Ipi itakufaa: Mchuano wa saa janja OnePlus, Apple, Samsung unavyoweka watumiaji njiapanda
- Wakati zote zikiwa na uwezo wa kufanya kazi kama rimoti, saa ya OnePlus inakaa muda mrefu na chaji kuliko nyingine.
- Kama wewe ni mpenzi wa saa ndogo, saa ya Apple itakufaa na kama saa ya wastani, Samsung itakufaa.
- Utahitaji wastani wa kati ya Sh360,000 hadi Sh930,000 kumiliki saa hizo.
Dar es Salaam. Katika pililkapilika zako za kila siku, unaweza kuwa shahidi wa umaarufu wa saa janja miongoni mwa mikono ya watu wengi wanaopenda umaridadi wa vifaa vya elekroniki vya kidijitali.
Tofauti ya saa hizo na zilizozoeleka ni mfumo wa kidijitali ambao unaambatana nazo ikiwa ni pamoja na uwezo wake wa kufanya kazi kama kisaidizi cha simu janja kwa kusomea arafa au meseji, kujibu simu zinazopigwa na hata kusikiliza muziki bila haja ya kuwa karibu na simu yako.
Kuna saa janja nyingi mtaani lakini je, ipi ni ipi? Uchambuzi huu umeanika utofauti uliopo kati ya saa janja kutoka Samsung Galaxy toleo la tatu, Saa janja ya Apple toleo la sita na saa janja ya OnePlus kwa zinavyozidiana na kukaribiana.
Duara au mraba? Utachagua kipi
Ungependela saa yako iwe na muonekano gani? Kama unapenda saa yenye umbo la duara, utabaki na chaguo kati ya Samsung na OnePlus pekee kwani Apple saa zao ni za mraba.
Wataki saa ya Apple ikiwa na ukubwa wa inch 1.73 kwa 1.50, saa ya OnePlus ina ukubwa wa inch 1.83 kwa 1.83 na Samsung ikiwa na inch 1.82 kwa 1.77 hivyo kuiacha Oneplus ikiwa ni kubwa zaidi na kumfaa ambaye anapendelea saa kubwa.
Saa janja hufanya kazi kama kisaidizi cha simu janja kwa kuonyesha meseji na kujibu simu unazopigiwa. Picha| Giphy.
Kioo ‘kinamata’ zaidi
Mbali na maumbo, Apple na OnePlus wametumia malighafi ya Sapphire kutengeneza kioo cha saa zao ambayo ni ngumu kukwaruzika. Samsung imetumia malighafi ya kioo aina ya Gorilla ambacho ni kama kinachotumika katika simu janja matoleo ya sasa.
Iwapo utazipima saa hizi kwa teknolojia, kioo cha OnePlus na Apple ni bora zaidi kwa kuwa kioo cha Samsung kinaweza kukwaruzika kirahisi endapo mtu hatoweka kinga kwa ajili ya kioo hicho almaarufu kama “protector”.
Uwezo wa kushika mtandao
Saa janja kutoka Samsung na Apple zimetengenezwa na laini ya kielektroniki ambayo mtoa huduma anaweza kuiwasha na saa ikaanza kushika mtandao. Katika hili, OnePlus wamepigwa bao.
Tovuti ya GSM Arena inayochapisha habari za teknolojia imesema saa za Samsung na Apple zina uwezo wa kushika mtandao wa 4G endapo zitawezeshwa kufanya hivyo na mtoa huduma na hivyo kuziwezesha saa hizo kuwa na uwezo wa kupiga simu hata ikiwa mbali na simu.
Soma zaidi:
- Nyeusi, nyeupe: Yanayofahamika kuhusu OnePlus 9, OnePlus 9 Pro
- Ahueni: Wapata teknolojia mpya ya kukamua mafuta ya mawese Kigoma
- VIDEO: Epuka fangasi sehemu za siri kwa kufanya haya
Zinavyopambana na vumbi na maji
Raha ya saa isikusumbue kuvua vua wakati wa kunawa mikono, kuoga na kadhalika. Kwa saa hizi, zote zina uwezo wa kutumika ndani ya maji na zinaweza kukabiliana na vumbi.
GSM Arena imeainisha kuwa saa zote zinaweza kukabili maji hadi mita 50 ndani ya maji kwa dakika 30.
Hata hivyo, kama unapenda nakshi nakshi, saa ya Samsung ina kijinakshi ambacho kinazunguka kinachoweza kutumika kama “stopwatch” kwa kuhesabu sekunde zilizotumika katika kufanya kitu iwe ni kupiga mbizi, kukimbia, kubana pumzi na kadhalika. Saa za OnePlus na Apple hazina nakshi hiyo.
Uwezo wa kukaa na chaji
Betri katika saa za kawaida huisha bila taarifa yaani utashtukia tu mishale haitembei. Lakini kwa saa janja, unao uwezo wa kuona betri likiwa limejaa, limetumika nusu na hata linapoelekea kuisha chaji.
Betri la saa ya Samsung lina uwezo wa kutunza chaji wa mAh 340 ambayo ina uwezo wa kutumika kwa siku mbili kwa mujibu wa tovuti ya Toms Guide wakati Apple ina betri lenye uwezo wa MAh 303.8 ambalo linaweza kutumika kwa saa 18, chini mara mbili zaidi ya lile la Samsung.
Kwa upande wa betri, huenda OnePlus imewapiga wote vikumbo kwa kuwa na betri lenye ukubwa wa MAh 402 ambayo inaweza kutumika kwa wiki mbili kwa mtumiaji wa kawaida na siku saba kwa aliye na matumizi makubwa huku ikihitaji dakika 45 tu kuchaji kikamilifu.

Kutoboa mifuko kupata saa yako
Licha ya kufahamu sifa zote, muhimu ni kujua kama mfuko wako unaweza kununua saa hizo. Kwa mujibu wa watengenezaji, OnePlus inapatikana kwa gharama ya Sh369,000 (bila kodi na gharama za usafirishaji), Samsung inapatikana kwa Sh765,000 na Sh925,000 kwa saa ya Apple.
Kwa pesa hiyo, utajipatia saa ambayo ina uwezo wa kupima kiwango cha hewa ya “Oxygen” katika damu, kukupatia taarifa mbalimbali zinazoingia katika simu yako, kukusaidia katika mazoezi na kukukumbusha vitu kadha wa kadha ambavyo huenda unasahau ikiwemo kujinyoosha pale unapokuwa umekaa kwa muda mrefu ofisini.
Pia, unaweza kutumia saa hizo kama rimoti kwa ajili ya televisheni na zote zinachajiwa bila waya.
Utanunua saa ipi ukienda dukani? Kazi ni kwako.