Sababu za Tanzania kutowarejesha wanafunzi 420 waliopo China
Imesema kutokana na kuheshimu masharti na mahitaji ya karantini hiyo yanayozuia mtu yeyote kutoka ama kuingia katika mji huo kwa kusudi la kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo hadi hapo Serikali ya China itakapoondoa karantini hiyo. Picha|Mtandao.
- Yasema ni hatua ya kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo nchini.
- hadi sasa hakuna mwanafunzi au Mtanzania yeyote aliyebainika kuambukizwa virusi hivyo na kuwasihi kuendelea kuwa watulivu.
- Uganda nayo yakataa kuwarejesha nyumbani wanafunzi wake waliopo China.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema haina mpango wa kuwarejesha nchini wanafunzi 420 waliopo mji wa Wuhan nchini China kwa kuwa nchi zilizofanya hivyo zilisababisha kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona katika nchi husika.Imesema hadi sasa hakuna mwanafunzi au Mtanzania yeyote aliyebainika kuambukizwa virusi hivyo na kuwasihi kuendelea kuwa watulivu.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jana (Februari 14, 2020) inaeleza kuwa kwa sasa haifikirii kuwarejesha wanafunzi hao nchini na imewatoa hofu kuwa inaendelea kufuatilia hali zao kwa karibu.
“Wizara inapenda kuuhakikishia uma kwamba Serikali ya Tanzania haina mpango wa kuwaondoa ama kuwasafirisha wanafunzi hao walioko Wuhan kwa kuwa wako katika uangalizi maalum (quarantine) nchini humo,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali wa wizara hiyo, Emmanuel Buhohela.
Imesema kutokana na kuheshimu masharti na mahitaji ya karantini hiyo yanayozuia mtu yeyote kutoka ama kuingia katika mji huo kwa kusudi la kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo hadi hapo Serikali ya China itakapoondoa karantini hiyo.
Pia imebainisha kuwa uamuzi wa kutowaondoa ama kuwasafirisha wanafunzi hao kurejea nyumbani unatokana na taarifa za kitabibu zinazobainisha kutokea milipuko ya homa ya virusi hivyo katika mataifa ambayo awali yaliwaondoa wananchi wao wakati wa mlipuko na kusababisha kusambaa kwa virusi hivyo na kuleta madhara zaidi kwa mataifa hayo.
“Serikali pia inakamilisha mpango wa mawasiliano ya moja kwa moja kwa njia za simu (hotline) zitakazotumiwa na wataalamu wa saikolojia (psycho-social support) kwa ajili ya kuwapatia ushauri nasaha wanafunzi na wazazi wakati juhudi za kudhibiti mlipuko huo zikiendelea,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Zinazohusiana:
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), hadi kufikia jana Februari 14, 2020 watu 49,053 wameambukizwa ugonjwa huo duniani na vifo 1,381 vimeripotiwa ambapo visa zaidi ya asilimia 99 vikitokea China.
Nchi jirani ya Uganda nayo imesema kuwarudisha nyumbani raia wake kutoka Wuhan kunaweza kusababisha maambukizi hayo kufika katika nchi hiyo huku ikiongezea kwamba miundombinu ya Taifa hilo haiwezi kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo.
Hata hivyo, Serikali ya Uganda imesema kwamba inatuma dola za Marekani 60,000 ili kuwasaidia wanafunzi wake waliokwama katka mji wa Wuhan nchini China uliotengwa kufuatia mlipuko wa virusi vya corona.
Wiki iliyopita, WHO lilitangaza kwamba mlipuko wa virusi vya corona ni ugonjwa wa dharura kwa dunia nzima kwasababu ya hofu kwamba nchi maskini huenda zikashindwa kukabiliana na mlipuko huo.