Bunge laingilia kati mgomo wafanyabiashara soko la Kariakoo
- Wabunge waomba sakata hilo lijadiliwe kwa dharura.
- Spika aomba apewe muda kujiridhisha na hali halisi.
- Waziri Mkuu kukutana na Wafanyabiashara leo, aomba waendelee na shughuli zao.
Dar es Salaam. Spika wa Bunge la Tanzania Dk Tulia Ackson amewaomba wabunge kuwa na subira wakati akijiridhisha kuhusiana na mgomo wa wafanyabiashara katika soko la Kariakoo kabla ya kuruhusu bunge kutoa kauli yake kwa Serikali.
Tulia aliyekuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Makete Festo Sanga ambaye aliomba Bunge lisitishwe ili suala la mgomo wa wafanya biashara katika soko la Kariakoo lijadiliwe kwa dharura kutokana na umuhimu wake amesema ni muhimu kuwa na taarifa kamili za sakata hilo kabla Bunge halijatoa maelekezo kwa Serikali.
“Hivi ninavyozungumza hakuna biashara inayoendelea eneo lile kuna mgomo unaoendelea ambao umesababishwa na kamata kamata inayoendelea, sheria ya kikodi ya EFD na usajili wa maghala, nimeona udharura wa jambo hili Wabunge tujadili na Serikali itoe kauli ili shughuli ziendele,” amesema Sanga.
Mbunge wa Makete Festo Sanga alipokuwa akitoa hoja kuhusiana na Mgomo wa wafanyabiashara unaoendelea soko la Kariakoo.Picha l Guru
Spika Tulia alimkaribisha Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dk Ashatu Kijaji ili atoe kauli ya Serikali ambapo licha ya kukiri kuwa kuna changamoto ya mgomo alisema vikao vinaendelea kati ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na maafisa kutoka taasisi mbalimbali za Serikali.
“Mkuu wa Mkoa pamoja na maafisa kutoka Wizara ya Fedha na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wapo kwenye kikao na viongozi wa wafanyabiashara wa Kariakoo, na yapo maeneo ndani ya Kariakoo ambapo shughuli zinaendelea,” amesema Dk Kijaji.
Hata hivyo kauli ya Kijaji ilipingwa na Mbunge wa Viti Maalumu Hawa Mwaifunga na baadae Mbunge wa Makete Festo Sanga kuwa hakuna kikao kinachoendelea na hakuna makubaliano yaliyofikiwa hivyo ni muhimu Bunge likajadili suala hilo.
Pamoja na Spika Tulia kumpa nafasi nyingine Waziri Kijaji kufafanua suala hilo aliendelea kusisitiza kuwa wapo baadhi ya wafanyabiashara waliofungua maduka yao, ndipo akawaomba wabunge apate kwanza taarifa rasmi kabla ya kuamua chochote kuhusiana na suala hilo.
“Watu wangu wanafuatilia kama Kariakoo biashara zinaendelea au hapana lakini jambo la dhahiri ni kwamba kuna changamoto, waziri amesema kuwa kuna kikao kuashiria kwamba ipo changamoto na pia amesema kuhusu mgogoro,” amesema Spika Tulia.
Kwa mujibu wa Festo Sanga chanzo cha mgogoro huo ni makato makubwa ya Kodi kutoka kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kulazimishwa kutumia mashine za elektroniki za kutolea risiti (EFD), kuanzishwa kwa kodi mpya ya ghala pamoja na ushuru mkubwa wa bidhaa bandarini.
Soma zaidi:
Waziri Mkuu atoa kauli
Wakati hayo yakijiri Bungeni Jijini Dodoma kupitia ukurasa rasmi wa mtandao wa Twitter, Ofisi ya Waziri Mkuu ilichapisha taarifa ikiuarifu umma kuwa kiongozi huyo atakutana na kamati ya wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo, pamoja na Mawaziri wa sekta husika na Mamlaka ya Mapato Tanzania ( TRA) leo.
“Mkutano huo unatarajiwa kufanyika Saa 8 Mchana kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu Magogoni – Ikulu Jumatano tarehe 17 Mei 2023 kwa uratibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa wakati Serikali ikifanya jitihada za kupata ufumbuzi wa changamoto zilizopo wafanyabiashara hao wafungue shughuli zao ili kuwapa nafasi wahitaji kupata huduma za bidhaa mbalimbali kutoka kwenye soko hilo kubwa linalohudumia Tanzania na Afrika Mashariki.
Mapema hii leo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla alifika katika soko hilo na kuzungumza na wafanyabiashara ambapo aliwaahidi kuwakutanisha na Waziri Mkuu ili kutatua changamoto hizo.
“Nasimamisha oparesheni zote, alafu nafungua njia ya mazungumzo kwenda kuonana na kiongozi wa shughuli zote za Serikali msaidizi namba tatu wa Rais ni jambo kubwa ambaye yeye atawaita mawaziri wote, atamwita Waziri wa Fedha, atamwita Waziri wa Viwanda..,” amesema Makalla.
TAARIFA MUHIMU
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajia kukutana na kamati ya wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo, Mawaziri wa sekta husika na Mamlaka ya Mapato Tanzania ( TRA).
1/3— Ofisi ya Waziri Mkuu (@TZWaziriMkuu) May 15, 2023
Latest
