Ahueni: Wapata teknolojia mpya ya kukamua mafuta ya mawese Kigoma

March 11, 2021 6:47 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Mfanyakazi kutoka SIDO akiendesha mtambo huo wa kukamua mafuta ya mawese, mtambo ambao umetengenezwa na SIDO kwa ufadhili wa ITC. Picha| ITC Video.


  • Ni mashine yenye uwezo wa kukamua mafuta ya mawese kwa kasi na kuokoa muda wa wafanyabiashara.
  • Mashine hiyo imetengenzwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kwa ufadhili wa kituo chake cha biashara (ITC).
  • Imekabidhiwa kwa wanawake wajasiriamali mkoani Kigoma. 

Dar es Salaam. Ni furaha na nderemo katika Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, magharibi mwa Tanzania baada ya kikundi cha wanawake wajasiriamali cha kata ya Kinazi kukabidhiwa mashine ya kisasa ya kukamua mawese.

Sasa wana uhakika wa kuongeza uzalishaji wa mafuta hayo yanayotumika kupikia chakula na shughuli za viwandani ili kujipatia kipato kwa ajili ya kuendeleza familia zao. 

Umoja wa Mataifa kupitia kituo chake cha biashara (ITC) umejibu ombi la wanawake wajasiriamali hao wa Kigoma kwa kuwapatia mashine ya kisasa ya kukamua mawese na hivyo kupunguza muda wa kukamua mafuta hayo kutoka saa nane hadi mbili bali.

Mashine hiyo ambayo imetengenzwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kwa ufadhili wa ITC utawasaidia wanawake hao kupata mafuta yenye ubora zaidi na hivyo kuongeza wigo wa soko la bidhaa hiyo muhimu nchini. 

Mwenyekiti wa kikundi hicho chenye wanachama 28 kilichoanzishwa Julai mwaka 2019, Benta Sauja amesema miaka ya nyuma walikuwa wanahangaika sana kwa sababu walikuwa wanatumia muda mwingi kukamua mafuta kwa kutumia mashine duni.

Mjasiriamali huyo wa zao la chikichiki ambayo ndiyo hutoa mafuta ya mawese amekiambia kituo cha habari za Umoja wa Mataifa (UNIC) kuwa walikuwa wanatumia siku nzima kukamua pipa moja la mbegu na wanapata lita 25 tu za mafuta. 

“Sasa hivi mashine hii (mpya) inakamua vizuri tunapata mafuta ya kutosha, na bado hatuhangaiki unapeleka mzigo wako unatua na kazi ni kusimamia tu ni namna gani viende na  hakuna maumivu yoyote yale, hata mtoto hawezi kulia tena kuwa unamtuma nipelekee huu mzigo,” amesema Sauja. 

Kwa mujibu wa kikundi  hicho, mashine hiyo mpya inakamua vizuri na makapi ya chikichi yanakuwa meupe lakini yale ya mashine ya kienyeji mtu unazunguka hadi unachoka na unaamua kumwaga hata kabla chikichi hazijalainika vizuri. 

Teknolojia hiyo inawezesha ukamuaji wa mafuta katika muda wa kati ya dakika 12 hadi 15 pipa moja linakuwa limeshakamuliwa na mchakato wa kuchemsha mafuta unaanza. 

Katibu wa kikundi hicho Elisia Nzogela akizungumzia matarajio yao amesema wanategemea mafanikio kwa sababu walizoea mashine za kienyeji lakini walipojaribu mashine mpya waliona mafanikio ni mazuri. 


Soma zaidi:


“Nichukue fursa hii kuwashukuru wafadhili ambao ni ITC kupitia Kigoma Joint Programme, na SIDO pia niwapongeze sana kwa kuwa nimeona mashine hizi zimeandikwa SIDO Kigoma, kwa hiyo niwapongeze kwa hilo. Lakini lingine ni utunzaji kwa kuwa mashine hizi ni nzuri na ni mpya na zinafanya kazi vizuri na zote mmeziwasha hapa tumeshuhudia,” Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mwamvua Mrindoko amesema wakati wa makabidhiano ya mashine hizo.

Programu ya pamoja kwa Mkoa wa Kigoma ilianza mwaka 2017 na mashirika ya Umoja wa Mataifa ya chakula na kilimo (FAO), mpango wa chakula (WFP), kituo cha biashara cha kimataifa (ITC) na maendeleo ya mitaji (UNCDF).

Programu hiyo inalenga kuwasaidia watu hasa wanawake na vijana kukabiliana na changamoto mbalimbali kwa kuwezeshwa kiteknolojia na mitaji kuendesha shughuli zao za kiuchumi. 

Licha ya changamoto za uzalishaji wa chikichi hilo ikiwemo upatikanaji wa pembejeo, mbegu bora na soko, uzalishaji wa mawese umekuwa ukionyesha matumaini baada ya Serikali na wadau wa zao hilo kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji.

Hali ya hewa ya Tanzania inaruhusu michikichi kustawi kwa wingi hasa katika mikoa ya Kigoma, Mbeya (Wilaya ya Kyela) na Pwani ambayo ina hali ya kitropiki hasa joto la wastani na mvua za kutosha. 

Enable Notifications OK No thanks