Itakuwaje ikiwepo sayari ya wanaume peke yao?
- Ni filamu inayomhusu mwanadada ambaye anajikuta katika sayari iliyo na wanaume tu baada ya kupata ajali.
- Akiwa katika sayari hiyo, Aede anajikuta matatani baada ya wenyeji kutokufurahia ujio wake.
- Hata hivyo Hewitt anajitokeza na kuasi jamii yake kumtetea binti huyo.
Dar es Salaam. Kumekuwepo na utani miongoni mwa jamii ikiwa baadhi ya watu wakitaniana kuwa kila jinsia ipatiwe sayari yake. Yaani wanaume wapewe sayari yao na wanawake wapewe sayari yao pia.
Hata hivyo, huenda wengi walio na ndoto ama fikra hizo wanakatishwa tamaa na uhalisia kwani kanuni za uumbaji tayari zimeamua kuwa jinsia zote, zitaishi pamoja na kutegemeana, huenda ni kitu kisichowezekana.
Lakini, itakuwaje pale jambo hili likitokea? Hilo limetokea kwenye filamu ya “Chaos Walking” ambapo sayari ina mwanamke mmoja tu ambaye anaishi katikati ya wanaume.
Yote inaanza na ajali. Ajali ambayo inamfanya Viola Eade ajikute mwanamke pekee katika sayari ya Prentisstown ambayo ina wanaume tu na wote wanaongozwa na Mayor Prentiss!
Anapoamua kuwa msaada wa Aede, anakuwa amesaliti jamii yake. Picha| Variety.
Mfanano wa sayari hiyo na sayari ya dunia, haimlazimishi kuvalia nguo maalumu, wala kuona haja ya kubeba silaha ili ajilinde lakini ukweli wa kwamba sayari hiyo imejaa wanaume tu, kama ilivyo kwako, na kwake bado unampatia wasiwasi.
Kati ya wanaume wote wa sayari hiyo, jicho la Aede linamdondokea Todd Hewitt ambaye ni mwanaume mdogo kuliko wote katika sayari hiyo.
Hewitt ambaye ni yatima aliyelelewa na baba zake Cillian pamoja na Ben, amezaliwa akiwa na nguvu za ajabu ambazo kutokana na umri wake, bado hajazifahamu.
Hadihi zilizopo katika sayari hiyo zinamwaminisha Todd Hewitt ambaye ni mdogo miongoni mwa wanaume wote kuwa kiumbe kinachojulikana kama Spackle, kiliwaua wanawake wote katika sayari hiyo na kuwaacha wanaume waliosalia na sifa ambayo huenda wanawake wangeifurahia sana.
Soma zaidi:
- Nukta Africa yazindua maabara ya mafunzo ya aina yake Tanzania
- Mikakati itakayowainua wanawake kiuchumi Tanzania
- Corona: Facebook yabana zaidi wapotoshaji mtandaoni
Kila mwanaume katika sayari hiyo, mawazo yake yanawekwa hadharani. Yani kila anapowaza, ni kama moshi fulani hivi unaonekana kichwani na mawazo yake yanasikika.
Kwa Hewitt, inamuwia vigumu kwani hajui kile mwanadada Aede anafikiria. Anajiuliza kama anafurahishwa naye, kama anafikiria, kama anataka kumuua. Hajui na hajazoea kutokuona mawazo ya yeyote.
Hata hivyo, ujio wa Aede haumfurahishi Mayor Prentiss ambaye anaanzisha safari yake ya kumuua.
Pale Hewitt anapogundua kuwa usalama wa Aede upo matatani, anaapa kuwa mlinzi wake. Na hapo, anakuwa amesaliti jamii ya wanaume wenzake.
Kuwa na Aede, Hewitt anaanza kufahamu yale yaliyojificha katika historia ya sayari yake na huenda ikawa ni chanzo cha kuzigundua nguvu zake..
Mimi na wewe hatuzijui lakini kupitia skrini za kuangalizia filamu za Century Cinemax, unaweza kupata jibu la maswali unayojiuliza kwa gharama hadi Sh10,000 tu kuitazama filamu ya “Chaos Walking”.
Leo tumeishia hapa, sijui wiki ijayo tutakuwa na nini?