Maumivu: Serikali kuongeza ushuru wa forodha vifaa vya ujenzi 2020-21
- Baadhi ya vifaa vitakvyoongezewa ushuru ni mabati, nondo na marumaru.
- Lengo la hatua hii ni kulinda na kukuza viwanda vya ndani vinavyozalisha bidhaa hizo pamoja na kuongeza ajira.
- Vifaa hivyo vimekuwa vikitumiwa zaidi katika shughuli za ujenzi wa majengo.
Dar es Salaam. Huenda Watanzania wakapata msukumo zaidi wa kutumia vifaa vya ujenzi vinavyotengenezwa na viwanda vya ndani baada ya Serikali kupendekeza kuongeza ushuru wa forodha kwa baadhi ya vifaa hivyo zikiwemo marumaru zinazotoka nje ya nchi.
Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango akiwasilisha bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka 2020/21 amesema mapendekezo hayo yatasaidia kulinda na kukuza viwanda vya ndani vinavyozalisha vifaa hivyo.
Dk Mpango amependekeza kuongeza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa za marumaru zinazoingizwa kutoka nje.
Marumaru zimekuwa zikitumika kupendezesha sakafu na kuta za nyumba kwa muonekano tofauti.
Pia Serikali itaendelea kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 25 au Dola za Marekani 250 (Sh578,700) badala ya kiwango cha asilimia 25 au dola za kimarekani 200 (Sh462,997) kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kwenye bidhaa za chuma kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwenye nondo na kwa mwaka mmoja.
Amesema viwanda 16 vya nondo kati ya 25 vilivyoko nchini Tanzania vina uwezo wa kuzalisha nondo tani milioni 1.083 kwa mwaka ikilinganishwa na mahitaji ya tani 295,000 kwa mwaka.
Ongezeko la ushuru huo kwa bidhaa zinazotokea nje ya nchi, utasaidia kukuza soko la viwanda vya ndani. Picha| Brodge of hope.
Dk Mpango amesema Serikali iendelee kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 10 au Dola za Marekani 250 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric ton) kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwenye bidhaa za mabati badala ya ushuru wa asilimia 10 pekee.
Amesema hatua hiyo ni kulinda viwanda vya ndani kutokana na udanganyifu wa thamani halisi ya mabati yanapoingizwa kutoka nje (underinvoicing and under valuation), na kulinda ajira na mapato ya Serikali.
“Lengo la hatua hii ni kulinda na kukuza viwanda vya ndani vinavyozalisha marumaru pamoja na kuongeza ajira,” amesema waziri huyo.
Huenda ongezeko hilo la ushuru likawa maumivu kwa Watanzania wanaoagiza vifaa hivyo nchi za nje kwa sababu gharama za ujenzi zinaweza kuongezeka.
Lakini itakuwa fursa kwa viwanda vya ndani kuongeza uzalishaji na kuuza zaidi kwa Watanzania ambao wana uhitaji mkubwa wa kuwa na majengo ya kuishi na biashara.
Mbali na vifaa vya ujenzi, zipo bidhaa za kilimo ambazo pia zimependekezwa kuongezewa ushuru.
Kati ya bidhaa hizo ni chai ambapo Dk Mpango amependekeza ongezeko la ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa za aina hiyo zinazoingizwa kutoka nje.
Dk mpango amesema lengo ni kuhamasisha kilimo cha chai hapa nchini pamoja na kuongeza ajira katika sekta ya kilimo.
Zinazohusiana
- Tanzania kuondoa kodi, ushuru wa vifaa tiba vya Corona
- Ahueni: Serikali ikipendekeza ongezeko la kiwango cha mapato ya waajiriwa
- Serikali kushusha tozo maendeleo ya ufundi (SDL)
Pia , kwa upande wa zao la kakao, Dk Mpango amependekeza ongezeko la asilimia 10 la ushuru wa forodha kutoka asilimia sifuri ya hapo awali ili kuchochea na kuhamasisha kilimo cha zao hilo Tanzania.
Nchini Tanzania, kakao hulimwa katika Wilaya za Kyela na Rungwe mkoa wa Mbeya ambapo huzalisha zaidi ya asilimia 80 ya kakao yote nchini.
Maeneo mengine ni Ifakara-Morogoro na Maramba-Tanga na mchakato wa kulima zao katika mkoa wa Kigoma unaendelea.
Inakadiriwa kuwa Tanzania huzalisha tani 7,000 za kakao kila mwaka.
Pia, Serikali imependekeza kuendelea kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa za mboga mboga ikiwa na lengo la kulinda wakulima wa ndani ili kuendeleza kilimo cha mbogamboga na maua nchini.
Latest