Wabadili taka za plastiki kuwa nguo

May 11, 2019 6:52 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Shughuli hiyo inafanyika katika karakana yao ambapo taka za plastiki ikiwemo mifuko inakatwa vipande vidogo vidogo na kugeuzwa kuwa nyuzi ambazo zinafumwa kuwa kama kitambaa. Picha| UNEP.


  • Wakazi wa eneo la Kougougou katika mji wa Ouagadougou nchini humo  wamebuni mbinu mpya ya kuzibadili taka za plastiki kuwa mavazi, mikoba na pochi.
  • Taka hizo zinakatwa vipande vidogo vidogo na kugeuzwa kuwa nyuzi ambazo zinafumwa kuwa kama kitambaa.
  • Mpaka sasa wamefanikiwa kurejeleza tani 2,400 za taka na kujipataia mapato yanayofikia Sh12.9 milioni.

Dar es Salaam. Kama taka kwako hazina thamani, basi wenzako wamekuwa wakizitumia kama fursa ya kutengeneza bidhaa mbalimbali ili kujipatia kipato na kuwa sehemu ya kutunza mazingira. 

Wakazi wa eneo la Kougougou katika mji wa Ouagadougou nchini Burkina Faso  wamebuni mbinu mpya ya kuzibadili taka za plastiki kuwa mavazi, mikoba na pochi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UN) iliyotolewa Mei 9, 2019, wakazi  hao  ambao wengi wao ni vijana na wanawake kupitia kikundi chao cha NEERE wameamua kugeuza lundo la taka za plastiki zilizosambaa mjini humo kuwa rasilimali muhimu.

Shughuli hiyo inafanyika katika karakana yao ambapo taka za plastiki ikiwemo mifuko inakatwa vipande vidogo vidogo na kugeuzwa kuwa nyuzi ambazo zinafumwa kuwa kama kitambaa.

Kitambaa hicho hutumika kutengeneza mavazi, pochi na mikoba ambapo inasaidia kumaliza changamoto ya Burkina Faso ya ukosefu wa udhibiti mzuri wa taka.

“Takribani wanawake 70 wamefundishwa jinsi ya kukusanya, kuchambua, kusafisha na kufuma taka hizo kuwa kitambaa,” inaeleza taarifa hiyo.


Soma zaidi:


Mradi huo ambao ni chachu ya utunzaji wa mazingira unaungwa mkono na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Umoja wa Ulaya (EU).

“Plastiki ni fedha iliyo kwenye mpito kwa sababu iwapo unafahamu jinsi ya kuitumia na kuibadilisha, taka ni fedha. Watu walizoea kutupa plastiki, sasa sisi tunaibadili kuwa mtindo,” anaeleza Mratibu wa NEERE, Damien Lankoande katika taarifa hiyo.

Mwakilishi wa UNEP kanda ya Afrika, Juliette Koudenoukpo amesema kuwa taka za plastiki ni changamoto kubwa nchini Burkina Faso kwa sababu zinaziba mitaro ya maji, zinaua mifugo.

Yassia Savadogo na Ouedraogo Odile wakionyesha baadhi ya nguo na mikoba inayotengenezwa kwenye karakana yao. Picha|UN News.

Akinukuliwa na UN, Koudenoukpo amesema wanawake ambao wako kwenye kikundi hicho siyo tu wanatunza mazingira bali pia wanapata kipato na kuleta manufaa kwa jamii zao.

Mpaka sasa kikundi hicho kilichoanza kazi hiyo mwaka 2007 kimesharejeleza tani 2,400 za plastiki na mapato ya mwaka yameongezeka kutoka dola za Marekani 1,120 (Sh2.57 milioni)  mwaka 2007 hadi dola 5,620 (Sh12.9 milioni) mwaka huu.

Enable Notifications OK No thanks