Coming to America: Filamu maalum kwa watu wasiotaka kuvunja viapo

March 12, 2021 1:35 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni filamu inayomhusu mfalme anayepaswa kwenda kinyume na mila na desturi zilizowekwa na watangulizi wake.
  • Inakusogeza na kukukumbusha juu ya ahadi ya ndoa ambayo uliiweka katika enzi za mahusiano yako.


Dar es Salaam. “Mimi Rodgers George, ninakupokea wewe binti sayuni kuwa mke wangu wa ndoa ninaahidi kukulinda, kukupenda siku zote za maisha yangu hadi kifo kitakapotutenganisha”. 

Ahadi hiyo huenda inawakumbusha wanandoa wengi siku yao ya ndoa. Ni kweli ahadi hiyo hutunzwa? 

Mara nyingi wakati unaweka ahadi hiyo kwa umpendaye iwe ni kanisani au msikitini na hata mbele ya jamaa, huwa mawazo yapo kati yenu wawili. Lakini kadri siku zinavyoenda, hambaki wawili tu, kazi zitaingia, ndugu watakuja, majukumu pia yataanza kuongezeka na taratibu, kwa baadhi ahadi hizo hubaki pasipo kuwa na maana tena.

Ni kama ilivyo kwa Mwana Mfalme Akeem (Eddie Murphy), wa Zamunda katika filamu ya #ComingtoAmerica ambaye kuilinda familia na mke wake ilikua katika kiapo cha ndoa yake. Lakini baada ya kuwa mfalme, maslahi yake yanahamia katika kuhakikisha usalama wa watu anaowaongoza na kulinda mila na desturi za wana Zamunda.

Mfalme Akeem ambaye ni baba wa binti watatu, anapata kigugumizi kumwandika mtoto wake wa kike, binti mfalme Meeka kama mrithi wake pale maisha yake yatakapoisha.Shinikizo kubwa likitoka kwa baba yake, Mfalme Jaffe Joffer kuhusu mila za wana Zamunda ambapo anayetakiwa kurithi mikoba ya ufalme ni mwanaume.

Kuwa mwanaume, haimanishi kuwa Lavelle atakubaliwa kirahisi na jamii ya wana wa Zamunda. Picha| Screen Rant.

Kama bado hujaelewa, ufalme wa Zamunda una utamaduni wake ambao wanawake wanachukua nafasi ya pili katika jamii ikiwa ni kutokuruhusiwa kufanya biashara na kuwa watiifu kwa waume zao, na wanaume kwa ujumla.

Mfalme Akeem kukosa mtoto wa kiume inampa mawazo lakini huzuni zake hazidumu kwa muda mrefu kwani anapokea habari za kuwa ana mtoto wa kiume ambaye alimpata kabla hajaoa na ni zaidi ya miaka 20 imepita. 

Kwa Mfalme Akeem, hili ni jibu kuu, ni mwisho wa masimango, na ni heshima ya kuwa anaweza kupata mtoto wa kiume hivyo anafunga safari ya kwenda Marekani kumsaka kijana wake wa kiume.

Lichaya kuwa hajawahi kumuona baba yake tangu azaliwe, kijana Lavelle ambaye anahangaika kutafuta kazi, haoni sababu ya kukataa kwenda kwa baba yake ambako atakuwa mwana mfalme yeye na mama yake wanafunga safari kwenda kwa Mfalme Akeem kukutana na familia mpya ya wana wa Zamunda.


Soma zaidi:


Ni dhahiri kuwa siyo rahisi kwa Lavelle kukubaliwa na wana wa falme ya Zamunda eti kwa sababu tu yeye ni mwana mfalme wakati binti mfalme Meeka amejifua maisha yake yote kama mrithi wa taji la ufalme pale maisha ya baba yake yatakapofikia tamati. 

Kupatikana kwa penzi la kweli katika ardhi ya ugenini, wasichana kupingana na miko, familia kuungana na wafalme kufahamu makosa yao, ni kati ya vitu ambavyo filamu hii imekusudia kukupatia.

Je Lavelle ataweza kukalia kiti cha ufalme kisa tu yeye ni mwanaume?

Je, Meeka atakubali kushuka chini ya Lavelle ambaye ni mgeni katika ardhi ya Zamunda na kumruhusu atawale wana wa Zamunda?

Jibu maswali yote kwa Gharama ya hadi Sh10,000 katika kumbi za kuangalizia filamu ikiwemo Dar Free Market, Aura Mall na Mlimani City

Enable Notifications OK No thanks