Bodaboda, wajasiriamali waomboleza kifo cha Rais Magufuli

March 18, 2021 7:15 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Wengasema atakumbukwa kwa kupigania maslahi ya wanyonge hata kwa kuweka afya yake matatani.
  • Baadhi wanahoji kama atapatikana kiongozi wa kuziba pengo lake.

Dar es Salaam. Sura za huzuni miongoni mwa Watanzania ni jambo ambalo unaweza kuliona pale unapokuwa katika mitaa ya Mkoa wa Dar es Salaam. 

Ni asubuhi lakini wengi wameshikilia simu zao wakihama kutoka mtandao mmoja kwenda mwingine kufahamu kuhusu taarifa za mshtuko za kufariki dunia Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Wengine wameshikilia redio zao wakisikiliza hotuba ambayo ilitolewa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan jana usiku ( Machi17, 2021) na ukiwatazama utaona taya zao zikiiacha midomoyao wazi na mikono yao ikiwa kiunoni. 

Dereva wa bodaboda mtaa wa Victoria mkoani hapa, Musa Omary ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa uongozi wa Dk Magufuli  ulirahisisha kazi zake kwa kiasi kikubwa kuanzia ujenzi wa barabara za mitaa na barabara kuu na miundombinu mingine kwa ujumla.

“Katupa fursa nyingi. Mwanzo tulikuwa tunakatazwa hata bodaboda tusiingie mjini, ila yeye alituruhusu tuingie mjini lakini sharti ukamilike. Helmet mbili, viatu, leseni na pikipiki iwe na vibali. Unaingia bila shaka yoyote,” amesema Omary akielezea kifo cha Rais Magufuli.

Zaidi, mdau huyo wa usafirishaji amesema chini ya Magufuli hata tozo za vyombo vya moto zinazotozwa na Mamlaka ya Mapato Tanznaia (TRA) zimepungua kutoka Sh40,000 kwa miaka mitatu hadi Sh70,000 kwa miaka mitano.

“Kafanya vitu vingi ambavyo vimetusaidia, kwa hiyo tutamkumbuka kwa mambo mengi,” amesema Omary huku uso wake ukiwa na huzuni.

“Tumepoteza shujaa na sidhani kama atapatikana kiongozi mwingine wa kupambana na rushwa kama alivyofanya Magufuli,” amesema Ndisulo. Picha| Bloomberg.

Kwa wengine, Kifo  cha Magufuli kimerudisha picha za viongozi mbalimbali walioondoka wakati watu wao bado wakiwategemea wakiwemo viongozi wa dini.

Mbunifu wa katuni Taurus Mangi, amesema anafananisha hali iliyopo miongoni mwa Watanzania kama safari ya wana wa Israel waliompoteza Musa karibu wanafika kanani kwani walipata shida kujiuliza itakuwaje Musa aliyewatoa Misri hayupo tena.

Mangi amesema, “Musa ndiye aliyeanzisha safari ya kuelekea kanani kwa mkono wa Mungu. Tumuombe Mungu atupe Joshua anaetufaa. Kama Taifa tuendelee kumtegemea Mungu.”

Mangi amesema ombi lake ni Mungu kumpatia Mama Samia Suluhu uongozi na ujasiri kama aliokuwa nao Magufuli ambapo alikuwa kiongozi aliyekuwa na maono makubwa kwa Tanzania.


Soma zaidi


Majonzi na simanzi juu ya kuondoka kwa Rais Magufuli hayajawagusa Watanzania waliopo nchini tu bali hata waliopo nchi za nje.

Kwa Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Okayama kilichopo Japan, Whitney Ndusilo amesema ni vigumu kufikiri kuwa kuna kiongozi ambaye atawapambania Watanzania wanyonge kama alivyofanya Rais Magufuli.

Kwa binti huyo Mtanzania, Magufuli alifanya kazi kubwa na alijitoa vilivyo kutetea maslahi ya Watanzania huku wakati mwingine akiiweka rehani hata afya yake.

“Tumepoteza shujaa na sidhani kama atapatikana kiongozi mwingine wa kupambana na rushwa kama alivyofanya Magufuli,” amesema Ndisulo.

Watanzania wengine watamkumbuka kwa namna Magufuli alivyokuwa mnyenyekevu kwa watu aliowaongoza, matani aliyokuwa akiyafanya katika hotuba zake na hamasa yake kwa uzalendo.

Mkazi wa Tabata Kinyerezi aliyefahamika kwa jina moja, Sada amesema kwake Magufuli atabaki kuwa kiongozi wa wanyonge kwani hakuna Rais aliyewahi kuwa karibu na Watanzania kama alivyokuwa Magufuli. 

Aliwasikiliza, aliwasaidia hata kwa pesa zake.

“Niliona hotuba hiyo usiku. Nilibaki na butwaa sikupata usingizi hadi saa nane, nitamkumbuka kwa ucheshi wake kwani alikuwa mnyenyekevu jamani, kula mahindi yaliyopikwa na Watanzania, kulipa bili za watu hospitalini, ni mengi siwezi kuyamaliza,” amesema Sada.

Rais Magufuli amefariki jana Saa 12 jioni katika hospitali ya Mzena Mkoani Dar es Salaam wakati akipatiwa matibabu. 

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema kifo hicho kimetokana na tatizo la moyo la mfumo wa umeme ambalo alikuwa nalo kwa zaidi ya miaka 10.

Enable Notifications OK No thanks