Kicheko: Serikali yazidi kuondoa maumivu mikopo elimu ya juu Tanzania
- Serikali yaondoa asilimia 10 iliyokuwa inatozwa kwa wanufaika waliochelewa kuanza kulipa mkopo.
- Tozo ya asilimia sita kulinda thamani ya mkopo nayo yaondolewa.
- HESLB yaendelea kuwabana wanufaika urejeshaji mikopo.
Dar es Salaam. Wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu Tanzania wameanza mwezi Mei kwa neema zaidi kutokana na kuendelea kupunguziwa maumivu baada ya Serikali kutangaza kuondoa asilimia 10 ya faini kwa wale wanaochelewa kuanza kurejesha fedha hizo.
Hii ni hatua ya pili kuchukuliwa na Serikali ndani ya siku nne kutokana kuwepo na vilio vya wanufaika wa mikopo hiyo ambayo hutolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi Elimu ya Juu ya Tanzania (HESLB).
Mapema wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani Mei Mosi mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza kuondolewa kwa tozo ya asilimia sita (Value Retention Fee) iliyokuwa inatozwa kwa ajili ya kulinda thamani ya fedha katika urejeshaji wa mkopo huo muhimu katika kukuza elimu ya juu nchini.
Mbali na tozo hiyo, wanufaika waliochelewa kufanya marejesho baada ya muda wa ahueni kupita walikuwa wakitakiwa kulipa faini ya asilimia 10 ya thamani ya mkopo husika.
Kwa mujibu wa utaratibu wa HESLB, mnufaika anatakiwa kuanza kulipa mkopo wake ndani ya miaka miwili na endapo muda huo utapita bila kulipa anaanza kutozwa asilimia 10 ya kuchelewesha malipo.
Hata hivyo, leo wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ameliambia Bunge jijini Dodoma kuwa Serikali inaondoa tozo ya adhabu ya asilimia 10 ya mkopo ambayo inatozwa kwa wanufaika wanaochelewa kulipa mikopo hiyo.
“Serikali inaiagiza Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kuondoa pia tozo ya adhabu ya asilimia 10 ya mkopo ambayo inatozwa kwa wanufaika wanaochelewa kulipa mikopo hiyo,” amesema Prof Ndalichako.
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika moja ya shughuli ya chuo hicho mbele ya ukumbi wa Nkurumah. Picha| Mtandao.
Prof Ndalichako amesema tozo ya asilimia 6 ya kulinda thamani ya fedha katika urejeshaji wa mkopo itaondolewa rasmi Julai 1, 2021 wakati wa kuanza kwa mwaka mpya wa fedha.
Hata hivyo, Serikali imesema itaendelea kutoza kiwango cha asilimia 15 ya mishahara ya wanufaika walioajiliwa na Sh100,00 kwa wasio na ajira kila mwezi ili kurejesha mikopo hiyo.
Kiwango hicho cha asilimia 15 kimekuwa kikilamikiwa na wadau mbalimbali wakieleza kuwa ni kikubwa ikilinganishwa na kipato cha wahitimu wengi wa vyuo vikuu na kutaka Serikali ipitie upya ili kuwapatia ahueni.
Zinazohusiana:
- HESLB kuboresha mfumo wa utoaji, urejeshaji mikopo elimu ya juu.
- Wanafunzi 25,532 wapata mikopo awamu ya kwanza
HESLB yaimarisha ukusanyaji mikopo
Wakati Serikali ikitoa hiyo kwa wanafuika wa mikopo elimu ya juu, HESLB nayo imezidi kujiimarisha kuwafuatilia wanafaika waliohitimu masomo ya vyuo vikuu ili wareje mikopo waliyotumia wakiwa masomoni.
Prof Ndalichako amesema katika mwaka wa fedha 2020/21, HESLB imekusanya Sh139.3 bilioni ikiwa ni asilimia 72 ya lengo la kukusanya Sh194.1 bilioni ya mikopo iliyoiva.
Fedha hizo zimekusanywa kati ya Julai mwaka jana hadi kufikia Machi, 2021.
Amesema pia wanufaika wapya 14,807 wametambuliwa na kupewa ankara zao kurejesha mkopo ili kuwawezesha wanafunzi wanaosoma kupata mikopo wakiwa vyuoni.
“Aidha, ukaguzi umefanyika kwa waajiri 3,979 na taarifa za mkopo zimehuishwa kwa wanufaika 321,629 kupitia kwa waajiri wao,” amesema Ndalichako katika hutuba yake.
Katika kuongeza ufanisi wa urejeshaji wa mikopo, HESLB imeanzisha mfumo rahisi wa kidigitali wa urejeshaji mikopo (Loanee Individual Permanent Account – LIPA) ambao unamuwezesha mnufaika au mwajiri kupata taarifa za deni na utaratibu wa kulipa kutoka popote alipo.
Latest
