Wagonjwa wa Corona wazidi kuongezeka Tanzania, sasa wafikia 19

March 30, 2020 12:43 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Wagonjwa wengine watano wathibitika leo.
  • Dar yaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi.
  • Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu awataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huo. 

Dar es Salaam. Idadi ya wagonjwa wa virusi vya corona nchini  imezidi kuongezeka baada ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu kubainisha leo ongezeko la wagonjwa wengine watano na kufanya Tanzania kuwa na wagonjwa 19.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo (Machi 30, 2020) Waziri Mwalimu amesema wagonjwa hao wamethibitika kuwa na ugonjwa huo baada ya kupimwa katika maabara kuu ya Taifa jijini Dar wa Salaam.

“Kati ya wagonjwa hawa, watatu ni kutoka Dar es Salaam na wawili kutoka Zanzibar ambao taarifa zao zitatolewa na Waziri wa Afya Zanzibar,” inaeleza taarifa hiyo iliyotolewa leo ( Machi 30, 2020) mchana.

“Hivyo sasa jumla ya wagonjwa wa COVID-19 ni 19 akiwemo mmoja aliyetolewa taarifa za Waziri wa Afya Zanzibar tarehe 28/3/2020,” imeeleza taarifa hiyo.

Akizungumzia wagonjwa wapya wa Dar es Salaam, amesema yupo mwanaume wa miaka 49 ambaye ni Mtanzania ambaye alikutana na raia wa kigeni kutoka miongoni mwa nchi zilizoathiriwa na ugonjwa huo. 

Wagonjwa wengine wawili ni mwanamke (21) na mwanaume (49) ambao ni miongoni mwa watu ambao walikuwa wanafuatiliwa na mamlaka.


Zinazohusiana


Mpaka sasa mkoa wa Dar es Salaam  ndiyo unaongoza kuwa na wagonjwa wengi wa Corona wanaofikia 11 ukifuatiwa na visiwa vya Zanzibar (5), Arusha (2) na mmoja alithibitishwa katika mkoa wa Kagera.

“Kazi ya kufuatilia watu waliokutana na wagonjwa hawa inaendelea (contact tracing). Aidha tunawataka wananchi wote waendelee kuchukua tahadhari kujikinga na ugonjwa huu,” amesema Ummy katika taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) ugonjwa huo ameambukiza watu 634,835  na kuua watu 29,891 duniani kote huku juhudi za kutafuta dawa na chanjo zikiendelea.  

Enable Notifications OK No thanks