Maadhimisho ya siku ya wanawake Tanzania 2026 kupambwa na vazi la batiki
- Vazi hili linatarijia kufungua fursa kwa wafanyabiasha na kuwaingizia kipato.
Dar es Salaam. Huenda maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yakawa ya aina yake nchini Tanzania mara baada ya Serikali kulitangaza vazi la batiki kuyapamba maadhimisho hayo kwa mwaka 2026.
Maadhimisho hayo ambayo hufanyika Machi 8 kila mwaka maeneo mbalimbali duniani hulenga kusheherekea mafanikio ya wanawake na kutambua mchango wao katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Ili kufungua milango ya fursa ya biashara hususan batiki Serikali imetangaza vazi hilo litakuwa sare rasmi ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka 2026, ikiwa ni hatua ya kuhamasisha matumizi ya bidhaa za ndani na kuinua wajasiriamali wa sekta hiyo.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima aliyekuwa akizungumza Februari 17,2026 alieleza kuwa lengo la kutumia vazi hiilo katika maadhimisho hayo ni kuwainua wazalishaji wa ndani.
“Kwa mwaka huu tumeamua tuvae vazi la batiki, kwa kadri mkoa utakavyokuwa umechagua aina hiyo ya batiki yao na lengo ni moja tu kuendelea kuwainua wajasiriamali wa ndani wa mikoa husika,” alisema Dk Gwajima.

Kwa wapenzi wa fasheni vazi hili si jipya, lilianza kuwa maarufu nchini Tanzania kuanzia miaka ya 1970 kabla ya kupotea na kuibuka tena na kupewa umaarufu zaidi na vijana wa kizazi cha sasa maarufu kama Gen Z.
Kwa kutangazwa kwa vazi hilo inamaanisha kuwa Serikali imeamua kuliweka kando vazi la kitenge ambacho kimekuwa kikivaliwa mara kwa mara katika maadhimisho hayo kikipigwa chapa na nakshi mbalimbali ikiwemo picha za viongozi wanawake au wake wa maraisi.
Huenda sasa juhudi za kuitangaza batiki zinaanza kuzaa matunda tangu kufuatia uzinduzi wa Siku ya Batiki Tanzania uliofanyika Julai 9, 2022, katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba.
Wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Roijok Progress Centre Rose Urio alieleza kuwa siku hiyo ilianzishwa kwa lengo la kuifanya batiki itambulike kitaifa na kimataifa.
Wakati huo, zaidi ya wazalishaji 800,000 kutoka vikundi 180 nchini walikuwa wanategemea batiki kama chanzo cha kipato.

Machi 8 ya kitofauti
Kwa mujibu wa Dk Gwajima, tofauti na maadhimisho ya kitaifa yanayofanyika eneo moja mwaka huu maadhimisho yatafanyika katika ngazi zote kuanzia vijijini, mitaa, kata, halmashauri, wilaya hadi mikoa kwa kufuata mwongozo uliotolewa na Serikali.
Maadhimisho ya siku hii yataongozwa na kauli mbiu inasemayo “Haki na usawa kwa wanawake na wasichana: Msingi jumuishi wa ufikia Dira 2050.”
Kauli mbiu hiyo inalenga kuhamasisha maendeleo jumuishi, kutambua haki za wanawake na wasichana na kuhakikisha utekelezaji wake kwa vitendo ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Latest