Wagonjwa wa Corona wafika 480, Tanzania ikiongoza Afrika Mashariki
- Idadi hiyo imeongezeka baada ya Serikali kutangaza wagonjwa wapya 196.
- Sasa Tanzania ndiyo ina wagonjwa wengi zaidi Afrika Mashariki.
- Waliopona mpaka sasa wamefikia 167 na waliofariki dunia ni 16.
Dar es Salaam. Wagonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) wamefikia 480 nchini Tanzania baada ya Serikali kutangaza ongezeko la wagonjwa wapya 196 leo, kiwango ambacho ni juu zaidi Afrika Mashariki.
Kwa idadi hiyo, Tanzania ndiyo inaongoza kuripoti wagonjwa wengi wa Corona katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yenye nchi sita za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Tanzania.
Kenya inashika nafasi ya pili kwa kuwa na wagonjwa 374 hadi jana ikifuatiwa na Rwanda (212), Uganda (79), Burundi (15) na Sudan Kusini imeripoti wagonjwa 34.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema leo jijini Dodoma kuwa wagonjwa hao wapya wamepatikana kati ya Aprili 23 na 28, 2020 ambapo 174 wapo Tanzania bara na 22 visiwani Zanzibar.
Idadi ya wagonjwa hao wapya ndiyo idadi ya juu kabisa kutangazwa kwa siku moja tangu Wizara ya Afya ilipotangaza wagonjwa 53 Aprili 17 mwaka huu.
Amesema wagonjwa waliobaki hali zao zinaendelea vizuri na wanaendelea kupatiwa matibabu katika vituo maalum vya tiba.
“Kati ya wenye maambukizi 297 waliobaki, watu 283 tunafurahi kueleza Taifa wanaendelea vizuri wakisubiri na kufuatiliwa afya zao na tunao wenzetu 14 ambao wako chini ya uangalizi wa madaktari wetu,” amesema Majaliwa.
Mwenendo wa Ugonjwa wa Corona Nchini pic.twitter.com/P6KjND7csz
— Msemaji Mkuu wa Serikali (@TZMsemajiMkuu) April 29, 2020
Hata hivyo, Waziri Mkuu hajasema wagonjwa hao wapya wanatoka katika maeneo gani nchini, licha ya kuwa kwa takwimu za Wizara ya Afya za hadi Aprili 20, jiji la Dar es Salaam lilikuwa ndiyo kitovu cha COVID-19 kwa kuwa na wagonjwa 143.
Aidha, Majaliwa amesema kuwa idadi ya wagonjwa waliopona imeongezeka kutoka 48 hadi kufikia 167 ambapo wagonjwa 83 ni kutoka Tanzania Bara na waliobaki wako Zanzibar.
Idadi ya waliopona nchini ni sawa asilimia 34.7 au mtu mmoja kwa kila watatu walioripotiwa kuwa na ugonjwa huo nchini.
Zinazohusiana
- Mikakati ya Tanzania kukabiliana na virusi vya Corona
- Picha, sauti ya uzushi virusi vya corona zinavyojipenyeza mtandaoni Tanzania
- Unayotakiwa kufahamu kuhusu virusi vya Corona
Wakati idadi ya waliopona ikiongezeka, Waziri Mkuu ametangaza kufariki dunia kwa wagonjwa wengine sita na hivyo kufanya idadi ya waliofariki kwa COVID-19 kufikia 16 (asilimia 3.4) kutoka 10 walioripotiwa awali.
Serikali pia inaendelea na zoezi la kuwafuatilia watu wote waliokutana na wagonjwa siku za hivi karibuni ambao wanatakiwa kukaa karantini kwa siku 14 ili kufanyiwa uchunguzi kama wana maambukizi ya ugonjwa huo.
“Hadi Aprili 28 juzi watu 614 wameruhusiwa (kurudi nyumbani baada kukaa karantini siku 14) katika mikoa ya Zanzibar, Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Kilimanjaro, Kagera, Mwanza, Songwe lakini pia Tunduma, Kigoma na hapa Dodoma,” amesema Majaliwa.
Akimalizi kutoa taarifa ya COVID-19, Waziri Mkuu amewataka Watanzania kuendelea kuzingatia miongozo inayotolewa na wataalamu wa afya na kuepuka taarifa za uzushi za kwenye mitandao ya kijamii.