Kiti cha ofisini: Rafiki au adui wa afya yako?

October 24, 2020 8:07 am · Joshua
Share
Tweet
Copy Link

                         


  • Siyo kila kiti kimeundwa kukidhi mahitaji ya ukaaji wa watu tofauti.
  • Ukikalia kiti kisicho sahihi unajiletea matatizo ya misuli na mgongo.
  • Kalia kiti kinachoendana na umbile lako na aina ya kazi unayofanya. 

Ninaingia katika ofisi moja kwa ajili ya masuala fulani ya kiutawala kisha nakutana na rafiki yangu wa siku nyingi ambae pia ndiye muhusika katika ofisi hii. 

Kwa muda tunasahau hata kuwa kilichonipeleka pale siyo stori za kiuswahiba bali masuala nyeti kabisa ya kiofisi.

Hata hivyo, katika kuongea huku ananiambia “Daktari hivi viti vyetu vitakua na shida kubwa sana maana wengi wanalalamika vinawaumiza mgongo.”

Ikanibidi nitazame kiti anachokalia ambacho kinafanana na viti vyote wanavyotumia wafanyakazi wa ofisini. Baadhi ya viti hivi havina  ubora wa kibaiomekaniki ambao humuwezesha mtu kufanya kazi yake bila maumivu na kuwa hata kama angezingatia ukaaji mzuri bado kingemletea shida tu.

Basi acha tuangazie kwa undani kama kiti chako kinaweza kuwa rafiki mwema ama adui wa afya yako.

Siyo kila kiti kimeundwa kukidhi mahitaji ya ukaaji wa watu tofauti. Aina ya kiti kilichoundwa kukidhi mahitaji hayo ni kiti cha kiegonomiki. Kiti bora ni kile ambacho hukidhi mpangilio wa dawati la kazi, ukubwa wa mwili wa mfanyakazi (yaani vipimo vya mwili) na aina za kazi anazofanya katika dawati lake la kazi. 

Vitu hivi vyote havina budi kuzingatiwa wakati unachagua kiti cha kutumia. 

Mfanyakazi anapaswa kukaa katika kiti ambacho hufanya miguu yake ikae kwa kunyooka kabisa na bila kujikunja sana ama kunin’gin’gia na bila kutengeneza mzio ama mkazo kwenye eneo la mapaja. Picha|Mtandao.

Kwanini kuna umuhimu wa kutumia kiti sahihi? 

Huenda unaona hakuna umuhimu huo lakini majibu yake yatakushangaza.Majeraha yanayotokana na ukaaji wa muda mrefu ni mojawapo ya matatizo ya kiafya yaambatanayo na kazi za ofisini. Kazi hizi za ukaaji muda mrefu hazitumii nguvu nyingi ya misuli. 

Lakini haimanishi zinawatenga watu na majeraha yatokanayo na kazi za watu ambao hufanya kazi zinazohusisha utumiaji mkubwa wa misuli au kazi za shuruba. Zingatia haya unapochagua kiti cha ofisini: 

Mosi, kiti cha aina moja kinaweza kabisa kisiwe sahihi kwa watu wote kwa ujumla. Hii hutokana na utofauti wa kimaumbile na vipimo vya miili, jambo ambalo ni la kiasili kabisa.

Pili, kuwa na taarifa sahihi kuhusu urefu wa mtumiaji wa kiti. Kitako cha kukalia hupaswa kuwa ¼ ya urefu wa mwili mzima.

Tatu, siyo kila kiti hufaa watu wa kazi zote. Mfano kiti cha mtu wa benki huwa tofauti na yule atakayefanya kazi za kiwandani au yule ambaye kazi zake hutumia kompyuta zaidi. Na mwisho ni kuzingatia gharama za matengenezo ya kiti husika ili kimfae kila anayekitumia. 


Soma zaidi:


Sifa ya kiti bora

Sasa tuangalie ni vitu gani ambavyo ni haiba za kiti bora cha kutumia hasa kwa kazi za ofisini ambazo huusisha kukaa muda mrefu, walau kwa kudodosa.

Moja ni uwezo wa kiti hiki kuweza kuongezwa kimo cha kiti, yaani urefu wake. Pili ni uwezo wa kurekebisha urefu wa eneo la kukalia yaani eneo la kitako. 

Kimsingi mfanyakazi anapaswa kukaa katika kiti ambacho hufanya miguu yake ikae kwa kunyooka kabisa na bila kujikunja sana ama kunin’ginia na bila kutengeneza mzio ama mkazo kwenye eneo la mapaja. 

Eneo la kupumzishwa mgongo ama kwa kimombo “backrest”. Eneo hili linapswa kuwa na uwezo wa kusogezwa mbele au nyuma au kuongezwa urefu. 

Pia linapaswa kuwa na uwezo wa kuhimili na kusaidia mgongo kukaa katika umbo lake la asili bila kujikunja na hasa eneo lile la mgongo wa chini.

Mwisho ni eneo la kukaa kuwa pana pamoja na eneo la kupumzishia mikono. Eneo la kukalia linapaswa kutosha na kutobana mwili. Hii itasaidia kuondosha kurundikana na kuweka mkazo ambao unaweza kuathiri misuli ya mwili. 

Nakunja jamvi langu kwa maneno haya, sio kila kiti lazima kiwe na matairi. Kuna wakati kazi yako ingefaa zaidi kwenye kiti kilicho tulia kuliko kiti kilicho na matairi ambacho humaanisha hakiwezi kutulia sehemu moja. 

Zingatia haya ili kuweza kufurahia kazi yako kwa ufanisi mkubwa. Kama ilivyo ada, nakukumbusha jukumu la afya ni la kwako mwenyewe na kwamba kinga ni bora kuliko tiba. 

Nipo!! 

Dk Joshua Lameck Sultan ambaye kitaaluma ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) na Mkurugenzi wa Indigo Afya. Hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.

Enable Notifications OK No thanks