Corona ilivyoshusha ukuaji wa uchumi Tanzania hadi asilimia 4.8 mwaka 2020

June 10, 2021 8:19 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Licha ya hali ya uchumi ya nchi nyingi duniani kukua kwa kiwango hasi, uchumi wa Tanzania umekuwa kwa kiwango chanya.
  • Ukuaji huo umechangiwa na sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya habari na mawasiliano. 
  • Hata hivyo shughuli mbalimbali ikiwemo shughuli za malazi na sanaa ziliathirika.

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema uchumi wa Tanzania ulikuwa kwa kasi ya wastani wa asilimia 4.8 mwaka 2020 kutoka ukuaji wa wastani wa asilimia 7 mwaka 2019, ukiathiriwa zaidi na ugonjwa wa virusi vya corona (Uviko-19) unaoendelea kuathiri mataifa mbalimbali ulimwenguni. 

Kasi hiyo ya ukuaji wa uchumi mwaka 2020, ipo chini na matarajio ya awali ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya ukuaji wa asilimia 5.5. Kwa takriban muongo mmoja sasa ukuaji wa uchumi katika taifa hilo la Afrika Mashariki ulikuwa ukikua kwa wastani wa asilimia 7. 

Dk Nchemba amelieleza Bunge jijini Dodoma leo (Juni10, 2021) wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa taifa ya mwaka 2020 na mpango wa maendeleo mwaka 2021/22 kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache ambazo uchumi wake umekuwa kwa kiwango chanya licha ya mlipuko wa Uviko-19.

“Licha ya mlipuko wa Uviko 19 Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zilizokuwa na ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2020 uliokuwa chanya. Pato la taifa la Tanzania lilikua kwa asilimia 4.8% ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7% wa mwaka 2019,” amesema Dk Nchemba. 

Waziri huyo ameainisha kuwa, pato ghafi la Taifa lililozalishwa nchini lilikuwa Sh148.5 trilioni mwaka 2020, ikilinganishwa na Sh139.6 trilioni mwaka 2019 huku idadi ya watu Tanzania Bara ikikadiriwa kuwa watu milioni 55.9, ikilinganishwa na watu milioni 54.2 mwaka 2019.

Dk Nchemba amesema uchumi wa Tanzania ulikuwa kwa kasi ya wastani wa asilimia 4.8 mwaka 2020. Picha| Dk Nchemba.

Kiongozi huyo ameeleza kuwa wastani wa pato kwa mtu lilikadiriwa kufikia Sh2.6 milioni sawa na Dola za Marekani 1,151 kwa mwaka 2020 ikilinganishwa na Sh2.5 milioni sawa na dola za marekani 1,118.9 kwa mwaka 2019. Ongezeko hilo la wastani wa pato la mtu kwa mwaka ni sawa na ongezeko la asilimia 3.1.

Hata wakati uchumi wa Tanzania ukikua, baadhi ya shughuli zinazofanywa na Watanzania zilidorola kutokana na ugonjwa wa Uviko-19 ambao ulilazimisha watu kuchukua tahadhari mbalimbali ikiwemo kujitenga, kufunga ofisi na kadhalika.

Dk Nchemba amesema athari za janga la Uviko-19 zilijitokeza zaidi katika shughuli za kiuchumi za malazi, huduma ya chakula pamoja na sanaa na burudani ambazo zilikuwa na ukuaji hasi kwa mwaka 2020. 

Hata hivyo, sekta zilizokua kwa viwango vya juu kwa mwaka 2020 ni pamoja na sekta ya Ujenzi (9.1%), habari na Mawasiliano (8.4%), uchukuzi na Uhifadhi wa Mizigo (8.4%) na huduma zinazohusiana na Utawala zilizokuwa kwa wastani wa 7.8.

Shughuli zingine ni pamoja na shughuli za Kitaalamu, Sayansi na Ufundi (7.3%), madini na Mawe (6.7%) pamoja na afya na huduma za Jamii (6.5%).

Hali ya uchumi duniani na kikanda

Licha ya uchumi wa Tanzania kukua, hali haikuwa sawa kwa nchi nyingine Afrika na duniani baada ya kuathiriwa na uviko-19.

Dk Nchemba amesema, kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ya Aprili 2021, dunia ilikuwa na mdororo wa uchumi kwa kupata ukuaji hasi wa 3.3% ikilinganishwa na ukuaji chanya wa 2.8% wa mwaka 2019.

“Ukuaji hasi ulisababishwa na kupungua kwa shughuli za kiuchumi duniani hususan biashara, usafirishaji, na utalii kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Uvico 19,” amesema Dk Nchemba.

Hata hivyo, uchumi wa dunia unatarajiwa kuimarika na kufikia ukuaji wa asilimia 6 mwaka 2021 na asilimia 4.4 mwaka 2022 ikiwa ni matokeo ya kurejea kwa shughuli za kiuchumi kutokana na kusambazwa kwa chanjo ya Uviko-19 na hatua za kuinua uchumi zinazochukuliwa na nchi mbalimbali.

Kwa upande wa uchumi wa Afrika na kikanda, nchi za kusini mwa jangwa la Sahara pia zilikuwa na ukuaji hasi wa uchumi wa wastani wa 1.9% ikilinganishwa na ukuaji chanya 3.2 kwa mwaka 2019.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW