Uzingatie nini unaponunua nguo mtandaoni?

December 16, 2020 11:35 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na saizi na vipimo vyako kabla ya kuagiza.
  • Pia unaweza kuhakiki sera ya kurudisha bidhaa pamoja na usafirishaji.
  • Kuepukana na kuagiza bidhaa feki, soma maoni ya wadau waliowahi kununua bidhaa hiyo.

Dar es Salaam. Baada ya kufurahishwa na mwanamitindo aliyeivaa nguo hiyo, wengi huagiza nguo hizo wakiwa na maono ya kupendeza kama mwanamitindo anavyoonekana.

Kwa baadhi wanaobahatika, nguo zao huwakaa vizuri lakini kwa baadhi, huenda nguo hizo hazijawahi kuliona jua, mwezi wala nyota tangu wazinunue kwani zimeishia kubaki makabatini huku zingine zikitupwa ama kugawiwa ndugu au marafiki wanaoendana nazo.

Je, walikosea wapi? Jifunze kutokufanya makosa hayo wakati ukifanya manunuzi ya nguo mtandaoni: 

Kuwa makini na saizi ya nguo unayoagiza

Kutokana na wapi nguo yako imetengenezwa, huenda ikatofautiana na saizi yako halisi mfano, nguo zinazotengenezwa nchini China zina saizi tofauti na zile zinazotengenezwa Uturuki na hata Marekani. 

Kuepukana na manunuzi ya nguo itakayokubana ama kutokukutosha, hakikisha unatoa vipimo vyako sahihi kulingana na vipimo vya nguo kwa nchi husika.

Kabla ya kuchagua nguo yako, hakikisha uneangalia vipimo vyako kama vinaendana na nguo hiyo| Elite Readers.

Kagua sera ya kurudisha bidhaa

Kila duka la mtandaoni lina sera ya kurudisha bidhaa. Yapo mengine ambayo hayaruhusu mtu kurudisha nguo pale anapoipokea hata kama isipomtosha ama asiporidhika nayo.

Ili kuepukana na usumbufu pamaja na uharibifu wa fedha zako, ni vizuri kuelewa sera hizo ili endapo nguo haijakaa sawa mwilini mwako, uwe na uwezo wa kuirudisha na kupata ile inayokufaa zaidi.

Pata ushauri kwa watu wanaonunua nguo mtandaoni

Watu wengi hupuuzia hili lakini ni kitu kinachoweza kukusaidia kufanya maamuzi. Mfano unataka kuagiza kiatu na bei yake siyo haba, unaweza kusoma maoni ya watu wengine walionunua ili ujue kama wana malalamiko au wanampa mwenye duka sifa kwa kuwa na bidhaa nzuri.

Pia baadhi ya maduka ya mtandaoni huandika idadi ya mauzo ya bidhaa hiyo hivyo unaweza kuepuka kuingizwa chaka kwa kununua nguo isiyoendana na fedha yako.


Soma zaidi:


Zingatia nyota za muuzaji

Kwa kimombo hizi zinaitwa ‘rates’ na huonyeshwa kwa alama ya nyota ambazo huwa na rangi ya njano.

Mara nyingi kwa wauzaji wa mtandaoni wanaoaminika, wanakuwa na nyota tatu, nne hadi tano ikiwa ni ishara kuwa huduma wanayoitoa inaridhisha wateja wao.

Kabla ya kuagiza nguo yako, angalia idadi ya watu walioagiza nguo na nyota zake kama zinaridhisha.

Enable Notifications OK No thanks