Ahueni: Sony yaingiza sokoni kiyoyozi kinachovaliwa mwilini
- Kinaitwa Reon Pocket na kina uwezo wa kumpatia mtumiaji wake baridi au joto.
- Kinaambatana na nguo yake maalumu ambayo mtumiaji anatakiwa kuivaa wakati wa kutumia.
- Kinaweza kuwa msaada kwa wakazi wanaoishi kwenye miji yenye joto kama Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Hakika huwa ni usumbufu kwa baadhi ya watu wanaoishi katika maeneo yenye joto kama jiji la Dar es Salaam pale ambapo kunywa maji mengi ili kudhibiti joto hilo.
Na wakati mwingine kulazimika kuvaa nguo nyepesi ili kupunguza makali ya joto hilo ambalo nyakati za mchana huwa kiwango cha juu likiambatana na jua.
“Mimi binafsi kipindi cha joto hunigharimu fedha nyingi sana. Mara nyingi huwa ninalazimika kuchukua bajaji ili nipunge upepo,” amesema Jessica Kimoso mkazi wa jijini humo.
Katika kipindi hicho, Jessica amesema wakati wa joto ndiyo kipindi anachotumia maji mengi zaidi kwa mwaka kwani huoga mara nyingi kuliko kawaida.
Hata hivyo, huenda wadau wa teknolojia wamesikia kilio cha Jessica na wengine ambao wanapitia adha hiyo na kubuni kiyoyozi kidogo kiitwacho “Reon Pocket” ambacho kinaweza kupoza mwili pale mwenye nacho anapokitumia.
Siyo joto tu, kama mtumiaji atakuwa kwenye eneo la baridi, kifaa hicho pia kinaweza kumpatia joto.
Baada ya kuiweka mashine hiyo kwenye mfuko wa nguo na kuivaa, mtumiaji anaweza kuiunganisha na simu ya mkononi ambayo itafanya kazi kama rimoti yake. Picha| Google Images.
Kinafanyaje kazi?
Reon Pocket ni kifaa kilichobuniwa na kampuni ya Sony ya Japan kwa ajili ya kumpooza mtu na kumpatia joto kwenye kipindi cha baridi.
Kifaa hicho kinakuja na nguo yake maalumu ambayo ni T-shirt ambayo imeshonewa mfuko kinachovaliwa mwilini ili kiweze kufanya kazi.
Baada ya kuiweka mashine hiyo kwenye mfuko wa nguo na kuivaa, mtumiaji anaweza kuiunganisha na simu ya mkononi ambayo itafanya kazi kama rimoti yake.
Hapo anaweza kuongeza na kupunguza ubaridi au joto kadiri ya matakwa yake.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la The Verge, kifaa hicho kinaweza kupunguza joto la mwili kwa nyuzi joto 13 kwa maana kama kiwango cha joto cha Dar es Salaam siku hiyo ni nyuzi joto 28, kifaa hicho kitaipunguza kufikia nyuzi joto 15.
Kwa kufanya hivyo, itamuondolea mtumiaji wake adha ya joto mwilini mwake japo bado uwalakini upo juu ya namna gani kifaa hicho upepo wake utafika usoni.
Zinazohusiana
- Usiyoyajua kuhusu mtandao wa 5G
- Safari ya mwisho ya Google Plus
- Zingatia haya unaponunua taa za nyumbani
Reon Pocket inachajiwa na ikijaa, inaweza kufanya kazi ndani ya saa mbili hadi tatu kulingana na mahitaji ya mtumiaji.
Mdau wa teknolojia Sam Byford nchini Marekani mbaye amefanya uchambuzi wa kifaa hicho amesema utendaji kazi wa kifaa hicho ni sawa na kuchukua kipande cha barafu na kukiweka kwenye ngozi iliyopigwa na joto.
Zaidi, mdau huyo amesema hata mtu akiwa amekivalia kifaa hicho, hakionekani na hivyo kumpatia mtumiaji wake amani.
Reon Pocket ina uzito wa takriban gramu 80 huku ikigharimu Sh371,520 kama utakinunua katika mtandao wa Amazon (Japan).
Endapo utahitaji na t-shirt yake, utalazimika kuinunua tofauti kwa Sh46,440 huku kifaa hicho kikiwa na uwezo wa kufanya kazi na simu za iPhone (iOs) na Android.
Hata hivyo, kifaa hicho kwa sasa kinapatikana Japan peke yake huku kukiwa hamna matangazo ya kukiuza kimataifa.
Huenda baada ya janga la Corona kuisha na kuruhusiwa kwa safari za kimataifa, kifaa hicho kinaweza kuanza kusambazwa katika masoko duniani.