Serikali yaahidi mazingira rafiki kuongeza idadi ya redio Tanzania
- Dk Mwakyembe amesema Serikali itaendelea kuenzi mchango na kazi nzuri inayofanywa na vituo vya redio nchini
Dar es Salaam. Waziri wa habari, utamaduni, Sanaa na Michezo Harrison Mwakyembe amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya uanzishaji wa redio nyingi zaidi nchini ili kuenzi mchango wa redio hapa Tanzania.
Dk Mwakyembe ameeleza leo (Februari 13, 2020) katika taarifa iliyotolewa na wizara yake kuwa redio zimekuwa zikifanya kazi nzuri zenye mchango mkubwa kwa Taifa.
“Serikali ya Tanzania itaendelea kuenzi mchango na kazi nzuri inayofanywa na redio hapa nchini ikiwemo kuendelea kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya uanzishaji wa redio nyingi zaidi,” amesema Dk Mwakyembe katika ujumbe wake wa maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani.
Siku ya redio ulimwenguni huadhimishwa kila mwaka baada ya Umoja wa Mataifa (UN) kuitangaza rasmi Februari 13, 1946ili kuelimisha na kuhamasisha umuhimu wa redio. Siku hiyo ndiyo redio ya umoja wa mataifa ilianzishwa.
Zinazohusiana:
Hadi kufikia Februari 12, 2020, waziri huyo amesema Tanzania ilikuwa na vituo vya redio 204 vilivyosajiliwa hapa nchini vikiwemo 21 vya masafa ya mtandaoni (online radio) hali inayowafanya Watanzania kupata haki yao ya msingi ya kikatiba.
Wadau mbalimbali wa redio nchini nao wameeleza namna redio zilivyosaidia kubadilisha maisha yao ikiwemo kuwapa ajira.
“Redio imebadilisha maisha yangu. Redio imenisaidia kutafuta wito wangu. Ntazidi kuipenda redio,” amesema Michael Baruti, mwanahabari wa Shirika la habari la Uingereza (BBC) kupitia ukurasa wa Twitter.
Radio changed my life… Radio helped me to find my calling… Radio will always have my heart… Happy World Radio Day
— Michael Paul Baruti (@michaelbaruti) February 13, 2020