumiaji atakiuka kanuni alizojiwekea, humkumbusha na wakati mwingine humpa adhabu kwa kuzifungia programu za simu yake zisifanye kazi kwa muda fulani mpaka atimize masharti aliyowekewa.
Hata hivyo, ufanisi wa Apps hizo hutegemea zaidi utayari wa mtumiaji mwenyewe kuondokana na matumizi ya simu na mitandao ya kijamii iliyopitiliza, hazihusiki moja kwa moja na mabadiliko ya tabia ya mtu.
Matumizi ya mitandao ya kijamii yakizidi humfanya mtu kuwa mtumwa. Picha| southafricanrecoveryfilmfestival.com
Nini kifanyike?
Wachambuzi wa masuala ya teknolojia ya simu wanasema jambo la kwanza kabisa kwa mtu kuondokana na uteja wa mitandao ya kijamii kabla ya kutumia Apps ni kutambua kuwa kuna tatizo na kukubali kuondokana na tabia zisizofaa.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni usalama mtandaoni ya Kabolik, Robert Matafu anasema watu waliotharika na mitandao ya kijamii wanapaswa kupata elimu ya utendaji wa simu itakayowarahisishia njia ya kutoka kwemye uteja.
“Inaanza kwa kwenda kwenye simu za kawaida, tunahitaji kubadilisha mawazo yetu ili kupata matokeo chanya,” anasema Matafu.
Anabainisha kuwa ili kumaliza tatizo hilo ni vema zikaanzishwa kampeni za mtandaoni kuwatoa watu kwenye uteja wa mitandao ya kijamii, “Watanzania wanapenda matukio, kampeni kama #ZimaChallenge zitasaidia.”