Makamba azishauri benki, kampuni za simu kuondoa tozo za simu benki

March 19, 2020 1:57 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ameshauri kuondolewa tozo za malipo kwa miamala hiyo isiyozidi Sh50,000 kipindi hiki ambacho ugonjwa wa Corona unasambaa kwa kasi
  • Amesema hilo likifanyika kwa miezi mitatu litasaidia kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi.
  • Benki, kampuni za simu zamjibu. 

Dar es Salaam. Aliyekuwa Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba amezishauri benki na kampuni za simu nchini Tanzania kuondoa tozo za malipo kwa miamala ya fedha inayofanyika kielektroniki isiyozidi Sh50,000 kipindi hiki ambacho ugonjwa wa Corona unasambaa kwa kasi. 

Ushauri huo wa Makamba unakuja muda mfupi baada ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuwataka wananchi kufanya miamala kwa  njia mbadala ikiwemo za simu, kadi na intaneti ili kupunguza matumizi ya pesa taslimu.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo, BoT imeleeza kuwa kutokana na pesa hasa noti kupita katika mikono ya watu wengi, inaweza kusababisha kusambaa kwa virusi vya Corona.  

Makamba ambaye ni Mbunge wa jimbo la Bumbuli mkoani Tanga ametoa ushauri huo leo (Machi 19, 2020) katika ukurasa wake wa Twitter ikiwa ni hatua ya kuzihimiza taasisi za fedha kuwapunguzia gharama wananchi kipindi hiki ambacho duniani inakabiliwa na janga la Corona.

Amesema taasisi hizo ziondoe kabisa tozo kwa miamala yote isiyozidi Sh50,000 kwa muda wa miezi mitatu na kuongeza kuwa hilo linawezekana kufanyika wakati huu. 

“Katika kuhamasisha wananchi kutumia njia mbadala za malipo, kampuni za simu na mabenki yaondoe tozo za malipo kwa njia ya kielektroniki kwa miamala isiyozidi shilingi 50,000 kwa muda wa miezi mitatu. @VodacomTanzania @Tigo_TZ @airtel_tanzania @tba_forbankers hii mnaweza #COVID19,” ameandika Makamba katika ukurasa wake wa Twitter. 

Katika kuhamasisha wananchi kutumia njia mbadala za malipo, kampuni za simu na mabenki yaondoe tozo za malipo kwa njia ya kielektroniki kwa miamala isiyozidi shilingi 50,000 kwa muda wa miezi mitatu. @VodacomTanzania
@Tigo_TZ
@airtel_tanzania
@tba_forbankers hii mnaweza #COVID19
https://t.co/q4E0L0m9Pt

Amesema hatua hiyo itaongeza hamasa kwa wananchi kutumia njia mbadala za malipo ya mtandaoni ambazo ni salama na rahisi. 

Wafuasi wa Makamba ambaye mpaka kufikia leo mchana alikuwa na wafuasi  wamempongeza kwa ushauri huo huku wengi wakibainisha kuwa utasaidia kuwapunguzia wananchi ukali wa maisha.

“Wanatakiwa kuondoa kwa muda gharama za kutoa ama kupokea pesa na hii itakuwa ni hamasa sana kwa watu. Masterpass  Qr na Mastercard elimu itolewe kwa umma zaidi katika kipindi hichi,” amesema DonaldsonJr @DonaldmathewJr

Baadhi ya nchi ikiwemo Ghana, Kenya na Rwanda tayari zimechukua hatua ya kupunguza toza za miamala ya mtandaoni na kodi kwa kushirikiana na makampuni ya simu na benki za biashara ili kuhimiza matumizi ya miamala ya kielektroniki. 


Zinazohusiana


Kampuni za simu, benki zamjibu Makamba

Kupitia mtandao wa Twitter, baadhi ya kampuni za simu na benki za biashara nchini zimeeleza kuwa zimepokea ushauri uliotolewa na Makamba na wanaangalia uwezekano wa kufanikisha suala hilo. 

 “@JMakamba kwa ushauri mzuri ambao sisi kama taasisi ya kifedha tunaupokea na kuangalia ni namna gani tunaweza lifanikisha hili,” inasomeka sehemu ya ukurasa wa Benki ya Access Tanzania (@AccessBank_Tz). 

Kampuni za Vodacom, Airtel na Tigo zimemjibu Makamba na kumueleza zimepokea ujumbe huo ambao ukifanyiwa kazi unaweza kuwaletea wananchi ahueni. 

“Habari, tunashukuru kwa kuwasiliana nasi. Tunapenda kukuhakikishia kuwa maoni yako na ushauri tumeyapokea na tunaahidi kuyazingatia, lakini kwa sasa tunashauri kuendelea kutumia huduma za Airtel money kufanya miamala kwa utaratibu uliopo, ahsante,” inasomeka sehemu ya ujumbe wa ukurasa wa Twitter wa Airtel. 

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Tanzania ina wagonjwa sita wa virusi vya Corona. 

Ugonjwa huo ambao unasambaa kwa kasi duniani  kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO) umepoteza maisha ya watu 7,807 na 191,127 wameambukizwa duniani hadi jana.

Enable Notifications OK No thanks