OnePlus: Simu yenye mapinduzi ya kamera kuwekwa hadharani leo
- OnePlus imeingia ubia na kampuni gwiji kwa utengenezaji wa kamera kuweka heshima katika kamera ya simu.
- Inatarajia kuchuana sokoni na matoleo mapya ya Samsung, Apple na Huawei.
Dar es Salaam. Vita ya kubuni simu bora miongoni mwa kampuni zinazozalisha simujanja ulimwenguni imezidi kuwa kubwa baada ya kampuni zinazokua kwa kasi kuendelea kuleta ushindani wa simu kali kwa bidhaa maarufu za Samsung, Apple, na Huawei.
Hivi karibuni baadhi ya kampuni zinazozalisha simu za mkononi zimezindua matoleo mapya ya simu zao ikiwemo Samsung Galaxy S21 Ultra na iPhone 12, iPhone 12 mini, iPhone 12 Pro na iPhone 12 Pro Max ambazo muundo, kamera, uhifadhi na sifa nyingine ziliacha matoleo hayo yakiendelea kuchuana sokoni.
Hata hivyo, huenda mchuano huo ukaingiliwa kati na simu mpya za kampuni ya OnePlus ambayo leo Jumanne (Machi 23, 2021) inatarajia kuzindua simu za OnePlus 9 na 9 Pro ambazo sifa yake kuu ni kamera.
Ili kuleta mapinduzi makubwa ya kamera miongoni mwa simu janja, OnePlus imeshirikiana na kampuni ya Hasselblad ambayo ni moja ya magwiji katika soko la kamera kutengeneza kifaa hicho cha kupigia picha katika simu hizo.
Soma zaidi:
- Nje, ndani: Simu mpya ya Samsung ikiingia sokoni
- Apple kuingiza sokoni simu mpya ya iPhone 12 Oktoba
- Upo tayari kununua simu ya mkononi ya zaidi ya Sh4 milioni?
Hata hivyo, picha za awali zinaonyesha simu hiyo kuwa na kamera tatu na sehemu ilipokaa kamera inataka kufanana na simu ya Oneplus Nord10 na OnePlus NordT na kidogo ina mfanano na Samsung Galaxy S21.
Simu ya awali kutoka kwa OnePlus, OnePlus 8 Pro inauzwa kwa Sh1.62 milioni sawa na iPhone 12 ambayo pia inauzwa kwa bei hiyo hiyo. Je, simu mpya zijazo zitauzwa kwa Shilingi ngapi ikiwa wakati Oneplus 8 Pro inazinduliwa Aprili 24, 2020 iliuzwa kwa Sh2.31 milioni?
Kwa mujibu wa tovuti ya habari za teknolojia ya The Verge, OnePlus inatarajia kufanya uzinduzi huo leo jioni (saa 11:00 jioni) kwa saa za Afrika Mashariki kwa njia ya mtandao ambapo mbali na simu, kampuni hiyo inatarajia kuzindua kwa mara ya kwanza saa janja (smart watch).
Kufahamu zaidi kuhusu mbivu na mbichi za simu hii, kuanzia uwezo wa kamera yake, bei, nini kipya na utofauti wake na simu zingine, endelea kutufuatilia kupitia mitandao ya kijamii @NuktaTanzania.