Majaliwa aagiza mradi wa umeme wa Julius Nyerere ukamilike kwa wakati
- Amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania kusimamia mradi huo ili ukamilike kwa wakati.
- Majaliwa amesema shughuli za ujenzi wa mradi huo haziathiriwi na mvua zinazoendelea.
- Kukamilika kwa mradi huo kutachochea ukuaji katika sekta ya viwanda.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) na amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Dk Tito Mwinuka asimamie mradi huo ili ukamilike kwa wakati.
Mradi huo utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 unajengwa katika mto Rufiji.
Waziri Mkuu aliyekuwa akizungumza leo (Mei 14, 2020) amesema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo mkubwa wa kimkakati nchini Tanzania.
“Nimetembelea eneo la mradi na kujionea shughuli zote zinazoendelea, kazi inayofanyika ni ya uhakika huku kukiwa na matumaini makubwa ya kukamilisha mradi mapema kabla ya muda uliopangwa,” amesema Majaliwa.
Zinazohusiana:
- Majaliwa: Serikali haifanyi biashara utoaji huduma za maji
- Majaliwa azungumzia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha Tanzania
- Majaliwa mgeni rasmi maombi ya kitaifa dhidi ya Corona
Aidha, Waziri Mkuu amemwagiza mkandarasi anayejenga mradi huo aukamilishe kwa wakati kwa sababu imebainika kuwa mvua zinazoendelea kunyesha nchini haziathiri utekelezaji wa ujenzi huo.
Mradi wa umeme wa maporomoko ya maji ya Mto Rufiji unajengwa na kampuni ya Arab Construction kwa pamoja na kampuni ya Elsewedy Electric zote za kutoka nchini Misri.
Umeme utakaozalishwa na mradi huo unatarajiwa kuingizwa kwenye gridi ya Taifa na kuifanya nchi kuwa na umeme wa uhakika pamoja na kuiwezesha Tanzania kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa uchumi wa viwanda na mradi wa reli ya kisasa.
Mbali na kuliwezesha Taifa kuwa na umeme wa uhakika, pia mradi huo umewezesha kupungua kwa changamoto ya ajira baada ya Watanzania wengi wakiwemo wakandarasi kupata ajira za kudumu na za muda mfupi.