Maoni mchanganyiko zawadi ya maua kwa wapendanao Tanzania
- Wakati wengine wakifikiria ni kitendo cha upendo wengine wanasema ni kupoteza fedha.
- Hata hivyo, zawadi hiyo inatakiwa kutolewa kwa wakati sahihi na kwa mtu anayeelewa maana.
- Baadhi wanashauri unapompa mtu zawadi ya maua uambatanishe na kitu kingine kinacho dumu muda mrefu.
Dar es Salaam. “Nilijiuliza sana nimpatie zawadi gani kwenye kumbukizi ya siku yake ya kuzaliwa. Ilikuwa ni mara ya kwanza kuadhimisha siku hiyo akiwa mpenzi wangu na kwa muda wote sikua nafahamu anapenda nini zaidi.
“Niliamua kutafuta mtu na aliniambia maua, chokoleti na zawadi moja ya kudumu vingefaa,” ni maneno ya Thomson Nathaniel mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam wakati anafikiria zawadi ya kumpatia mpenzi wake.
Baada ya kupatiwa maua na zawadi zingine, Gladness ambaye ni mpenzi wa Nathaniel alikuwa na furaha isiyo kifani.
“Alienda kununua vase (chombo cha kuwekea maua) na aliyaweka mule. Huwezi amini licha ya kuwa yamekauka, maua hayo anayo hadi leo,” amesema Nathaniel ambaye alifanya hivyo mwezi Julai mwaka 2019.
Tangu hapo, Nathaniel amesema amekuwa akimpelekea mpenzi wake maua lakini amekuwa akiyaweka kwenye vase nyingine na kuyatupa yanapokauka lakini hajawahi kuyatupa yale aliyopewa mwanzo.
Suala la kutumia maua ya asili (natural flowers) kama zawadi ambayo watu wanapeana kwa sababu mbalimbali, limekuwa likileta mijadala ambayo inaibua hisia tofauti kama ni sahihi au siyo sahihi maua kutumika kama zawadi.
Nukta (www.nukta.co.tz) ilifanikiwa kupata mitazamo hiyo ya watu kuhusu hisia juu ya maua na jinsi ambavyo inaweza kuwa sehemu ya kuimarisha mahusiano ya watu kwenye jamii.
Maua ni ishara ya upendo na amani lakini yana hisia tofauti kwa kila mtu anayepewa. Picha|Urban Design Flowers.
Je, kuna hisia gani zilizojificha nyuma ya kupokea au kumpa mtu maua?
Gladness Malima ambaye amekaa na maua aliyopewa na Natahaniel kwa zaidi ya mwaka mmoja amesema baada ya kupewa ua lile na mpenzi wake alijifikiria mambo mengi yakiwemo muda aliouchukua na kumfikiria kiasi cha kumnunulia maua.
“Ni kweli yamekauka lakini kila nikiwaza kuwa alinipa yeye yanabaki kuwa maua maalumu kwangu. Sina hata mpango wa kuyatupa,” amesema Malima.
Naye mtaalam wa picha, Evon Evance amesema kumpatia mtu ua ni ishara inayoonyesha kuwa mtu huyo ana umuhimu endapo litatolewa kwa muda muafaka.
“Mtu akikupatia mdoli ana maana yake, akimpa mtu kazi za sanaa ina maana anafahamu mtu kuwa anapenda vitu vya sanaa na akimpa ua, ni ishara ya uzuri kwani maua ni mazuri. Ni vigumu kuelezea lakini ndivyo ilivyo,” amesema Evans.
Wakati Evans akifikiria kuwa maua ni zawadi nzuri ya kumpa mtu, wengine wanafikiri maua ni kiashiria cha mtu kuonyesha jinsi anavyompenda na kumthamini mtu aliye karibu naye.
Mkulima wa vitunguu na mazao ya bustani Enalisa Nguma amesema baba yake alikuwa akimpatia maua mara kwa mara.
“Kila mara nilipokuwa nikiadhimisha sikukuu za kuzaliwa, baba alikuwa akinitumia furushi kubwa la mawaridi mekundu. Ilinipatia hisia ya aina yake,” amesema mkulima wa mazao ya bustani jijini Dar es Salaam, Enalisa Nguma.
Wakati hao wakifurahia maua katika muktadha ya mahusiano mema ya urafiki na undugu, wapo watu wengine ambao mimea hiyo wanaihusisha zaidi na mapambo ya nyumba au sherehe tu.
Mkazi wa jijini Mwanza, Suzana Mbeshi ameiambia Nukta kuwa kumpatia maua pekee kama zawadi haina maana kwake.
“Sasa maua mimi ukinipa nayafanya nini? Siwezi kula wala chochote. Bora hata uniletee pipi nitabadilisha ladha mdomoni,” amesema Mbeshi ambaye hajawahi kupokea zawadi ya maua.
Mbeshi anaamini kununua maua ni kupoteza fedha kwa sababu siyo bidhaa ya kudumu.
Soma zaidi:
- Kigoma kinara wa usajili mashamba Tanzania bara
- Fursa uzalishaji wa maua Tanzania
- Haya ndiyo masoko ya maua Tanzania
Tofauti na Mbeshi, Mkazi wa Morogoro Tekla Simon amesema yeye anapenda maua lakini yasije “makavu”, badala yake, atakayempelekea maua, aambatanishe na kitu kingine kama chokoleti, chupa ya mvinyo, saa na hata kitu kingine cha kushikika.
“Sina tatizo na kupewa maua lakini nikiyapokea na kitu kingine kama chokoleti au kinywaji nitafurahi zaidi,” amesema Simon.
Naye Mkazi wa Dar es Salaam Badru Rajabu amesema kwa upande wake utamaduni wa kupeana maua ni wa kimagharibi, kuliko kupeleka maua ni vyema akanunua kilo ya nyama na kupeleka nyumbani.
“Maua ni kwa watu wa uchumi wa kati. Angalia hata sehemu yanapouzwa, Masaki na Oysterbay. Huwezi kwenda Mbagala ukakuta maua yanauzwa,” amesema Rajabu aliyesema utamaduni huo ni mgeni kwa Watanzania.
Amesema yapo mambo mengi ya kuangazia wakati mtu akitafuta zawadi ya kumpatia rafiki au ndugu na siyo maua pekee kwa sababu hayadumu na watu wengi hawaoni kama ni kitu cha maana kwao.
Usikose muendelezo wa makala haya ambayo tutaangazia rangi za maua na maana yake katika matumizi ya shughuli mbalimbali.