Wanaomiliki redio Tanzania wapungua, televisheni wapaa

Daniel Samson 0951Hrs   Julai 01, 2019 Teknolojia
  • Waliokuwa wanamiliki redio mwaka 2011/2012 walikuwa asilimia 55 kabla ya kushuka hadi kufikia asilimia 43 mwaka 2017/2018. 
  • Wanaomiliki televisheni wameongezeka kutoka asilimia 16 hadi asilimia 24 mwaka jana. 
  • Maendeleo ya teknolojia ya simu za mkononi yachangia mabadiliko hayo. 
  • Redio bado kimebaki kuwa chombo cha kuaminika kwa watu kupata habari. 

Dar es Salaam. Idadi ya Watanzania wanaomiliki televisheni imezidi kuongezeka nchini huku wale wanaomiliki redio kama chombo cha kupata habari na burudani wakizidi kupungua kwa kasi.

Ripoti mpya ya mapato na matumizi ya kaya mwaka 2017/18 iliyotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imebainisha kuwa idadi ya Watanzania waishio Tanzania bara wenye redio imeshuka hadi asilimia 43 mwaka 2017/2018 kutoka asilimia 55 iliyorekodiwa mwaka 2011/2012.

Hiyo ni sawa na anguko la asilimia 12 ndani ya kipindi cha miaka saba iliyopita au sawa na kusema, kwa sasa Watanzania 43  kati ya 100 ndiyo wanamiliki redio ambazo huzitumia kupata habari mbalimbali za ndani na nje ya nchi. 

Kushuka kwa Watanzania wanaomiliki redio kulianza kujidhihirisha mwaka 2007 ambapo katika kipindi hicho ilikuwa ni theluthi mbili au asilimia 66 kabla haijaporomoka kufikia asilimia 55 mwaka 2011/2012. 

Hata hivyo, wachambuzi wanaeleza kuwa huenda wamiliki wamepungua kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya simu za mkononi ambazo kwa sasa zinatoa na huduma ya redio kwa masafa ya FM. 

Katibu Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) , Neville Meena ameiambia www.nukta.co.tz kuwa mabadiliko ya teknolojia yamerahisisha upatikanaji wa taarifa, jambo linalowafanya watu wasitegemea tu redio za nyumbani kupata habari. 

Amesema wakati mwingine malengo ya kuanzisha vituo yanaweza kuathiri hata wasikilizaji kumiliki redio na kuwafanya kutafuta namna nyingine ya kupata habari kwa haraka na urahisi. 


Zinazohusiana:


Wakati Watanzania wakiendelea kuzitupa mkono redio, wanaelekeza macho yao katika kumiliki runinga (televisheni).

Ripoti hiyo inabainisha kuwa idadi ya watu wanaomiliki televisheni imeongezeka kutoka asilimia 16 mwaka 2011/2012 hadi asilimia 24 mwaka jana. 

Kwa viwango hivyo  vya wamiliki wa televisheni, tunaweza kusema bado redio ndio chombo muhimu ambacho wa Watanzania wanakitumia kupata taarifa lakini siku zijazo idadi hiyo inaweza kushuka zaidi. 

Zipo sababu mbalimbali ambazo zinazofanya redio ziendelee kuaminika ikiwemo ukuaji wa teknolojia ya simu za mkononi na intaneti ambapo mtu anaweza kusikiliza redio mahari popote kwa kutumia simu ya mkononi.

Wakati huo huo, wanaopenda kuandalia televisheni kwa kutumia simu janja, wanalazimika kuwa na kifurushi cha intaneti cha kutosha ikizingatiwa kuwa baadhi ya vituo televisheni vinarusha matangazo mtandaoni.

Wakati Watanzania wakiendelea kuzitupa mkono redio, wanaelekeza macho yao katika kumiliki runinga (televisheni). Picha|Mtandao.

Wakati kukiwa na mabadiliko ya umiliki wa redio na televisheni Tanzania bara, idadi ya vituo vya redio na televisheni inaongezeka kila mwaka, jambo linafungua fursa kwa wamiliki wa vituo hivyo kuangalia namna ya kuwafikia kwa ukaribu watu wanaokwenda na mabadiliko ya teknolojia ikiwemo matumizi ya intaneti kupata habari. 

Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) za mwaka 2018, hadi kufikia Desemba mwaka jana, kulikuwa vituo vya radio 158 na televisheni 51 na idadi hiyo imekuwa ikiongezeka kila mwaka. 

Umiliki wa vyombo vya mawasiliano ili kupata habari ni moja ya visharia vinavyotumika kupima mgawanyo wa mapato na matumizi katika kaya ili tathmini ya mwenendo wa ukuaji wa sekta ya mawasiliano na uchukuzi nchini Tanzania. 

Ripoti hiyo pia inaonyesha umiliki wa baiskeli kama chombo cha usafiri umeongezeka kutoka asilimia 4 mwaka 2011/2012 hadi asilimia 11 mwaka jana, jambo linaloonyesha usafiri bado unahitajika katika shughuli mbalimbali za maendeleo nchini. 

Kutokana na umuhimu wa baiskeli, Umoja wa Mataifa imetenga siku ya Juni 3 kila mwaka kuwa siku ya baiskeli duniani kwa sababu mbali na gharama zake, matumizi ya baiskeli ni safi na yanajali mazingira na ni usafiri endelevu. 

Related Post