Wadau wazungumzia agizo la Makonda kufungua biashara, kula ‘bata’ Dar
- Baadhi ya wamiliki wa biashara wamepanga kufungua biashara zao ifikapo Juni.
- Wadau wengine wamesema waliitumia nafasi hiyo kuboresha maeneo yao.
- Hata hivyo, huenda hali isiwe kama ilivyozoeleka.
Dar es Salaam. Baadhi ya biashara zikiwemo kumbi za starehe, baa na hoteli jijini Dar es Salaam zimepanga kurejesha biashara zao siku za hivi karibuni baada ya kuzifunga shughuli hapo awali ili kuzuia kusambaa zaidi kwa virusi vya ugonjwa wa corona.
Ifahamike kuwa Serikali ya Tanzania haikutangaza kufungwa biashara au shughuli zozote za kiuchumi lakini baadhi wafanyabiashara ya huduma za burudani walifanya uamuzi wa ndani kusitisha kwa muda biashara zao ukiwemo mgahawa maarufu wa Samaki Samaki.
Uongozi wa Samaki Samaki ulisema Mei 13 kuwa upo mbioni kufungua biashara zake tena Juni mosi mwaka huu ikiwa ni takribani miezi miwili tangu ifunge migahawa yake iliyopo sehemu mbalimbali jijni hapa.
Mapema wiki hii Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alitangaza kuruhusu biashara zilizokuwa zimefungwa kurejesha huduma kuanzia Mei 25, 2020 na kuendelea kuchapa kazi huku tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 zikiendelea kuzingatiwa.
“Naomba wenye hoteli, wenye mabaa, wenye makampuni, wenye biashara zote turudi kazini,” Makonda mesema hayo hivi karibuni.
Hata wakati biashara za aina hiyo zikiwa zimefungwa, wapo ambao wameutumia muda huo kufanya mabooresho. Picha| Arrival guides.
Kufunguliwa kwa biashara hizo za ukarimu na burudani kutakuwa ni ahueni kwa wadau mbalimbali wanaozitegemea kupata mkate wao wa kila siku wakiwemo washereheshaji, MaDj na waimbaji.
Allen Henjewele ambaye ni mshereheshaji (host) wa burudani ya kuimba kwa biti almaarufu kama “Karaoke” amesema matangazo ya kufunguliwa huduma hizo likiwemo la Makonda ni kama “sauti iliyoshushwa kutoka Mbinguni”.
“Mimi nilisitisha kazi zangu tangu Machi. Maisha yetu ni toka tule,” Henjewele ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz).
Mshereheshaji huyo ambaye ofisi yake ilifungwa tangu Machi 17 a huku akibainisha kuwa kipindi chote hicho “hali haikuwa hali.”
“Mambo hayatokuwa kama yalivyokuwa mwanzo. Watu wategemee kupunguziwa mishahara na hata kufutwa au kusimamishwa kazi,” amesema Henjewele akieleza kuwa wamiliki na wafanyakazi wa biashara wanatakiwa kujipanga.
Zinazohusiana
- Wasanii wa Kenya, Tanzania wakutana kujadili suluhu ya Corona
- Wanafunzi vyuo vikuu waugeukia muziki kutoka kimaisha
- Corona inavyoathiri kazi za wanamuziki Tanzania
Mshindi wa mashindano ya muziki ya Bongo Star Search (BSS) mwaka 2018, Saraphina Michael ambaye hutumbuiza kwenye hoteli mbalimbali jijini Dar es salaam amesifu hatua iliyochukuliwa akieleza kuwa uchumi wa baadhi ya watu ungekuwa sehemu mbaya.
“Wapo watu wengi wanaotegemea biashara hizo kwa ajili ya kupata kipato na kufungwa kwa biashara hizo kuliwaathiri wengi hasa wahudumu na wadau wa burudani,” amesema.
Kwa wafanya biashara wengine, kufunga biashara kwa ajili ya kuzuia kuenea kwa corona ilikuwa ni fursa kwao kufanya maboresha ya ofisi zao.
Meneja wa ukumbi wa starehe wa Elements, Mohamad Hamad ameiambia Nukta kuwa wapo kwenye matengenezo yanayolenga kuongeza nafasi kwenye ofisi yao ili pia kusaidia kufanisha ushauri wa wataalamu wa afya wa kukaa angalau umbali wa mita moja.
“Ukarabati ukiisha, tutawatangazia wadau wetu kuwa tumefungua” Hamad ameiambia Nukta.