Infinix Smart 5A: Simu ya “kutoboa” usiku kucha

August 17, 2021 10:50 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Sifa kuu ya simu hii ni betri linalokaa kwa zaidi ya saa 24.
  • Inamfaa mtumiaji mwenye matumizi makubwa ikiwemo michezo ya mtandaoni.
  • Kwa kamera na picha bado bado sana.

Dar es Salaam. Ni vigumu kutaja makampuni yanayotengeneza simu zinazotumiwa na Watanzania na kusahau kampuni ya Infinix yenye makao makuu nchini China. 

Kwa Infinix, zinasifika kuwa na uwezo mkubwa wa kukaa na chaji ikilinganishwa na baadhi za simu zenye majina makubwa kwenye tasnia hiyo.

Agosti 2, 2021, kampuni hiyo imeingiza sokoni simu aina ya Infinix 5A ambayo sifa zake kuu ni betri linalotosha “kutoboa” usiku kucha.

Nini kipya kwa Infinix 5A

Huenda ni muendelezo wa kutafuta jina katika simu zenye uwezo wa kukaa na chaji kwa muda mrefu kwani tayari Infinix ina nafasi yake kwenye mijadala ya simu miongoni mwa Watanzania. 

Simu zinazotengenezwa na kampuni hiyo zimekuwa na uwezo wa kukaa na chaji kwa hadi saa 28 baada ya kuchajiwa.  Kwa Infinix 5A, simu hiyo ina betri yenye uwezo wa mAh 5000, uwezo ambao ni sawa na baadhi ya simu ikiwemo Samsung Galaxy S21 Ultra, Tecno Camon 17 na infinix Note 10. 

Kwa upande wa pili, simu hiyo imeziacha baadhi ya simu zenye majina makubwa ikiwemo za mwaka 2021 kama OnePlus 9 na OnePlus 9Pro (mAh4,500) na iPhone12 ya mwaka 2020 ambayo betri lake lina uwezo wa mAh3,687.

Betri la uwezo kama wa simu ya Infinix linamfaa mtu ambaye ana matumizi makubwa ya simu ikiwemo wanaocheza michezo ya video (video games) na hata kwa mfanyabiashara, inaweza kumfaa kama simu ya mawasiliano ya kiofisi kwani kwa matumizi ya wastani, betri hilo linaweza kudumu kwa siku moja na nusu.

Kila mtu ana mapendeleo yake pale anapokuwa ananunua simu. Kwa Infinix iliyojitwalia kura za ndiyo kwenye uwezo wa betri, kuna sehemu zingine ambazo simu hiyo inaweza isiwafurahishe baadhi ya watumiaji wake.

Infinix inasifika kwa betri lenye uwezo wa kudumu kwa zaidi ya saa 12. Picha| My Mobile.

Uhifadhi wa kumbukumbu

Kadri simu inavyokuwa na uwezo mkubwa wa kuhifadhi kumbukumbu za muda mfupi (RAM) ndiyo inatoa urahisi wa kuvinjali kirahisi mtandaoni. 

Kwa simu ambazo uhifadhi wa RAM ni mdogo, unaweza kutumia dakika moja kufungua programu (app) moja tu huku ukilazimika kusubiri zaidi unapofungua app nyingine.

Kifupi ni kuwa, kadri simu inapokuwa inafanya kazi nyingi kwa wakati moja, kasi yake ya kufanya kazi inapungua. Ndiyo mwanzo wa kioo cha simu kuganda (stuck).

Kwa Infinix 5A, uwezo wake wa uhifadhi ni mdogo. Ina uhifadhi wa GB 2  ikilinganishwa na Infinix Note 10 (GB4), Samsung A52 (GB6) na Tecno Camon 17 (GB6).

Uwezo wa uhifadhi wa jumla (ROM), uhifadhi ambao unatunza picha, muziki, meseji, apps na hata video ni wa GB4 ambao kwa matumizi ya kawaida, inaweza kufaa japo kwa mtu anayetengeneza maudhui ya video, atalazimika kuwa na mifuulizo ya kufuta baadhi ya video.

Hata hivyo, kwa simu ya Infinix, unaweza kuongeza uwezo wa uhifadhi kwa kuwa ina sememu ya kuweka kadi ya kumbukumbu ya hadi GB256.

Uwezo wa kamera

Ikilinganishwa na baaadhi ya simu tulizozifanyia uchambuzi ambazo ni za uchumi wa kati ikiwemo Samsung A52 na Tecno Camon 17, Infinix 5Aimepigwa kikumbo kwa kiasi fulani.

Kwa muktadha huo,  Simu ya Samsung A52 ni bora zaidi kuliko infinix 5A kwa uwezo wa kamera licha ya kuzidiwa uwezo wa betri na Infinix.

Mengineyo

Skrini ya Infinix 5A ina ukubwa wa inchi 6.52 ambayo ni kubwa kuliko Galaxy A52 japo ni dogo ikilinganishwa na Tecno Camon 17 na Infinix Note 10.

Simu hii inaweza kutumia usalama wa neno siri (password), namba za msimbo (Pin) na pia kufunguliwa kwa kuskani sura (Facial unlock).

Kwa mtu ambaye anahitaji simu kwa ajili ya  mawasiliano na inayokaa na chaji kwa muda mrefu, simu hii itamfaa.

Simu gani nyingine tukusaidie kuinyambua? Wasiliana nasi kupitia mitandao ya kijamii @NuktaTanzania au WhatsApp kupitia namba +255 677 088 088. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW