Magufuli aagiza mfanyabiashara wa Mwanza kufidiwa Sh24 milioni

February 20, 2020 12:34 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link

“Swala langu likaenda Takukuru wakafanya uchunguzi Wizara ya Afya wakakuta kuna kasoro kwamba malalamiko yangu yalikuwa ya msingi. Takukuru wakanipa mrejesho wa maandishi…” amesema Mnyaga. Picha| Rodgers George.

  • Ni fidia ya hasara aliyoipata ikiwemo kufunga chuo cha afya alichowahi kukifungua mkoani Mwanza.
  • Ni baada ya kuhangaika kumtafuta Rais kwa muda mrefu bila mafanikio.
  • Mtoa huduma huyo amesema kwas asa amefirisika na anaishi maisha yasiyokuwa yake.

Dar es Salaam. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kulipa Sh24 milioni kwa mtoa huduma binafsi wa afya mkoani Mwanza, Godfrey Mnyaga kama fidia baada ya kulalamika kuwa urasimu wa serikalini umemsababishia hasara iliyotokana na sababu mbalimbali ikiwemo kufunga chuo chake cha afya mkoani humo.

Katika malalamiko yake kwa Rais Magufuli leo (Feb 20, 2020) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Madaktari Tanzania yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mnyaga aliyekuwa akimiliki chuo cha afya mkoani Mwanza, amesema aliletewa mitihani yenye dosari na alivyotoa malalamiko kwa mamlaka hayakuwafanyiwa kazi. 

Mnyaga amesema licha ya dosari hizo na kutoshughulikiwa jambo lake, aliingia gharama za kulipia mitihani ya wizara hiyo ili kuwawezesha wanafunzi hao kutimiza ndoto zao za masomo lakini dosari za mitihani hiyo zilijitokeza tena mwaka uliofuata. 

“Kweli nilikataa kupokea hiyo mitihani, wakachukua wanafunzi wangu wakawapeleka vyuo vingine,” amelalamika Mnyaga aliyekuwa akimiliki Chuo cha Gisan health training institute. 

Mnyaga amesema alipata hasara katika suala hilo ikiwemo gharama alizotumia kulipia mitihani hiyo. 

Baada ya hapo, mwekezaji huyo aliendelea kufuatilia haki yake bila mafanikio licha ya madai ya kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilithibitisha kuonewa kwake.

“Swala langu likaenda Takukuru wakafanya uchunguzi Wizara ya Afya wakakuta kuna kasoro kwamba malalamiko yangu yalikuwa ya msingi. Takukuru wakanipa mrejesho wa maandishi…” amesema Mnyaga.


Zinazohusiana


Heka heka za kufuatilia malalamiko yake zilimfikisha hadi kwa Katibu Mkuu wizara ya Afya bila mafanikio.

“Katibu Mkuu akaniita Dodoma nikaenda, nikamueleza, tukakutana nilipomuambia akafeel (aliona bayana) kabisa kwamba nilikuwa nimeonewa akasema nirudi mwanza,” amesema. 

Baada ya siku chache, Mnyaga alipokea barua kutoka kwa Katibu Mkuu ambayo majibu yake hayakuridhisha.

“Niliamua kufunga kabisa chuo, nilikuwa na mkopo benki, benki imenitia msukosuko mpaka leo nimefirisika naishi maisha ambayo hayakuwa ya kwangu.

“Kama inawezekana hawa watendaji wa afya wanifidie kwa sababu walinisababishia hasara,” amesema Mnyaga ambaye pia ameainisha amemtafuta Rais Magufuli kwa muda mrefu bila mafanikio.

Kutokana na maelezo hayo, Rais Magufuli ametoa maagizo kwa wizara hiyo kumlipa fidia ya Sh24 milioni baada ya kupitia nyaraka zilizowasilishwa kwake na Mnyaga zilizooonyesha uthabiti wa malalamiko yake.

“Mumrudishie milioni zake 24 na mshughulikie issue (suala) yake kwa sababu nimejaribu “kucheki” kwenye “communication” (mawasiliano) ambazo zipo barua za PCCB na kadhalika inaonyesha walivyokuwa wanaandika kuwa  ana kesi ambayo alionewa. 

Rais ameagiza kuwa wizara hiyo iimpatie fedha hizo “ikiwezekana ndani ya siku mbili muwe mmeshamrudishia. 

Enable Notifications OK No thanks