Nusu ya wanafamilia walivyokatwa miguu kwa “ugonjwa wa ajabu”- 2
-
Watoto hawa licha ya kuwa na miguu yao lakini wenza wao wamewakimbia wakihofia kuandamwa na madhira yanayoitesa familia hiyo.
-
Matumaini ya kuokoa ndoa na uhai wao yapo kwa wataalam wa afya waweze kuwapatia chanjo au tiba ya uhakika kukabiliana na tatizo hilo.
Mwanza. Watoto hawa licha ya miguu yao kukatwa, wenza wao wamewakimbia wakihofia kuandamwa na madhira yanayoitesa familia hiyo.
Matumaini ya kuokoa ndoa na uhai wao yapo kwa wataalam wa afya waweze kuwapatia chanjo au tiba ya uhakika kukabiliana na tatizo hilo.
Ndoa za watoto wa Amina Kalazi zimegeuka shubiri baada ya waume zao kuwatelekeza na kukimbia kusikojulikana. Wapo waliobadilisha namba na kususia watoto waliozaa na wake zao.
Hofu yao ni kuwa na mwendelezo wa kizazi kinachougua ugonjwa wa ajabu unaofuata kizazi hadi kizazi.
Mpaka sasa watoto wanne wote wa Amina licha ya kukatwa miguu na kugeuka tegemezi wote na watoto wao wametelekezwa na waume zao na kukata mawasiliano.
Ni mme pekee wa Rahma ndiye ambaye amekubaliana na matokeo ya mipango ya Mwenyezi Mungu na anasema magonjwa pia ni matokeo hapaswi kuyakimbia.
Rahma anaeleza kwa undani kwenye video jinsi ugonjwa ulivyoanza katika familia yake
Ugonjwa ulivyofanya familia kuishi kwenye lindi la umaskini
Umasikini ndio kikwazo kikubwa kinachoitesa familia hiyo ya Amina. Kulala njaa na kuishi kwenye pagale imekuwa kawaida kwao.
Amina anaeleza hata matatizo yanayowakumba ya ugonjwa huo yanapotokea makanisa, misikiti pamoja na watu wengine ndio hubeba msalaba wa kuwasaidia.
“Mfano gharama ya kukatwa miguu pamoja na gharama zingine za kukaa hospital kusafishwa kidonda hufikia zaidi ya Sh700, 000 kiasi ambacho kutokana na hali yetu hatuwezi kumudu hivyo watu wengine hujitokeza kubeba jukumu hilo kutusaidia, ” anasema Amina.
Anasema wakati mwingine huwa anaomba msamaha hospitali kulingana na gharama hizo kuwa kubwa.
“Huku Misenyi hakuna kanisa na msikiti usionijua na hata misikiti mingine ya mbali pia huwa naenda, nililazimu kuweka aibu pembeni ili nipate fedha ya kuwatibia watoto wangu, “
Hali ya kukata tamaa na maamzi ya kjia yalianza kingia kichwani mwake
“Nilikosa tumaini la kuishi, sikutaka kuendelea kuishi lakini nilipokuja kuwaangalia watoto na hawana msaada wowote niliamua kufunga mkanda kpambana,”
Kutokana na miguu yao kukatwa hulazimika kutembea kwa kutumia magoti huku wakishindwa kufanya shughuli za kujiingizia kipato. Picha|Mariam John.
Hofu imani potofu zatawala
Msitapha Ibrahim ni mmoja wa majirani wa familia ya Amina Kilazi, lakini pia ni mme wa Rahma anasema wengi huamini ugonjwa huo ni wa kurogwa kutokana na mfululizo wa matukio yaliyotokea hapo.
Changamoto hiyo imesababisha baadhi ya majirani kuamini kuwa huenda ni laana ya jambo fulani inawatafuna huku wengine wakiwa tahadhari sana kwa kuwataka kufanya tambiko la kimila.
Anasema yeye anamtazamo tofauti kwani ugonjwa huo ni sawa na magonjwa mengine yanayowapata binadamu ingawa huo unawaweza kuwa hatari kwakuwa unasambaa haraka.
Anasema kabla mke wake Rahma hajakatwa miguu aliwahi kuumwa na miguu mmoja ambapo baada ya kufikishwa hospitali na kupatiwa dawa alipata nafuu, changamoto imekuja mwaka jana akiwa na mimba ambapo alipata maumivu yliyosababisha miguu yake kukatwa.
Hatahivyo, Ibrahim anaomba wataalam wafanye utafiti kwa kuwa ugonjwa huo si kwamba unampata kila mtu isipokuwa unafuata damu.
Hata watoto ambao ni wazima wanahofu ndugu na jamaa.Happiness Mathias anomba afanyiwe uchunguzi kuona kama anaviashiria vya ugonjwa huo.
“Majirani na marafiki wameanza kutuogopa wakiamini tutawaambukiza, inauma sana naomba serikali atusaidie, ” anasema.
Soma zaidi:
Msamaria mwema ajitokeza
Wakati wakihaha alijitokeza msamaria ambaye atafuta wadau wengine pia kuiokoa familia hiyo na maumivu.
Dk Flora ambaye ni mkurugenzi wa taasisi ya Nitetee Foundation anasema baada ya kupata taarifa za mama huyo alimwomba huyo mama kuja jijini Mwanza kwa ajili ya kupata suluhu ya tatizo hilo.
“Nilipopata taarifa zao na kuelezwa kiundani kuhusiana na tatizo hilo niliamua kufanya taratibu za kuwaita wote ili kuona kama wanaweza pata huduma za kimatibabu ikiwemo chanjo ili kunusuru kizazi kilichobaki, ” alisema.
“Cha ajabu ugonjwa huo hauambukizi isipokuwa unafuata damu,”
Ukiachilia mbali msaada wa kimatibabu ambao anawasaidia watu hao wapate, pia Dk Flora pia kupitia wasamaria wenzie wamesaidia kuchangia ujenzi wa nyumba ya vyumba vitatu kwa ajili ya kuishi.
Anasema awali familia hiyo ilikuwa inaishi kwenye pagale hivyo ikamlazimu kutafuta fedha za kuwajengea nyumba ya kuishi.
Baadhi ya wanafamilia ambao miguu ya imekatwa kutokana na tatizo ugonjwa wa ajabu ambao hawaufahamu mpaka sasa. Picha| Mariam John.
Ni nini maombi yao?
Ombi kubwa la familia hiyo kwa sasa ni kwa serikali kupata chanjo ya kudumu ili kuokoa kizazi kilichopo kwa kuwa kwa sasa hawana amani baada ya wajukuu nao kuanza kupoteza miguu.
Amina anasema zamani alijua kizazi chake pekee ndicho chenye tatizo kumbe hadi wajukuu zake.
Madaktari bado hawana uhakika mkubwa juu ya chanzo halisi cha ugonjwa huo ulioikumba familia ya Amina.
Joachim Mazima, daktari aliyewafanyia upasuaji wa kuwakata miguu watoto saba wa amina, anasema ugonjwa huo kitaalam huitwa “Gangrene” ambayo huchangiwa na kuziba kwa mishipa ya damu.
Tatizo hilo, anasema, hupelekea uzalishaji duni wa tishu za ngozi na kusababisha eneo lilioathirika kukauka na kuoza.
“Viungo vinapooza na kusababisha mgonjwa kuwa na maumivu makali ambayo kikawaida hakuna njia yoyote ya kuyatibu zaidi ya kukata miguu hiyo,” anasema Dk Mazima ambaye amefanya kazi katika hospitali mbalimbali za umma na binafsi.
Ugonjwa huo kwa mujibu wa Dk Mazima mara nyingi huwapata wagonjwa wa Kisukari na huanza taratibu kushambulia mishipa na hubainika ukiwa umefika kwenye hatua za mwisho ambapo mgonjwa huhisi maumivu makali.
“Sio ugonjwa wa kurogwa ni kama magonjwa mengine kinachohitajika ni kufanya uchunguzi wa kina kwa watu waliobaki ili kuwaepusha na tatizo hilo ambalo linasababisha kuwaacha walemavu na kuwa tegemezi, ” anasema.
TANGAZO: #NuktaFakti ndiyo kiboko ya habari za uzushi na uongo
Akitolea mfano kwa mgonjwa aliyemfanyia operesheni ambaye ni Rahma anasema alilazimika kumkata mguu chini ya goti kwa kuwa baada ya kukatwa hospitali ya awali ugonjwa uliendelea kusambaa hali iliyosababisha kukatwa miguu chini ya goti.
Maelezo ya Dk Mazima hayajapishana na mmoja wa mtaalam wa afya kutoka hospital ya Bugando ambaye hakupenda jina lake litajwe kuwa ugonjwa huo anaufananisha na Gangrene japo ana wasiwasi kuwa huenda kinachowapata wanafamilia hao kikawa zaidi ya ugonjwa huo.
Daktari huyo anasema ugonjwa wa Gangrene wenyewe haushambulii miguu yote kwa wakati mmoja isipokuwa huanza na mguu mmoja kwanza kisha mguu mwingine hufuata.
“Ila ugonjwa wa familia hii wenyewe unachanganya kwa kuwa ukishaanza tu ndani ya siku chache umekuwa umesambaa sehemu za vidole vyote vya miguu na kuoza kwa haraka, ” anasema.
Alitaja baadhi ya dalili za ugonjwa wa gangrene kuwa ni mgonjwa kuhisi maumivu makali, ngozi kuwa na rangi tofauti, nyekundu, nyeusi, kufifia kwa ngozi hususan eneo lililoathirika.
Ishara nyingine ni miguu na vidole kuziba, kuvimba katika miisho ya chini ya miguu. Kisababishi Kikuu cha ugonjwa huo wa Gangrene anasema ni kisukari, kuvaa viatu visivyokutosha, madawa ya kulevya, sigara, sumu ya kemikali.
Ugonjwa huo pia unadaiwa kuchangia asilimia 80 ya vifo vya wagonjwa wa aina hiyo.
Hata hivyo, familia hiyo inadai kuwa hawajahi kukutwa na ugonjwa kisukari jambo linaloacha maswali zaidi.
Hata hivyo, daktari wa Bugando yeye anashauri watafiti wa magonjwa ya binadamu kufanya utafiti kwa kuchukua sampuli ya damu, na magonjwa mengine yanayohusiana na ugonjwa wa miguu ili kubaini chanzo cha tatizo hilo la familia ya Amina.
Habari hii imeboreshwa leo Machi 9, 2021 kwa kuongezewa video.
Latest
