Historia: Bei ya petroli yashuka hadi Sh1,520 kwa lita Dar
- Kushuka kwa bei hizo inatokana na kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji.
- Bei hizo mpya za petroli jijini Dar es Salaam ni za chini zaidi kuwahi kurekodiwa ndani ya kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Dar es Salaam. Unaweza kusema ni historia baada ya bei ya rejareja ya mafuta ya petroli na dizeli Tanzania kushuka kwa kasi na kufikia bei ya chini kuwahi kurekodiwa ndani ya miaka 10 iliyopita.
Mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na maji (Ewura) imetangaza kuwa kuanzia Juni 3, 2020 bei ya mafuta yaliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam itashuka kwa Sh348 kwa lita kwa petroli na Sh300 kwa lita upande wa dizeli.
Kutokana na mabadiliko hayo ya bei, wakazi wa Dar es Salaam sasa watakuwa wakinunua lita moja ya petroli kwa Sh1,520 kwa lita kutoka Sh1,868 ya bei ya rejareja iliyokuwa ikitumika Mei mwaka huu.
Wamiliki wa vyombo vya moto vinavyotumia dizeli wao watanunua dizeli kwa Sh1,546 kwa lita kutoka Sh1,846 ya bei ya rejareja ya Mei.
Watumiaji wa mafuta ya taa wao wataendelea kununua kwa bei ya Sh1,568 iliyokuwa ikitumika mwezi uliopita.
Kwa mantinki hiyo kwa sasa petroli inauzwa bei ya chini zaidi kuliko mafuta ya taa jambo ambalo ni adimu kutokea.
Bei hizo mpya za petroli jijini Dar es Salaam ni za chini zaidi kuwahi kurekodiwa ndani ya kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Mara ya mwisho ya bei kama hiyo ilitangazwa na Ewura Desemba 2009 ambapo bei kikomo ya petroli Dar es Salaam ilikuwa ni Sh1,585 kwa lita wakati elekezi ikiwa ni Sh1,475 kwa lita.
“Mabadiliko ya bei katika soko la ndani yanatokana na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji (BPS premium),” Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Godfrey Chibulunje ameeleza katika taarifa iliyotolewa Jumanne, Juni 2, 2020.
Soma zaidi:
Hata hivyo, wakazi wa mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, wao wataendelea kutumia bei zilizokuwepo kwa kuwa hakukuwepo shehena ya mafuta iliyoingilia Bandari ya Tanga. Hii itawahusu pia wanunuzi wa jumla wa nishati hiyo.
Kwa wakazi wa mikoa ya kusini ya Mtwara, Lindi na Ruvuma wao wataendelea kununua petroli kwa bei za rejareja zilizotangazwa Mei 6 kwa kuwa hakukuwa na shehena ya petroli iliyopokelewa Bandari ya Mtwara.
“Hata hivyo, bei za mafuta ya dizeli kwa jumla na rejareja mwezi Juni zimepungua kwa Sh425 kwa lita na Sh423 kwa lita mtawalia,” ameeleza Chibulunje katika taarifa hiyo.
Hata hivyo, watumiaji wa mafuta ya taa katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma watanunua nishati hiyo kutokana ukokotoaji wa bei za mafuta yaliyoingilia Bandari ya Dar es Salaam.
Latest