Biashara, sanaa ya uchoraji inavyochukua mkondo mpya Tanzania
- Ni baada ya wachoraji wa grafiki za mtandaoni kushika kasi.
- Wadau wa kazi zao zamani wamesema kazi za grafiki zina uhalisia.
- Wachoraji washauriwa kutumia teknolojia ya kisasa ili wabaki sokoni.
Dar es Salaam. Kabla ya programu za kompyuta kufahamika na watu wengi, wachoraji wa michoro na maandishi mbalimbali walikuwa wakifaidika zaidi na kazi za sanaa ya mkono ikiwemo kujipatia kipato cha kuendesha maisha.
Maduka, ofisi na sehemu za starehe na biashara zilipambwa na wadau wa sanaa waliotumia mikono yao kuchora maandishi, picha na hata alama mbalimbali katika kuta, mageti na mabango ya matangazo.
Hata hivyo, mambo yamebadilika kwa sababu matumizi hayo kazi za sanaa kwenye ofisi na biashara yamepungua kutokana na mabadiliko ya teknolojia yaliyowaibua wabunifu wa grafiki (graphic designers).
Wabunifu hao wanatumia programu za kompyuta kubuni na kutengeneza michoro na maandishi ambayo huchapishwa kwenye mabango ya ofisi au biashara za watu.
Mbunifu wa grafiki kutoka Kampuni ya Mayocoo, Innocent Joseph ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa kwa sasa watu wengi huchagua kazi za matangazo zilizobuniwa badala ya zilizochorwa kwa sababu kila mtu anahitaji kwenda na wakati.
Joseph anasema wachoraji wameathirika na teknolojia mpya kwa sababu kila kukicha mwanadamu anatafuta urahisi na njia nzuri ya kufanya jambo ili kukidhi mahitaji ya wateja wake.
“Teknolojia inabadilika kila siku, hata sisi wabunifu wa grafiki tuna kazi ya kujifunza mifumo mipya kila siku kwani ukizubaa tu unaachwa,” amesema Joseph.
Kabla ya teknolojia ya kompyuta kuwa maarufu, matangazo,picha na mabango yalichorwa na wachoraji kwa mkono na kalamu. Picha|Furaha Mwakitalu.
Kwanini grafiki badala ya kuchora?
Kila jambo hufanyika huku nyuma yake kukiwa na sababu. Kwa wafanyabiashara wa zamani, kuchora ndiyo ilikuwa habari ya mjini lakini kwa sasa, hali imebadilika kwani wengi wanahitaji mabango yaliyosanifiwa kwa programu za kompyuta.
Muuzaji wa mgahawa maeneo ya Mwananyamala mkoani Dar es Salaam, Rahma Shayo anasema ujio wa matangazo ya grafiki umekuwa ni ahueni kwa sababu umekuja na picha za uhalisia kuliko sanaa ya kuchora.
Mama lishe huyo anasema wachoraji aliowapa kazi hawajawahi kufanya kazi vizuri katika upande wa matangazo ya chakula na hata matangazo mengine.
“Unamwambia mtu nichoree chipsi na mishikaki hapa, baba kinachochorwa hata ukipita huwezi kusema hizo ni chipsi wala mishikaki lakini ukisema utoe Sh100,000 yako utengeneze bango chipsi inaonekana ni chipsi na tomato ni tomato sio uji,” anasema Shayo.
Sababu nyingine ni watu kwenda na wakati na kuachana na michoro ya rangi kwenye kuta ambayo inaonyesha ishara ya kuwarudisha nyuma.
Fundi cherehani wa Tabata Kinyerezi jijini hapa, Patrick Sande anasema matangazo ya kuchora yalikuwa ni zamani lakini kwa sasa siyo dili tena kutangaza baadhi ya biashara.
Anasema picha humvutia mteja hata kuingia ofisini kuona unachofanya na mara nyingi, picha zenye uhalisia ndiyo zinafanya hivyo.
“Kumpata mchoraji akakuchorea mtu aliyevaa suti kama unayoiwaza kichwani au iliyopo kwenye picha ni karibu na hakuna,” anasema fundi huyo.
Sande ambaye ameshona nguo kwa zaidi ya miaka 10 anasema kwa sasa matangazo ya grafiki huvutia wateja wengi zaidi kwani ni nadhifu na yanahamishika pale unaobadilisha ofisi.
“Ofisi yangu ya Kimara hadi leo ina picha ya tangazo kuwa ninashona suti. Nimehama sasa mwaka wa tatu lakini tangazo lipo, nimekuja huku imebidi nigharamike tangazo lingine,” anasema Sande na kubainisha kuwa matangazo ya grafiki huonekana hata usiku kwani yanaweza kuwekewa taa.
Uchoraji umewapatia watu ajira ba kuwakwamua vijana kiuchumi. Picha| Nelson Makamo.
Ni nini hatma ya wachoraji?
Hata wakati ubunifu wa grafiki ukichukua enzi za uchoraji, bado wadau wa sanaa ya penseli, brashi na rangi hawajaona hali hiyo kama mwisho wao.
Mdau wa sanaa ya uchoraji wa jijini Dar es Salaam, Furaha Mwakitalu, anasema haiwezi kuisha kwani kila siku mahitaji ya sanaa hiyo yanaendelea kukua.
Mwakitalu amesema ni kweli wafanyabaishara wengi wameachana na matangazo ya kuchorwa kwa mikono lakini hiyo imeibua fursa za uchoraji wa picha za penseli na za rangi almaarufu kama “portrait photos”.
“Hawana budi kujifua upya, tusikatae kuwa dunia na mahitaji ya sanaa yanabadilika hivyo ni muda wa kutafuta zana za teknolojia za wana sanaa na kuanza kazi,” anasema Mwakitalu.
Mchoraji huyo amesema kwa kufanya hivyo siyo tu watashindana na wabunifu wa grafiki bali watakuwa na nafasi ya kufanya kazi pamoja nao kwani zipo kazi ambazo wabunifu wa grafiki wanahitaji michoro ya kidijital.
Wachoraji wanatakiwa kuwekeza zaidi kwenye teknolojia hasa katika uchoraji wa kidijitali unatumia kompyuta za kisasa ili kurahisisha kazi zao.
Mchoraji Sise Christopher anasema kwa kawaida ili kazi za kuchora za kidijitali zifanyike vizuri, unahitaji kompyuta maalumu ambayo skrini yake ni kubwa kuwezesha uchoraji.
“Ni kama karatasi lakini ya kidijitali inakuwa na peni yake maalumu ambayo unaweza kuchora kwa uzuri kabisa kama kwenye karatasi,” anasema Christopher akibainisha kuwa bei ya mashine hiyo imechangamka kidogo.
Katika soko la mtandaoni la Amazon, mashine hiyo inauzwa kwa Sh1.1 milioni.
Wachoraji wanaweza kuhamishia sanaa zao kidijitali kwa kutumia bidhaa zana maalumu. Picha| Supportive Guru.
Changamoto za kazi ya grafiki
Hata wakati dunia ikigeukiwa fani ya grafiki, bado yapo mambo mbalimbali ambayo hayajakaa sawa kwa wabunifu wake ikiwemo matumizi ya teknolojia na malipo yatokanayo na kazi zao.
Licha ya umuhimu wa kazi hiyo, baadhi ya vijana wanalalamikia malipo duni yatokanayo na kazi za grafiki kwa sababu hazithaminiwi kama zilivyo kazi zingine, jambo linalowafanya wasipate malipo yanayokidhi mahitaji yao.
“Kwa kiwango cha chini, ninaweza kufanya kazi sita mpaka 10 kwa mwezi hivyo kwa mwaka ninaweza kufanya kazi 92 na wateja wale wale na wapya,” amesema Joseph ambaye ana uhakika wa Sh3.3 milioni kwa mwaka.
Joseph ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa kazi za sanaa bado hazithaminiwi na hivyo malipo yake bado yako chini.
Katika sehemu ya pili ya makala haya, tutaangazia kwa undani mambo ya kuzingatia unapoamua kuifanya sanaa ya uchoraji kama kazi ya kukuingizia kipato. Endelea kubaki na Nukta Habari.
Latest



