Mazoezi yatakayokusaidia kuimarisha utendaji wa moyo wako

October 10, 2020 5:33 am · Joshua
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kujishughulisha na kuepuka kukaa sehemu moja muda mrefu.
  • Kufanya mazoezi ya aerobiki ikiwemo kuendesha baiskeli, kutembea, kukimbia na kuogelea.
  • Kutokufanya mazoezi kunasababisha matatizo ya moyo. 

Unafanya mazoezi ya kuimarisha usukumaji wa damu walau dakika 150 (saa 2:30) kwa wiki? Kama sivyo hauko peke yako. 

Tafiti zinaeleza kuwa ni mtu mzima mmoja tu kati ya watano ndiye hufanya mazoezi ya kutosha ili kuwa na afya njema. 

Ufanya mazoezi huongeza ufanisi wa unavyofikiri, kuhisi hata kupata usingizi bora zaidi. Na iwapo kazi zako ni za kukaa muda mrefu basi kupunguza muda wa kukaa ni hatua nzuri ya awali ya kuanza nayo. 

Lakini mazoezi ni zaidi ya kuimarisha misuli na utendaji wa mwili. Mazoezi husaidia kuimarisha afya ya moyo ambao ni injini ya mwili wako. Fanya haya kwa mtu mzima ili uimarishe afya ya moyo:

Fanya mazoezi ya aerobiki 

Pata walau dakika 150 za mazoezi ya aerobiki kwa wiki nzima ya kiwango cha kati, au unaweza kupata saa 75 za mazoezi ya aerobiki mazito kidogo kwa wiki nzima. 

Mazoezi ya aerobiki ni mazoezi ya uvumilivu na mara zote mazoezi haya huimarisha moyo na mapafu, kwa jina jingine huitwa mazoezi ya moyo.

Mazoezi haya ni muhimu katika uchaguzi wako wa mazoezi na yana faida nyingi  kiafya ikiwemo kuchochea usukumaji wa damu na utendaji kazi wa misuli na moyo. Huchangia katika uchomaji wa mafuta yanayozidi mwilini.

Mazoezi ya aerobiki ni pamoja na kuendesha baiskeli, kutembea, kukimbia, kuogelea, kucheza mpira, kucheza mchezo wa kuteleza kwenye barafu, mchezo wa kupigana ngumi.

Mazoezi siyo tu yanakusaidia kuimarisha afya ya mwili bali yanawezesha moyo ambao ni injini ya mwili kufanya kazi kwa weledi. Picha|Mtandao. 

Fanya mazoezi ya kujenga misuli

Mazoezi ya aerobiki yaende sambamba na mazoezi ya kiwango cha kati hadi acha juu kidogo cha mazoezi ya kujenga misuli. Unaweza kutumia uzito uliopimwa au njia nyinginezo za kutengeza mzio. 

Mazoezi haya huweza kufanywa kwa kuupa upinzani mwili mfano, kupiga “push up”, kunyanyua vitu vizito, kuchuchumaa na kuinuka, kuvuta kitu kizito. Kwa kifupi mazoezi haya hufanya misuli ya mwili ifanye kazi vizuri.

Mazoezi haya yanaweza kufanyika walau mara mbili kwa wiki. Uimara wa misuli hupunguza matokeo ya ukaaji mbovu na kurundikana kwa mkazo ndani ya misuli na hivyo moyo wako kufanya kazi vizuri. 


Soma zaidi:


Punguza muda unaotumia ukiwa umekaa

Ongeza zaidi muda wa kujishughulisha. Haya ni matokeo ya mtindo wa maisha wa kisasa ambapo watu wengi hujikuta wakitumia muda mwingi zaidi wakiwa wamekaa kuliko kawaida. Jitahidi kunyanyuka kila baada ya saa moja au mawili baada ya kukaa muda mrefu.

Kisha ongeza kiwango cha mazoezi kulingana na wewe unavyoona mwili wako unazoea. Sanjari na hayo unaweza fanya haya kwa ajili ya mtoto.

Watoto wa miaka 3-5 wanapaswa kuruhusiwa na kuwa na muda wa kutosha kuweza kufanya michezo na shughuli mbalimbali ambazo hufanya miili yao ijishughulishe. Wasibanwe sana na wapewe muda wa uangalizi ili miili na mifupa yao iimarike katika ukuaji wao.

Wahimize watoto wako kufanya mazoezi ili kujenga afya zao. Picha| Mtandao. 

Watoto wa umri miaka 6-17 wanapaswa kupata walau dakika 60 kwa siku za mazoezi ya kati au mazito kwa ajili ya kuimarisha afya ya miili yao. Na hii ni sababu mojawapo ya uwepo wa michezo mashuleni kwani hulenga katika kuimarisha afya ya mwili sambamba na afya ya akili ya watoto hawa.

Tafiti za kisayansi zihusianisha kutokufanya mazoezi, kukaa sana na kutojishughulisha na magonjwa ya moyo, kisukari, saratani ya utumbo mpana pamoja na mapafu na kifo cha mapema. 

Jitahidi kuushughulisha mwili kwa ajili ya kuwa na afya bora hasa ya moyo wako.

Nipo!

Dk Joshua Lameck Sultan ambaye kitaaluma ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) na Mkurugenzi wa Indigo Afya. Hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.

Enable Notifications OK No thanks