Mkaa, mbogamboga vyachangia kupandisha mfumuko wa bei Tanzania
- Mfumuko huo wa bei umepanda hadi asilimia 3.3 mwaka ulioishia Julai 2020 kutoka asilimia 3.2 mwaka ulioishia Juni mwaka huu.
Dar es Salaam. Mfumuko wa bei kwa mwaka ulioshia Julai 2020 umeongezeka kidogo kufikia asilimia 3.3 kutoka asilimia 3.2 iliyorekodiwa mwaka ulioishia Juni mwaka huu ukichangiwa zaidi na kuongezeka kwa bidhaa za chakula na zisizo za chakula kama mkaa, unga wa mahindi, gesi ya kupikia na mbogamboga.
Mfumuko wa bei hupima kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.
Taarifa ya mfumuko wa bei iliyotolewa Agosti 10 2020 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza kuwa baadhi ya bidhaa za chakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Julai 2020 ni unga wa mahindi uliopanda kwa asilimia 7.9, mtama (asilimia 4.8), matunda (asilimia 4) na mbogamboga kwa 9.6.
“Kwa upande mwingine baadhi ya bidhaa zisizo kuwa za vyakula zilizoongezeka bei kwa mwezi Julai 2020 ikilinganishwa na Julai 2019 ni pamoja na mavazi yaliyopanda kwa asilimia 2.8, gesi ya kupikia kwa asilimia 5.9, samani (asilimia 2.7), gharama za ujenzi na ukarabati nyumba (asilimia 6.2) na mkaa kwa asilimia 11.6,” imesema sehemu ya taarifa hiyo ya NBS.
Zinazohusiana:
- Mfuko wa bei washuka kwa mara ya tatu mfululizo Tanzania
- Ijue mikoa kumi inayoongoza kwa mbuzi wengi Tanzania
Mfumuko huo wa bei umeongezeka kidogo baada ya kudumu katika kiwango cha asilimia 3.2 kwa miezi miwili mfululizo ya miaka inayoishia Mei na Juni mwaka huu.
Hata hivyo, kasi ya mfumuko wa bei za vyakula na vinywaji baridi kwa Julai 2020 umeendelea kubaki katika asilimia 3.8 kama ilivyokuwa Juni 2020.
Kiwango cha mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Julai 2020 nchini Tanzania ni cha chini ikilinganishwa na viwango vya nchi jirani za Afrika Mashariki za Kenya na Uganda.
Mfumuko wa bei kwa Julai mwaka huu nchini Kenya ulipungua na kufikia asilimia 4.36 kutoka asilimia 4.59 mwaka ulioishia Juni.
Huko Uganda, mfumuko wa bei kwa kipindi hicho uliongezeka hadi asilimia 4.7 kutoka asilimia 4.1 mwaka ulioishia Juni 2020, kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Mtakwimu Mkuu, Dk Albina Chuwa.
Mbogamboga ni moja ya bidhaa za chakula zinazotumika na kaya nyingi Tanzania. Bidhaa hizo ziliongezeka bei Julai 2020 ikilinganishwa na iivyokuwa Julai mwaka jana. Picha|Emanuel Feruzi/K15.
Latest



