Majaliwa: Serikali haifanyi biashara utoaji huduma za maji
- Amesema fedha ambazo wananchi huchangia hutumika kuboresha miundombinu ya maji.
Dar es Salaam. Serikali imesema hailengi kufanya biashara ili kupata faida katika huduma za usambazaji zinazotolewa na mamlaka zake nchini Tanzania bali inawawezesha wananchi kupata huduma hiyo kwa gharama nafuu.
Waziri Mkuu, Kassim aliyekuwa akizungumza leo (Februari 6, 2020) bungeni jijini Dodoma amesema katika ngazi ya mikoa na wilaya kuna kamati za maji zinazoratibu bei ya maji kulingana gharama za uendeshaji na upatikanaji wa huduma hiyo.
“Serikali hailengi kufanya biashara wala kupata faida kutokana na huduma za maji zinazotolewa nchini, ndiyo maana zimeundwa Kamati zinazoratibu huduma hizo kwenye maeneo mbalimbali ili bei ya maji ilingane na hali ya wananchi wake,” amesema Majaliwa.
Majaliwa alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Babati mjini, Pauline Gekul aliyetaka kujua mikakati ya Serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa maji salama kwa gharama nafuu licha ya huduma hiyo kufika vijijini kwa zaidi ya asilimia 70 na mijini kwa asilimia 80.
“Mwaka jana Ewura (Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji) walipandisha bili za maji kote nchini, jambo ambalo limesababisha wananchi wengi kushindwa kulipia bili hizo,” amesema Gekul katika swali lake.
Zinazohusiana
- Majaliwa azungumzia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha Tanzania
- TMA yatoa ushauri, tahadhari ujio mvua za vuli Oktoba
- Kicheko kwa wakulima, TMA akitoa mweleko mvua za msimu
Hata hivyo, Majaliwa amesema wakati mwingine kamati zilizoundwa huhitaji michango midogo midogo kutoka kwa wananchi, siyo ya kuifaidisha serikali bali ni kwa ajili ya kuboresha huduma zinazotolewa zikiwemo za ukarabati wa miundombinu ya maji yakiwemo mabomba.
“Huduma hii hatutarajii kusikia mwananchi analipa gharama kubwa inayomshinda. Tumeagiza Ewura wafanye mapitio ya maeneo haya kuona kwamba gharama haziwi zaidi ya mapato ya mwananchi kwenye eneo lake ili kuondoa usumbufu au dhana ya kwamba tunatoa huduma ya maji kama biashara,” amesema Majaliwa
Aidha, amesema atamuagiza Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa atoe taarifa itakayowafahamisha wananchi juu ya mambo ya kuzingatia wakati wa kutoa michango hiyo kuhakikisha upatikananji wa maji.