Bajeti wizara ya elimu yashuka tena

April 27, 2020 2:15 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Imeshuka kwa mara ya pili mfululizo hadi kufikia Sh1.34 trilioni katika mwaka 2020/2021.
  • Fedha za maendeleo nazo zimepungua hadi Sh857.5 bilioni kutoka Sh862.7 bilioni za mwaka 2019/2020.
  • Waziri Kivuli wa Elimu Suzan Lyimo ashauri Serikali kuongeza mkazo katika kuboresha mazingira ya kusomea. 

Dar es Salaam. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako ameliomba Bunge liidhinishe Sh1.34 trilioni kwa ajili matumizi ya mwaka 2020/2021 ikiwa ni pungufu kidogo kwa asilimia 2.8  ikilinganishwa na bajeti ya mwaka huu unaoishia mwezi Juni. 

Upungufu huo bajeti ni sawa na Sh37.9 bilioni ikilinganishwa na bajeti iliyopitishwa katika mwaka wa fedha wa 2019/20. Katika mwaka huu unaoishia Juni 30, Sh1.38 trilioni zilitengwa kuhudumia wizara hiyo muhimu nchini. 

Profesa Ndalichako aliyekuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake mwishoni mwa wiki bungeni jijini Dodoma,  amesema kati ya fedha hizo zilizoombwa, Sh857.5 bilioni au asilimia 63.5 ya bajeti ya wizara hiyo zitaelekezwa katika miradi ya maendeleo na fedha zilizobaki zitatumika kwa matumizi ya kawaida. 

Hata hivyo, kiasi cha fedha kilichoelekezwa katika miradi ya maendeleo kimepungua kidogo ukilinganishwa na makadirio ya mwaka huu unaoishia Juni ambapo wizara ilitenga Sh862.7 bilioni. 

Hiyo ina maana kuwa fedha zinazoelekezwa katika miradi ya maendeleo zimepungua kwa miaka miwili mfululizo tangu mwaka 2019/2020.

Lakini bado wizara hiyo imekuwa ikihakikisha fedha zinazoelekezwa kuboresha miradi ya elimu zinakuwa ni zaidi ya nusu ya bajeti yote inayopanga kila mwaka.

Mathalani kwa miaka mitano mfululizo tangu mwaka 2016/2017, fungu la bajeti ya maendeleo ya wizara hiyo imekuwa ni zaidi ya asilimia 50 ya bajeti yote, jambo linaonyesha kuna mwenendo wa kuridhisha katika kuinua elimu Tanzania.

“Hadi kufikia Machi 30, 2020 Wizara ilikuwa imepokea kiasi cha Sh734.8 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambayo ni sawa na asilimia 85.20 ya bajeti iliyoidhinishwa. Kati ya fedha hizo Sh459.9 bilioni ni fedha za ndani na Sh274.9 ni fedha za nje,” amesema Prof. Ndalichako. 

Bajeti ya wizara hiyo imekuwa ikipanda na kushuka katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Miongoni mwa miradi itakayotekelezwa katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 ni Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ambao unakusudia kuwawezesha wasichana waliopata mimba kurudi shuleni baada ya kujifungua. 

Mradi huo utatekelezwa kwa mkopo wa Sh1.2 trilioni (Dola za Marekani 500 milioni) uliotolewa na Benki ya Dunia mwaka huu, ikiwa ni hatua ya kuwapa fursa wanafunzi wa shule za sekondari nchini kupata mazingira bora ya kusomea. 


Zinazohusiana: 


Akitoa maoni ya kambi rasmi ya upinzani bungeni kwa wizara hiyo, Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Suzan Lyimo (Chadema) amesema ni muhimu Serikali ihakikishe bajeti inayotengwa kila mwaka inaelekezwa katika utatuzi wa changamoto za muda mrefu katika sekta ya elimu ikiwemo upungufu wa vyumba vya madarasa, vifaa vya kujifunzia na uhaba wa walimu shuleni. 

“Elimu bora kila mtoto ndiyo itakayosaidia Tanzania hii kupata maendeleo,” amesema Lyimo. 

Aidha, amesema katika kipindi hiki ambacho shule zimefungwa kutokana na janga la Corona, Serikali haina budi kutumia rasirilimali zake za Tehama kuwawezesha wanafunzi kusoma wakiwa nyumbani ili kuendelea kupata maarifa na ujuzi ili kuwawezesha kutimiza ndoto zao. 

“Ili tuweze kuboresha mazingira yetu ya utoaji elimu, ni lazima kama Taifa tujiulize Wizara yetu elimu imefanya nini mpaka sasa kutatua changamoto ya kukosa masomo hasa kipindi ambacho shule zimefungwa na hatujui zitafunguliwa kutokana na janga la Corona,” amesema Waziri huyo kivuli. 

Hata hivyo, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) leo Aprili 27, 2020 imeanza kurusha vipindi vya elimu katika redio ya TBC Taifa mahususi kwa wanafunzi wa Shule za Sekondari na Msingi ambao wako nyumbani.

Habari hii imeboreshwa kwa kuongezewa Infografia.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW